Makala

GWIJI WA WIKI: Timothy Sumba

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

UANDISHI ni bahari pana iliyo na mawimbi chungu nzima.

Wanaoazimia kujitosa katika ulingo huu hawana budi kuupalilia sana usomaji wao, kuongozwa na nidhamu na kujiruhusu kutawaliwa na ari ya kutunga miswada bora.

Bidii, usiri, uwajibikaji, stahamala na kujiamini ni sifa muhimu na za lazima kwa mwandishi yeyote kuwa nazo ili afanikiwe kitaaluma.

Salia imara katika jitihada za kufikia malengo yako, uwe mtu anayewajali wengine na mwaminifu katika shughuli zako. Ladha ya maisha haiwezi kukolea sawasawa kabisa usipokuwa na marafiki wa dhati.

Furaha na ustawi wa mwanadamu siku zote umejengeka katika msingi wa kutegemeana, kuhitajiana na kuchangiana mawazo.

Ukamilifu katika maisha hutegemea mchango wa marafiki wanaokuzunguka, si wanafiki ambao kubwa zaidi katika mipango yao ni kuzima maono na ndoto zinazotawala fikra zako!

Huu ndio ushauri wa mhariri na mwandishi Timothy Omusikoyo Sumba ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya Carlin, Donholm, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Omusikoyo alizaliwa mnamo Oktoba 5, 1974, kijijini Ebubule, kata ya Eshikalame, Mumias katika Kaunti ya Kakamega akiwa mwanambee katika familia ya watoto sita wa Bw Moses Sumba Simatwa na marehemu Bi Salome Anyango.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Kitale Union.

Alihamia baadaye Eshikalame kisha Shule ya Msingi ya Ingusi, Mumias alikofanyia KCPE mwishoni mwa 1991.

Mnamo 1992, alijiunga na Shule ya Upili ya Kitale kisha St Bedas Bukaya, Mumias kabla ya kuhamia Kisumu High.

Alifanya KCSE mnamo 1995.

Mjomba wake, Bw Pius Wamukoya, alimtafutia kazi ya ukarani katika kampuni ya East African Industries, eneo la Shimanzi, jijini Mombasa mnamo 1996.

Aliifanya kazi hiyo ya uhazili kwa muda mfupi kabla ya mshawasha wa kuwa mwalimu wa Kiswahili kwa lengo la kuwasambazia wengine ubora anaojivunia katika lugha hiyo kujenga kiota kikubwa ndani ya moyo na nafsi yake.

Alirejea Mumias mnamo 1997 na kuwa Mwalimu Msaidizi katika shule za Ingusi, Musanda na hatimaye Eshikalame alikofundisha Kiswahili na somo la Biashara.

Alijiunga na Chuo cha Walimu cha Baraka, eneo la Tarime mnamo 2002 na kuhitimu mwishoni mwa 2005.

Mwaka mmoja baadaye, ilhamu ya kujiendeleza zaidi katika Kiswahili na hatimaye kuupanua wigo wa kitaaluma ilimchochea kujiunga na International Correspondence School (ICS), Kakamega kusomea uanahabari hadi mwishoni mwa 2008. Ualimu na uanahabari ni taaluma zilizomvutia sana tangu utotoni.

UALIMU

Tangu ajitose kikamilifu katika ulingo wa ualimu mnamo 1997, Omusikoyo amefundisha Kiswahili katika shule nyingi za umma na za kibinafsi. Baadhi ya shule hizi ni Musanda, Ingusi, Shikalame, Etenje, Ugana, Mumias Muslim na Fesbeth Academy, Kaunti ya Kakamega.

Anakiri kwamba ilikuwa tija na fahari tele kufundisha baadaye katika darasa moja na waliokuwa walimu wake wa awali, Bw Richard Mage (Eshikalame) na Bw John Mukabana (Ingusi).