Makala

Haki ya umiliki wa mali katika ndoa ya njoo tuishi

Na BENSON MATHEKA September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Nchini Kenya kwa wakati huu, dhana ya ndoa ya kudhaniwa na haki za umiliki wa mali ni vipengele muhimu vya sheria ya familia vinavyoathiri maisha ya wapenzi wengi, hasa wale wanaoishi pamoja bila ndoa rasmi.

Sheria kama vile Sheria ya Urithi na Sheria ya Mali ya Ndoa ya 2013 zinatoa mwongozo kuhusu jinsi mali inavyomilikiwa, kugawanywa au kurithiwa katika muktadha wa ndoa ya kudhaniwa.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 96 cha Sheria ya Ushahidi, mwanamume na mwanamke walio kwenye uhusiano wa kuishi pamoja kama mume na mke kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi huchukuliwa kuwa wameoana. Kisheria, hii inajulikana kama ndoa ya kudhaniwa au kwa lugha ya mtaa, njoo tuishi.

Uhusiano huo, ingawa si ndoa rasmi kisheria (kama vile ndoa ya kanisani au ya serikali), unaweza kutambuliwa na mahakama kuwa ndoa kwa misingi ya mwenendo wa wahusika, hali ya kuishi pamoja, na namna wanavyojitambulisha kwa jamii.

Sheria ya Mali ya Ndoa ya 2013 inaeleza kwamba mali yoyote inayopatikana wakati wa ndoa ni mali ya pamoja, bila kujali nani aliinunua au jina la nani lipo kwenye hati miliki. Hii inamaanisha kuwa kila mmoja kati ya wanandoa ana haki ya asilimia 50 ya mali hiyo.

Hata hivyo, sheria hii inahusu ndoa zilizosajiliwa tu, chini ya Sheria ya Ndoa ya Kenya.

Je, ndoa ya kudhaniwa inaathiri vipi umiliki wa mali?

Iwapo wanandoa wameishi pamoja kwa zaidi ya miaka miwili na wanachukuliwa kuwa wameoana kwa kudhaniwa, basi mali waliyoipata pamoja inagawanywa sawa (50/50) wanapotengana, kuachana au mmoja wao kufariki.

Kwa mfano, iwapo walinunua nyumba au gari wakati wa kuishi pamoja, kila mmoja ana haki ya nusu ya mali hiyo  hata kama mali hiyo ilisajiliwa kwa jina la mtu mmoja tu.

Iwapo hawatambuliwi kuwa wameoana, basi mali inaweza kugawanywa kwa misingi ya sheria ya urithi, ambayo mara nyingi haimpi mwenza aliyebaki hai kipaumbele, hasa kama hakuna wosia.

Kama mwenza mmoja atafariki bila kuandika wosia, na wanatambuliwa kuwa walikuwa kwenye ndoa ya kudhaniwa, basi yule aliyebaki hai ataweza kurithi asilimia 50 ya mali. Asilimia nyingine itagawanywa kwa warithi wengine kulingana na sheria ya urithi.

Iwapo familia au mahakama haitambui uhusiano huo kama ndoa, huenda mwenza aliyebaki akakosa haki ya kurithi chochote, hasa pale ambapo mali hiyo ilisajiliwa kwa jina la marehemu pekee.

Kuelewa dhana ya ndoa ya kudhaniwa na haki za mali ni jambo la msingi kwa wapenzi wanaoishi pamoja bila ndoa rasmi. Kutofahamu sheria hizi kunaweza kusababisha hasara kubwa ya mali au migogoro isiyo ya lazima iwapo uhusiano utavunjika au mmoja kufariki.

Kama unaishi na mwenzi wako kwa zaidi ya miaka miwili, zingatia kusajili ndoa yenu rasmi ili kuimarisha ulinzi wa kisheria.Andika wosia ili kuhakikisha mali yako inagawanywa kwa njia unayopendelea.Tafuta ushauri wa kisheria mapema ili kulinda haki zako na za familia yako.