Hali tete ghasia zikizuka uchaguzini Tanzania
HALI ilikuwa tete Tanzania, ghasia zilipozuka jana nchini wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kumrejesha madarakani Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya wagombea wakuu wa upinzani kuzimwa kushiriki.
Kulingana na kundi la ufuatiliaji wa mtandao NetBlocks, huduma za intaneti zilikatwa kote nchini huku video ambazo hazijathibitishwa zikionyesha vijana wakirushia mawe maafisa wa usalama na kituo cha mafuta kikiteketea zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mashahidi waliripoti maandamano yaliyokumbwa na vurugu katika angalau mitaa minne ya jiji la Dar el Salaam, ikiwemo Kimara, Ubungo, Magomeni, Kinondoni na Tandale, huku polisi wakitumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Ubalozi wa Amerika nchini humo ulitoa taarifa ya tahadhari kuhusu usalama, ukisema kuwa maandamano yalienea maeneo kadhaa nchini.
Uchaguzi huu umefanyika bila ushiriki wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, ambacho kiongozi wake Tundu Lissu yuko gerezani akikabiliwa na mashitaka ya uhaini, madai anayokana. Tume ya uchaguzi iliondoa chama hicho Aprili mwaka huu baada ya kukataa kutia saini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Vilevile, mgombeaji urais wa chama cha pili kwa ukubwa cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, alipigwa marufuku kufuatia pingamizi lililotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na hivyo kumwachia Rais Hassan kushindana na wagombeaji kutoka vyama vidogo pekee.
“Hakuna uchaguzi Tanzania. Ni sherehe ya kutawazwa,” alisema Deogratius Munishi, katibu wa masuala ya kigeni wa CHADEMA, akizungumza na Citizen TV.
Serikali imesisitiza kuwa uchaguzi unafanyika kwa haki na imekanusha madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo kutoweka kwa viongozi wa upinzani.
Uchaguzi uliendelea pia katika visiwa vya Zanzibar, ambapo wapigakura wanachagua rais wa eneo hilo na wabunge. Hata hivyo, idadi ya wapiga kura ilionekana kuwa ndogo, hasa miongoni mwa vijana.
Baada ya kupiga kura katika mji mkuu wa kiutawala Dodoma, Rais Hassan aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kupiga kura.
“Naomba Watanzania wote walioko nyumbani wajitokeze na kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema Rais Hassan, ambaye anawania muhula wake wa kwanza kamili madarakani.
Rais huyo, ambaye ni mmoja wa viongozi wanawake wawili pekee barani Afrika, alipongezwa mwaka 2021 alipoingia madarakani kwa kulegeza misimamo mikali ya kisiasa iliyokuwepo chini ya mtangulizi wake John Pombe Magufuli, aliyefariki ghafla mwaka huo. Hata hivyo, katika miaka miwili iliyopita, mashirika ya haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani wameishutumu serikali yake kwa visa vya kutekwa kwa wakosoaji na kukamatwa kiholela.
Mwezi huu, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba — ambaye sasa ni mkosoaji mkubwa wa serikali — aliripotiwa kutekwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana. Polisi walisema wanachunguza tukio hilo, huku ripoti rasmi zikiwa bado hazijatolewa.
Shirika la Amnesty International limesema mazingira ya uchaguzi yamegubikwa na hofu, likithibitisha visa vya watu kutoweka kwa lazima, kukamatwa kiholela na hata mauaji nje ya sheria, likionya kuwa hatua hizo zinadhoofisha uhalali wa uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ilithibitisha kuwa upigaji kura wa awali wa maafisa wa usalama na watumishi wa uchaguzi siku ya Jumanne ulifuata sheria, ingawa chama cha ACT-Wazalendo kililalamika kuhusu udanganyifu, ikiwemo wapigakura bandia waliodaiwa kujifanya maafisa wa usalama.
Wakati huo huo, Kamishna wa Wilaya ya Dar es Salaam, Alfred Chalamila, aliwaonya wale alioita “wavurugaji wa amani” kwamba maafisa wa usalama wako tayari kuchukua hatua kali.
“Tanzania haitapoteza utamaduni wake wa muda mrefu wa amani,” alisema Chalamila.
Zaidi ya wapigakura milioni 37 wamesajiliwa kushiriki uchaguzi huu — ongezeko la asilimia 26 tangu mwaka 2020 — lakini wachambuzi wanaonya kuwa idadi ndogo wa wapigakura huenda ikaendelea kutokana na mtazamo kwamba Rais Hassan atashinda kwa urahisi.
Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa kumi jioni na matokeo ya awali yanatarajiwa ndani ya saa 24, huku tume ikiwa na hadi siku saba kutangaza matokeo rasmi.
Taharuki ilitanda katika Kituo cha Mpaka wa Namanga jana, baada ya maafisa wa Polisi Tanzania (TPF) kuweka doria kali kuzuia watu kuvuka mpaka kuelekea nchini humo, kufuatia vurugu za uchaguzi zilizoshuhudiwa siku nzima.
Idadi kubwa ya maafisa wa TPF walionekana wakilinda maeneo ya mpaka, hali ambayo ilisababisha shughuli nyingi za kibiashara kukwama.
Mashahidi walisema polisi wa Tanzania walionekana wakiwaonya wafanyabiashara wa nchi hiyo kwa nguvu kufunga maduka yao ili kwenda kupiga kura.
Hata hivyo, wafanyabiashara wengi walikaidi maagizo hayo na kuendelea na biashara zao, huku vijana wachache wa Kenya wakionekana kuwaunga mkono na kutishia kuandamana.