Hamasa dhidi ya pombe na dawa za kulevya ifanywe nyakati zote, si madhara yanapojiri
Na SAMMY WAWERU
ALIYEKUWA mwenyekiti wa shirika la kitaifa kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya, mihadarati na kudhibiti vileo (Nacada) John Mututho amekuwa katika mstari wa mbele kupambana na unywaji wa pombe nchini.
Pombe hasa ile haramu imekuwa kero katika baadhi ya maeneo nchini na Bw Mututho amekuwa kidedea dhidi ya vileo vya aina hiyo.
Mwanasiasa huyo, wakati akiwa mbunge alibuni sheria maalum zinazodhibiti mabaa na vilabu vinavyouza vileo. Kwenye Mututho Laws, mojawapo ilikuwa; maeneo yote ya kuuza pombe yahudumu kati ya saa kumi na moja za jioni hadi tano usiku.
Ni sheria ambazo zilionekana kushika kasi na kuzaa matunda lakini kasi hiyo sasa ni kitendawili. Baadhi ya mabaa yanahudumu mchana peupe, kuanzia asubuhi hadi asubuhi ya siku inayofuata.
Vijana na wazee wamekuwa mateka wa pombe, wanaishia kusahau majukumu yao katika jamii na isitoshe jasho lao takriban lote wanalielekeza kwenye mabaa na vilabu.
Wengi wao wameishia kulia na kusaga meno, wengine wakipoteza maisha yao kupitia unywaji wa pombe. Ni muhimu kukumbusha kuwa pombe ina madhara yake kiafya, kama vile kusababisha ugonjwa hatari wa Saratani.
Wakati mmoja hapa nchini, kisa cha waraibu kupoteza uwezo wa kuona kiliripotiwa, waathiriwa wakinukuliwa; “Hata mkizima mataa tutaendelea kunywa.”
Ni kauli yenye ucheshi, lakini yenye madhara yake.
John Mututho, ambaye alikuwa mbunge wa Naivasha kwa hakika ni mzalendo anayependa taifa hili tukufu la Kenya.
Uzalendo wake ulimchochea kuanzisha kituo cha kurekebisha tabia na maadili kwa mateka wa pombe na dawa za kulevya, kinachojulikana kama John Mututho Empowerment Center (Jomec) na kilichoko Nakuru.
Licha ya jitihada za kiongozi huyo, kuna mengi yanayohitaji kufanywa ili Kenya ijivunie kupambana na suala la dawa za kulevya na pombe kikamilifu.
Imekuwa mazoea hatua kuchukuliwa hasara inapojiri, na kuangaziwa na vyombo vya habari. Serikali na asasi husika hufumbua macho na maskio maafa yanapotokea, na baadaye hilo linazikwa katika kaburi la sahau.
Suala la kampeni dhidi ya pombe hasa ile haramu na ulanguzi wa mihadarati linapaswa kuwa ratiba ya kila siku.
Kaunti ya Kiambu na anakotoka kiongozi wa taifa, Uhuru Kenyatta imetajwa kuathirika pakubwa na pombe.
Ni kaunti iliyojaaliwa raslimali chungu nzima na zaidi ya yote inayoaminika kuwa tajiri, japo unywaji wa pombe umeipaka tope.
Swali ibuka, ni kina nani huunda na kugema pombe na ni kina nani wanaoiuza?
Nina uhakika asasi kama idara ya polisi inafahamu wazi wanaotekeleza shughuli hiyo, na kwa sababu ina mafisadi kadhaa inakuwa vigumu operesheni kufanywa inavyopaswa.
Mitaa mbalimbali, Kaunti ya Kiambu na Nairobi kila siku majira ya jioni ni lazima kama ibada maafisa wa polisi ‘kuzuru’ mabaa na vilabu vinavyouza vileo, ishara kuwa wanaelewa mchezo unaosakatwa.
Madhara yanapotokea, ni maafisa haohao wataongoza operesheni ya kukamata wahusika, na kuhadaa taifa jinsi walivyo katika mstari wa mbele kupambana na suala hilo tete.
Sisemi kuwa ni wote mafisadi, kuna kadhaa wazalendo wanaojitolea kwa hali na mali kukabiliana na kero hilo lakini wanaangushwa na wenye ubinafsi na tamaa.
Mbunge mwakilishi wa wanawake Kiambu Gathoni Wa Muchomba ameonesha jitihada katika vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya kaunti hiyo.
Hata hivyo, bidii yake huenda ikawa bure bilashi iwapo asasi zote, ikiwa idara ya polisi na mashirika ya kijamii, hazishirikiani.
Mwaka 2018 Martin Kamotho Njenga maarufu kama ‘Githeri Man’, alipitia marekebisho ya tabia na maadili kwa kilichotajwa kama kutekwa na unywaji wa pombe kupindukia.
Mwanamume huyo aliibua ucheshi mitandaoni na katika vyombo vya habari Agosti 2017, picha zake akiwa katika foleni ya kupiga kura akiwa amepakata mfuko uliotiwa kande ziliposambaa.
Licha ya kujivunia umaarufu, kiasi cha kupokea tuzo inayokabidhiwa Wakenya wanaokisiwa kufanyia jamii maendeleo, Head of State Commendation, Githeri Man aliripotiwa kulemewa na pombe.
Bi Gathoni alihimizwa na Rais Uhuru Kenyatta kumnasua, na ambapo alimsajili katika kituo cha Mamacare na Wa Muchomba, kilichoko Wangunyu, Kiambu, kinachoongozwa na mbunge huyo kama patroni.
Kamotho ambaye ni mzaliwa wa Githunguri, alipitia mafunzo kujaribu kumuondoa kwenye kero hiyo, lakini Taifa Leo iligundua baada ya kufuzu alirejelea maisha ya awali – unywaji wa pombe kupita kiasi. Wakati wa mahojiano ya kipekee, alidai Rais hakuafikia ahadi yake kwake.
“Nina shida, mimi ndiye tegemeo katika familia yetu,” alisema Bw Githeri Man ambaye ni mfanyakazi katika halmashauri ya jiji la Nairobi.
Huo ni mfano tu wa waraibu wa pombe, ambapo asasi husika zinapaswa kushirikiana na kuhakikisha hamasa inafanywa kila wakati.
Juhudi za Gathoni wa Muchomba na John Mututho zitaambulia patupu ikiwa ushirikiano hautakuwepo.
Serikali za kaunti zina wizara husika, ambazo zinapaswa kufanya kazi kwa karibu na viongozi wazalendo na mashirika ya kijamii.
Hamasisho na kampeni dhidi ya pombe hususan ile haramu na dawa za kulevya, isifanywe vyombo vya habari vinapofichua madhara, ila nyakati zote.