Hata wakizozana, wazazi wana haki sawa ya kulea watoto wao
Malezi ya mtoto ni jukumu la kisheria ambalo mzazi au mlezi hupewa ili kuhakikisha mtoto anapata mahitaji ya msingi kama vile chakula, makazi, elimu, huduma za afya na ulinzi wa haki zake za msingi.
Nchini Kenya, wazazi wote wawili – mama na baba – wana haki sawa za kisheria kuhusu mtoto. Sheria ya familia nchini inatambua nafasi muhimu ya wazazi wote wawili katika ukuaji na maendeleo ya mtoto.
Mizozo kuhusu malezi hujitokeza mara nyingi wakati wa kutengana kwa wazazi au talaka. Ni muhimu kufahamu kuwa ni mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuamua ni nani atapewa haki ya kumlea mtoto iwapo kuna mzozo.
Katika kufanya maamuzi, mahakama huzingatia zaidi maslahi ya mtoto – si matakwa ya wazazi au matamanio ya mtoto, bali kile kitakachomwezesha mtoto kukua katika mazingira salama, ya upendo na yanayomfanya kuwa raia mwema.
Sheria zinazotumika ni Katiba ya Kenya na Sheria ya Watoto ya mwaka 2022.
Sheria ya Watoto ya mwaka 2022 inaweka wazi kuwa msingi mkuu wa uamuzi wa malezi ni maslahi ya mtoto. Hii inaiwezesha mahakama kutumia busara yake kufanya maamuzi kulingana na mazingira ya kesi. Mabadiliko haya ya kisheria yanazingatia mienendo ya sasa na maamuzi ya kihistoria kama uliofanywa na Jaji Joel Ngugi, ambaye alitoa uamuzi kwamba hata baba anaweza kupewa haki ya malezi ya watoto wadogo.
Kawaida, ilikuwa ni mama aliyepewa malezi ya watoto walio na umri chini ya miaka 10. Hata hivyo, Jaji Ngugi alikiuka utaratibu huu kwa kumpa baba haki ya malezi ya watoto wake wa miaka 8 na 15, akieleza kuwa sheria za zamani hazihusishi hali zote za kisasa na kwamba maslahi ya mtoto yanaweza kutimizwa na mzazi yeyote anayefaa.
Malezi Kisheria humpa mzazi mmoja au wote wawili uwezo wa kufanya maamuzi makuu kuhusu maisha ya mtoto – kama vile elimu, afya, na dini. Kwa kawaida, hii hugawanywa kwa usawa (50-50), isipokuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwa mzazi mmoja hawezi kushiriki kikamilifu.
Malezi Halisi ni kuhusu ni mzazi gani ambaye mtoto ataishi naye kila siku nah ii inahusiana moja kwa moja na makazi ya mtoto.
Malezi ya Pamoja ni pale wazazi wanakubaliana kugawana muda na mtoto. Inaweza kuwa ya kisheria (mazazi wote wana haki sawa) au ya halisi (mtoto anakaa na mzazi mmoja siku fulani za wiki na mwingine siku zingine).
Mahakama pia inaweza kutoa malezi ya mzazi mmoja na mwingine kupewa haki ya kumtembelea mtoto.Mzazi mmoja hupewa haki ya malezi kamili na mwingine kupewa haki ya kumuona mtoto kwa nyakati fulani. Hata hivyo, wote wanabaki na haki sawa za kisheria.
Wakati wa kufanya uamuzi kuhusu malezi, mahakama huzingatia masuala yafuatayo kwa kuangalia maslahi ya mtoto kwanza:
Mazingira ya makazi ya mzazi – je, yanafaa kwa malezi ya mtoto?, nia ya mzazi kutaka malezi – je, ni kwa sababu nzuri au ni kwa nia ya kibinafsi?, matakwa ya mtoto – anataka kuishi na nani, na kwa nini?,Dini ya mtoto na maadili yanayofundishwa, maoni ya watoto wengine wa familia (kama wapo),matakwa ya wazazi wote wawili, umri wa mtoto na uhusiano wa mtoto na kila mzazi.
Kwa kuzingatia vigezo hivi, mahakama hulenga kuhakikisha kuwa mtoto anakua katika mazingira bora – kimwili, kihisia na kiakili.
Kwa ujumla, masuala ya malezi ya mtoto ni magumu na yanahitaji uamuzi wa kina unaozingatia maslahi ya mtoto kama kipaumbele. Aina tofauti za malezi – iwe ya pamoja, ya mzazi mmoja au kwa makubaliano – zimeundwa kushughulikia mahitaji mbalimbali ya kifamilia.