Makala

Hamuel Muguro Ngugi aliaga dunia katika mazingira gani ndani ya kituo cha polisi?

April 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

APRILI 13, 2019, maafisa wa polisi kutoka kituo cha Maragua, Kaunti ya Murang’a walitekeleza msako ambao uliishia mauti ya mshukiwa
mmoja.

Maafisa walivamia baa moja ya mji huo inayojulikana kama Starehe Bar na ambapo walikamata wahudumu wake wanne.

Wahudumu hao walitambulishwa kama Hamuel Muguro, Wairegi Cheki, Kamari na Waithaka Njeri.

Msako huo ulitekelezwa mwendo wa saa tano na dakika tano usiku, na hadi sasa, ni hatua ambayo imezua sokomoko kuu kiasi kwamba kuna
uchunguzi mkuu ambao unaendelezwa ili kutambua kama maafisa hao walikiuka haki za kibinadamu, walitumia mamlaka yao vibaya au walikuwa
na nia tu ya kuumiza washukiwa hao.

Hadi sasa, msako huo uko katika darubini ya mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa polisi (IPOA), wapelelezi kutoka mashirika ya haki za
kibinadamu na pia wakuu wa kiusalama katika Kaunti hiyo na pia kitaifa.

Ili kuelewa sokomoko katika kisa hiki, sheria za baa huhitaji wateja wawe wamemaliza uteja wao mwendo wa saa tano kamili.

“Lakini hivyo sio kusema kwamba saa tano zikifika wateja wafurushwe. Wale ambao hawakuwa wamemaliza kunywa pombe wanafaa kupewa muda
wamalize bora tu wasiuziwe baada ya saa tano. Pia, sheria hizo haziwashurutishi wahudumu kufunga milango na kuelekea nyumbani,”
asema Wakili Geoffrey Kahuthu wa mahakama kuu.

Katika hali hii, anasema kuwa yalikuwa makosa kwa maafisa wa polisi kuwakamata wahudumu wa baa hiyo mwendo wa saa tano na dakika tano.

Kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua anakiri kuwa “yalikuwa makosa ambapo hakuna mteja aliyekamatwa bali ni wahudumu pekee
walinaswa.”

Isitoshe, Bw Muguro alikuwa na matatizo ya kiafya na ambapo hata mwenye baa hiyo, Bw Kinuthia wa Ngai aliwaomba maafisa hao wasimtie
mbaroni bali wawakamate wenzake watatu.

Maafisa hao waliipuuza ombi hilo na ambapo Bw Muguro aliishia kuaga dunia akiwa katika seli za polisi.

Mbunge wa Maragua, Waithera Njoroge anasema kuwa kisa hiki kina utata mwingi na anaomba uchunguzi wa kina utekelezwe ili kubaini ni nini
hasa kilienda kombo katika msako huo.

“Ukiambiwa kuwa mtu ni mgonjwa unafaa kuwa makini sana. Haki za kibinadamu zinakushurutisha uchukue tahadhari usije ukazikiuka na
kumweka mshukiwa kwa hatari ya kiafya,” asema Njoroge.

Mbunge huyo anasema kuwa ikiwa maafisa hao waliambiwa kuwa mshukiwa alikuwa na matatizo ya kiafya, na iwe ni lazima wangemkamata, walifaa
kumwasilisha katika hospitali na wamtie pingu chini ya ulinzi wa kitanda cha hospitali.

Aidha, maafisa hao baada ya kugundua kuwa mshukiwa huyo aliaga dunia akiwa ndani ya seli inadaiwa kuwa walijaribu kuficha ukweli huo kwa
kuutoa mwili na kuupeleka katika wadi ya hospitali ya Maragua ili iwe na taswira kuwa aliaga akipokezwa matibabu.

Lakini kwa mujibu wa wale washukiwa waliokuwa katika seli hiyo pamoja na mwendazake wanakiri kuwa aliaga dunia akiwa ndani ya seli.

Mmoja wa mashahidi hao ni Bw Amos Mwangi ambaye anasema kuwa “kwa uhakika nikiwa mbele ya Mungu menzangu huyo alikohoa na akazima.”

Amos Mwangi ambaye alikuwa shahidi ndani ya kituo cha polisi cha Maragua mshukiwa akiaga dunia Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa mahabusu wengine walikuwa wamejaribu kuwaita maafisa waje wamshughulikie Bw Muguro baada ya kuzidiwa na matatizo ya kiafya
lakini wakapuiuzwa.

“Kuna mmoja wa maafisa hao ambao alinieleza kuwa hakuwa ameajiriwa kazi ya kushughulikia mahabusu ndani ya seli, kuwa hata angeaga dunia,
polisi walikuwa wamezoea kuona maiti,” asema.

Uchunguzi

Ni katika hali hii ambapo hata Inspekta Mkuu wa Polisi, Hilary Mutyambai ameagiza uchunguzi utekelezwe kikamilifu na ripoti rasmi iandaliwe kuhusiana na kisa hiki.

Aidha, Mwenyekiti wa tume ya huduma ya kikosi cha polisi (NPSC), Eliud Ndung’u Kinuthia ameonya kuwa kisa hiki kina taswira ya ukosefu
wa kinidhamu.

“Ni suala la kutamausha sana… Ikiwa ripoti itaandaliwa na IPOA ya kubaini hasa kulikuwa na utepetevu wa kimikakati katika utendakazi wa
polisi, usiwe na shaka kuwa kuna hatua itachukuliwa dhidi ya wahusika,” akasema.

Hayo yakijiri, marehemu atazikwa shambani la babake katika kijiji cha Gathigia-Irembu katika Kaunti ndogo ya Maragua, huku maafisa
wanaochunguza kisa hicho wakiendelea mbnele na kuandaa ripoti zao.