Jamvi La SiasaMakala

Hata kama sisemi mengi siku hizi, acheni ukabila na mheshimu raia, Uhuru ashauri viongozi

Na BENSON MATHEKA November 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta ametoa wito wa amani na kukomeshwa kwa ukabila nchini katika hotuba yake ya kwanza ya hadhara mbele ya Rais William Ruto na Naibu Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Peter Kimani wa dayosisi ya Kanisa Katoliki la Embu , Bw Uhuru alihimiza amani kati ya viongozi wa Kenya na wananchi.

“Tunapaswa kuomba amani nchini Kenya. Tuombe uwiano kati ya raia na viongozi wa Kenya. Tuache ukabila tupendane,” Bw Kenyatta alihimiza akishangiliwa na umati.Uhuru alikariri kuwa umoja nchini unapaswa kuwa kipaumbele kikuu na kwamba viongozi na raia wote wanapaswa kujitahidi kuchangia katika ukuaji wa nchi.

“Sote ni Wakenya. Kenya haiwezi kusonga mbele ikiwa kuna migogoro kati ya raia na kukosa heshima kwa kila mmoja. Viongozi, waheshimuni wananchi, na wananchi watawaheshimu,” alisisitiza.

Uhuru aliongeza kuwa tangu astaafu amekuwa akiepuka siasa. “Sina mengi ya kusema. Unajua siku hizi siongei sana. Mimi hutazama tu TV na kusikiliza redio,” Uhuru alisema huku akicheka.

Ushauri wa Rais huyo wa zamani unajiri kufuatia kipindi cha siasa za mgawanyiko nchini zilizoshuhudiwa katika kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na nafasi yake kuchukuliwa na Kithure Kindiki. Matokeo ya kutimuliwa kwa Gachagua yalifichua mpasuko mkubwa kati ya Ruto na Gachagua.

Ujumbe wa Uhuru wa amani ulikuwa na umuhimu mkubwa baada ya maaskofu wa kikatoliki hivi majuzi kujitokeza na kuikosoa serikali ya Ruto.

Ukosoaji wa viongozi wa serikali dhidi ya serikali uliibua hisia kali kutoka kwa rais, mawaziri na wanasiasa mbalimbali ambao waliwasuta kwa kumkashifu Ruto hadharani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Uhuru pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Askofu Kimani kwa kuwekwa wakfu na kuongeza kuwa askofu huyo alikuwa rafiki yake wa karibu.

Uhuru alimtaja askofu huyo mpya kama kiongozi anayewajibika, mnyenyekevu, mzungumzaji laini na mkarimu.’Nataka kuwahakikishia watu wa Embu, mmepata kiongozi anayewajibika sana, na mnyenyekevu sana,” alisema.

Bw Uhuru aliwataka viongozi wa kisiasa kuheshimu wale wa kidini akisema japo askofu mpya ni rafiki yake wa muda mrefu, hali imebadilika baada yake kupanda cheo.

“Bwana Askofu, najua wamekukaribisha hapa, lakini sasa nimepoteza rafiki. Nitabaki mpweke. Sitakuwa tena na rafiki wa kucheka naye. Sasa nitakuwa nikimtazama kwa mbali tu. Sasa ninamuogopa, sasa ni bosi, anaweza kuzuia maombi yangu kutoka juu,’ Rais huyo wa zamani alisema.

Rais huyo wa zamani alimshukuru Papa Francis kwa kumchagua rafiki yake kuwa Askofu mpya. Alifichua kuwa urafiki wake na Askofu Kimani ulichipuka tangu zamani na sasa, ingawa wawili hao watasalia kuwa marafiki. hatakuwa huru tena kutaniana naye.