Makala

HASSAN OLE KAMWARO: 1944 hadi 2019

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

ALIYESHIRIKIANA na waziri maarufu marehemu John Njoroge Michuki kuleta nidhamu katika sekta ya uchukuzi, Hassan Ole Kamwaro ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Kamwaro alihudumu pia kama mwenyekiti wa chama cha Wiper kati ya 2015 hadi kufariki kwake, na ambapo amepoteza vita dhidi ya kansa; maradhi ambayo yanaendelea kuvuma kwa kasi nchini.

Familia yake imeripoti kwamba aliaga dunia akipokezwa matibabu katika hospitali moja nchini Amerika.

Kwa mujibu wa familia hiyo, mwendazake alikuwa akipambana na aina mbili za kansa na ambazo ni ile ya koo na ingine ambayo wataalamu waliitaja kuwa ya lymphoma (cancer of the lymphnodes).

Kando na kujulikana kama mfuasi wa utaratibu wa kisheria, alikuwa akizua mijadala mikali kuhusu maono yake ya uchumba.

Mwaka wa 2013, akiwa na miaka 69, alitangazia ulimwengu kuwa alikuwa amepata mchumba wa kumfaa kama mke wa tatu na akiwa ni Bi Eunice Sesian aliyekuwa na umri wa miaka 23. Hata hivyo, kuna baadhi ya ripoti katika kabrasha la historia zinasema alikuwa ni mke wa nne.

Kamwaro akijishabikia kuhusu ueledi wake wa kunasa mwanadada huyo ambaye alikuwa na umri wa ujana, alisema kuwa “utamaduni wetu unatukubalia kuwa katika ndoa za mitara, kusaka wasichana wabichi kimaisha na bora tu uwe na uwezo wa kuwatunza, huna shida kuwa na hata 100.”

“Wakenya wasiwe na hofu kuwa huyu mke wangu mpya ana umri wa chini hata kuliko watoto wangu kwa sasa, ieleweke kuwa ndiye chaguo langu na tunapendana kwa dhati,” akasema wakati huo.

Ili kuwapa Wakenya ushahidi kuwa familia yake ilikuwa ikimuunga mkono katika ndoa hiyo, alisema ni wanawe ambao walikuwa wamechanga Sh200,000 za kugharimia harusi hii ya kitamaduni ya Kamwaro na mrembo Sesian.

Marehemu Kamwaro alizaliwa katika kijiji cha Olchorro kilicho katika Kaunti ya Narok na alikuwa akisisitizia wengi kuwa hangewezana na wanawake wa mijini kama wachumba kwa kuwa “walikuwa wameharibiwa na kasumba za kigeni kuhusu maisha.”

Kamwaro alimpoteza mke wake wa kwanza kupitia ajali ya barabarani, kinaya kikiwa akipoteza uhai wake kwa hatari barabarani, Kamwaro alikuwa mtekelezaji sera za kuhakikisha usalama katika sekta hiyo akiwa mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Utoaji Leseni za Uchukuzi (TLB).

Mwaka wa 2011 aliachwa na mke wawa pili. Hii ni licha ya kuwa akiachwa, alikuwa akiuguza jeraha shingoni.

Leo hii, wamiliki wa magari watakuambia kuwa huyu Kamwaro hakuwa ‘mchezo’ hasa akishirikiana na Michuki ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Uchukuzi.

Kwa pamoja, waliwashinikiza wamiliki hao kuweka magari yao ya uchukuzi wa umma vidhibiti kasi, madereva na makondakta wakashinikizwa wawe wakivalia sare rasmi na la mno, magari hayo yote yakashurutishwa kujiunga na ushirika rasmi ili yawe yakifuatiliwa kwa urahisi.

Aliondoka kutoka wadhifa huo mwaka wa 2007 na akajiunga na siasa ambapo alijaribu kumenyana na aliyekuwa simba wa Narok na Wamaasai kwa ujumla, marehemu William Ole Ntimama.

Alishindwa katika harakati hizo lakini afueni ikamrejelea ambapo utawala wa Rais Mwai Kibaki wakati huo mwaka wa 2010 ulimteua tena katika wadhifa wake wa awali wa TLB na akahudumu hadi mwaka 2012.

Kamwaro alikuwa mmoja wa vigogo vya kisiasa katika jamii ya Maasai na ambapo harakati zake hazikutimia kutokana na ugonjwa huo ulioanza kumsumbua kwa kiwango kikuu mwaka wa 2017.

Kifo cha mjukuu

Aprili 24, 2011, familia ya Kamwaro ilikuwa katika vyombo vya habari baada ya mjukuu wake – akifahamika kama Dkt Catherine Senewa Timaiyo – kupatikana akiwa ameuawa katika mtaa wa Bangladesh ulioko mjini Ongata Rongai.

Mwili wake ulipatikana kando mwa barabara na gari lake likiwa limesukumwa hadi ndani ya mto wa Mbagathi.

Mamake marehemu, Sally Naisiae Kamwaro alisema kuwa alikuwa na ushahidi kuwa mtoto huyo aliuawa kikatili lakini wapelelezi hawakumchukulia kwa uzito kiasi kwamba hadi leo, hakuna haki imetendeka.

Mpasuaji wa maiti, Dkt Johansen Oduor aliandaa ripoti ikionyesha kuwa marehemu alikuwa na majeraha ya kugongagongwa kwa silaha butu.

Haieleweki ni jinsi gani familia tajika na yenye kuelewa kuhusu utaratibu wa uchunguzi ilikaa kimya katika kisa hicho cha mauaji.