Makala

Hali ngumu sikukuu, utafiti mpya wa Benki Kuu ukionyesha bei ya nyanya, maziwa na vitunguu pia inaongezeka

Na BENSON MATHEKA December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JAPO bei ya mafuta ya petroli ilipungua mwezi huu, sukari na mafuta ya kupikia ni baadhi ya bidhaa za chakula ambazo zitapanda bei katika msimu huu wa siku kuu.

Hii ni licha ya gharama ya maisha kuwa asilimia 2.8 mwezi Novemba.Utafiti wa Sekta ya Kilimo wa Novemba 2024 uliochapishwa na Benki Kuu ya Kenya pia unaorodhesha nyanya miongoni wa bidhaa zitakazokuwa ghali ikitaja mvua ya Oktoba-Desemba kuwa chanzo.

Utafiti huo unabainisha kuwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilipanda kuanzia Novemba na kubebesha familia gharama ya ziada wakati wa msimu wa sikukuu.

Bidhaa hizo ni pamoja na unga wa mahindi, unga wa ngano, sukari, sukuma wiki na mchicha.Katika kipindi hicho, bei ya mahindi mabichi, aina fulani ya mchele, ndengu, maharagwe, maziwa, kabichi na vitunguu ilishuka.

Kupanda kwa bei za vyakula vilivyotajwa kumehusishwa na athari za uchumi na mvua za Oktoba-Desemba.’Bei za sukari na mafuta ya kupikia, zinatarajiwa kuongezeka kidogo Desemba 2024.

Hii inatokana na soko la kimataifa ambapo bei za bidhaa hizi zimekuwa zikiongezeka katika miezi ya hivi karibuni,’ utafiti huo unasema.Utafiti ulishirikisha wakazi wa Nairobi na viunga vyake, Nakuru, Gilgil, Mombasa, Eldoret, Kitale, Nyandarua, na Bomet.

“Wengi wanatarajia kuongezeka kwa bei ya nyanya kwani usambazaji unaweza kuathiriwa na msimu wa mvua wa Oktoba-Desemba 2024,”utafiti unasema.Ongezeko linalotarajiwa la bei ya nyanya kwa kiasi kikubwa linachangiwa na sababu za msimu kwani usambazaji wa nyanya hupungua wakati wa mvua na huongezeka wakati hali ya ukame inapoanza.

Utafiti unaeleza kuwa bei za aina nyingi za mchele zinatarajiwa kusalia tulivu ingawa bei itapanda kwa baadhi yake. Unasema mchele ni miongoni mwa bidhaa za chakula ambazo bei zake kwa ujumla zimekuwa afueni kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na uzalishaji wa ndani na uagizaji kutoka nje.Bei ya maziwa pia imekuwa tulivu kutokana na hali nzuri ya hewa ambayo imeboresha malisho.T

akwimu za hivi punde kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS) zinaonyesha kiwango cha mfumuko wa bei cha Novemba kilikuwa asilimia 2.8.Bei ya sukari, unga wa mahindi, mafuta ya kupikia, nyanya zilipanda hali inayoelezea ongezeko kidogo la mfumuko wa bei kutoka asilimia 2.7 mwezi Oktoba hadi asilimia 2.8.