Hatari ya kuongeza maziwa kwenye mboga za kienyeji, Omena
Nancy Oketch ni miongoni mwa Wakenya wengi wanaopenda sana mboga za kienyeji. Kila Jumapili baada ya ibada kanisani, huenda sokoni Kibuye na kuchagua kwa uangalifu mboga za majani asilia kupikia familia yake.
Hali hii pia ni ya kawaida kwa Dolrose Akinyi, mkazi wa Kisumu, ambaye anasema amekuwa akitegemea mboga hizo kwa muda mrefu, akizinunua kwa wingi siku maalum za soko.
“Hapo zamani kulikuwa na siku maalum za soko, kwa hivyo nilikuwa nanunua mboga nyingi za kutosha hadi siku nyingine ya soko,” aeleza.
Kutokana na uchungu wa asili wa mboga hizi, wanawake hao wanasema huwa wanazichemsha kwanza kisha kuzikaanga na kitunguu na nyanya kabla ya kuongeza maziwa kama njia ya kuzihifadhi.
“Kwa kuwa haziliwi mara moja, huwa nazipasha moto tena kwa kutumia maziwa ili zisiharibike,” asema Bi Akinyi.
Anasema aliiga utaratibu huu kutoka kwa mama yake, ambaye naye alifundishwa na mama yake mzazi.
“Alot mokuog (mboga zilizochemshwa na kuchachuka) ni nzuri kwa afya na huzuia magonjwa,” anakumbuka alivyofundishwa.
Kadri magonjwa ya mtindo wa maisha yanavyoendelea kuongezeka nchini, Wakenya wengi wameanza kugeukia lishe bora ili kuzuia maradhi kama saratani. Mboga za kienyeji ni chaguo maarufu kwa sababu ya virutubisho vyake na faida za kiafya.
Mboga hizi ni pamoja na managu, terere, mrenda, saga, kunde na majani ya viazi vitamu.
Kulingana na utafiti wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), asilimia 34 ya watu wanaoishi mijini na viunga vya miji nchini Kenya hula mboga hizi.
Hata hivyo, wataalamu wa lishe wameelezea wasiwasi wao kuhusu mbinu za kitamaduni za kupika mboga hizi, hasa matumizi ya maziwa, ambayo yanaweza kupunguza kiwango cha virutubisho vinavyopatikana.
Mboga hizi huwa na vitamini A, B na C kwa wingi, pamoja na madini ya chuma na pia zina viua sumu vya asili. Lakini kwa sababu ya ladha yake chungu, watu wengi huzichemsha kwa muda mrefu na kumwaga maji kabla ya kukaanga jambo linalopunguza virutubisho.
Bi Betty Okundi, Mkurugenzi wa Lishe na Chakula katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga, anasema kuwa matumizi ya maziwa hupunguza kwa kiasi kikubwa virutubisho vya mboga hizo.
“Maziwa yana madini ambayo hufunga chuma na baadhi ya vitamini katika mboga. Hii hupunguza uwezo wa mwili kuyeyusha virutubisho, hivyo mtumiaji hanufaiki vilivyo,” asema.
Bi Okundi anasema kuwa mboga zenye rangi ya kijani kibichi kwa kina huwa na madini ya chuma kwa wingi, jambo linalozifanya kuwa muhimu zaidi kwa wanawake wajawazito.
“Tunashauri wanawake wajawazito kula mboga hizi, lakini wengi wao huzipika kwa kutumia maziwa. Mwishowe hurudi hospitalini wakiwa na kiwango cha chini cha hemoglobini,” asema.
Onyo hili pia linahusu uji na omena zinapopikwa kwa maziwa kwani maziwa pia hufunga virutubisho vilivyomo kwenye vyakula hivyo.
Kutokana na umaarufu na faida za kiafya za mboga hizi, baadhi ya watu wameanza kuzipanda kwenye bustani za nyumbani, huku wengine wakiendelea kununua kutoka sokoni.
Baada ya kuvuna au kununua, hatua ya kwanza ni kutenganisha majani na shina gumu, kisha kuosha vizuri kuondoa mchanga na wadudu.
Bi Okundi anashauri maji yachemshwe kwanza kabla ya kuweka mboga. “Tumia maji kidogo ya moto yasiyohitajika kumwagwa,” asema.
Mboga zikishakatwa vipande vya kati (baada ya kuoshwa, si kabla), zichemshwe kwa dakika 10 hadi 15. “Wengine huzichemsha kisha kuzirushia maji baridi jambo linalosababisha virutubisho kupotea,” anaonya.
Baada ya kuchemshwa, zinaweza kukaangwa kwa vitunguu, nyanya na viungo vingine.
Caleb Odipo, mpishi katika hoteli moja Kisumu, anasema mikahawa mingi sasa imeacha desturi ya kuchemsha mboga kwa muda mrefu.
“Kwanza huchemsha maji, kisha huweka mafuta kidogo, chumvi na vitunguu vilivyokatwa. Kisha huongeza mboga zilizosafishwa na kukatwa,” asema.
Baada ya kupika kwa dakika 7 hadi 10, maji yaliyobaki huondolewa na kuhifadhiwa. “Kisha mboga hukanguliwa kwa mafuta kidogo na kumalizia kwa mchuzi wa kuku ili kuongeza ladha,” aongeza.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA