Hata mvua ikipungua, hatari ya maporomoko ingali ipo – Wataalamu
NA LABAAN SHABAAN
LICHA ya ubashiri wa idara ya hali ya anga kuonyesha mvua itapungua, hali ambayo imepisha ufunguzi wa shule, watalaamu wanaonya hatari bado ipo.
Mtaalamu wa uratibu na usimamizi wa kimazingira Prof Simon Onywere anaeleza kuwa hata mvua kidogo inaweza kusababisha maporomoko ya ardhi.
“Mvua nyingi zilizonyesha kwa wiki kadhaa zimelowesha mchanga maji. Kwa hivyo ni rahisi udongo kusongeshwa hata na maji madogo mvua inyeshapo,” Prof Onywere aliambia Taifa Leo.
“Bado kuna hatari ya janga la mvua. Cha muhimu ni kama mafuriko yatafanyika, utakuwa karibu na maeneo hatari?” aliuliza.
Kadhalika, msomi huyu anawashauri waliofurushwa makwao na mvua nyingi kuwa huu si wakati wa kurejea walikoishi kwa sababu maeneo hayo sasa ni chemchemi ya maji.
“Hii si mara ya mwisho tutashuhudia mvua nyingi kiasi hiki. Lakini kabla ya msimu wa mvua kubwa, kutakuwa na ilani kutoka kwa idara ya hali ya anga kwa wananchi kuwa macho,” alifafanua akiwasihi wananchi waepuke kuishi karibu na maeneo ya mkondo wa maji.
Mafuriko yanayoendelea nchini yamewaletea masumbuko takriban watu laki tatu huku zaidi ya familia 50,000 zikihama makwao baada ya mvua kuharibu mali zao.
Vile vile, angalau watu 257 wamefariki huku 188 wakijeruhiwa masika inapoendelea kuponda kaunti 31 nchini.
Licha ya hakikisho kuwa shule zinaweza kufunguliwa sasa, Idara ya hali ya hewa imeshikilia kuwa mvua nyingi zitaendelea.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Prof Onywere amewachachawiza wananchi kutumia matukio haya kujua sehemu za kuishi siku za usoni.
Kadhalika, ametia doa kwa serikali kwa kuwaagiza wananchi kuhamia sehemu nyingine bila kuwaarifu ni wapi hasaa wanafaa kujenga makazi yao.
“Ni kazi za mamlaka ya mipango kuhamasisha wananchi kuhusu sehemu mwafaka za kuweka makazi ili kuwaepusha na hatari ya majanga,” alieleza.
Prof Onywere hata hivyo anasema kuwa kuna changamoto za nakisi ya sheria zinazoongoza uratibu wa matumizi ya ardhi sehemu mbalimbali nchini.
“Kukiwa na sheria za kutosha zinazoongoza ujenzi na mipango ya matumizi ya ardhi, wananchi wataishi vyema kama zitafuatwa kikamilifu,” alisema.