Makala

Sababu za waogeleaji kupendelea Shela licha ya kina kirefu cha bahari

June 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

WAOGELEAJI wanajulikana kwa kupenda maji ya Bahari Hindi.

Licha ya kivuko cha Shela kwenye maji ya Bahari Hindi katika Kaunti ya Lamu kuvuma kutokana na kuwepo kwa maji ya kina kirefu ambayo ni hatari kwa usalama wa waogeleaji na hata wasafiri, wanaopenda kuponda raha za ufuoni kupitia kuogelea, bado ni sehemu pendwa.

Ni kwenye kivuko cha Shela ambapo visa kadhaa vya waogeleaji kupoteza maisha vimeripotiwa, wakiwemo wanafunzi.

Mara nyingi maji ya Bahari Hindi kwenye kivuko hicho cha Shela hurindima, ambalo ni dhihirisho la wazi kwamba yana nguvu si haba, hasa kutokana na maji hayo kuwa ya kina kirefu.

Isitoshe, maji ya kivuko cha Shela wakati mwingi huwa makali huku yakiandamana na mawimbi mazito.

Hali hiyo inatokana na kwamba Bahari Hindi eneo hilo kwa kiwango fulani huwa ya wazi-yaani Open Sea.

Licha ya kuwepo kwa hatari hizo zinazozingira kivuko hicho husika, wenyeji, wageni na watalii bado wanahisi papo hapo Shela ndipo zinapopatikana raha zote zinazofungamana na kuogelea.

Yaani hulka ya ‘wapiga sherehe’ hawa ya kupenda kuogelea eneo hilo hatari la kivuko au ufukwe wa Shela ni sawa na kuchezea maisha ki ‘shilingi kwa choo.’

Taifa Leo ilichunguza na kuchambua ni mambo gani hasa yenye upekee eneo hilo la Shela hadi kuwasukuma wenyeji, wageni na watalii kupenda kulifikia ilmuradi waogelee bila kushtuka au kuzijali hatari zinazowakodolea macho.

Mkurugenzi wa Idara ya Majanga ya Dharura na Uokozi wa Kaunti ya Lamu, Shee Kupi, alikiri kuwa eneo hilo la ufukwe au kivuko cha Shela kweli ni hatari kwa usalama wa waogeleaji.

Bw Kupi alilichambua eneo hilo la Shela kuwa na mfano wa mkondo unaotumiwa hata na vyombo vya usafiri wa baharini vya kimataifa kupita kutokana na maji yake kuwa ya kina kirefu si haba.

Alisema sababu kuu inayowachochea waja kufika kuendeleza tafrija zao, ikiwemo kuogelea ni kutokana na kwamba ufukwe na maji ya Shela ni safi.

Bw Kupi alisema sehemu za forodhani au makazi ya wavuvi na wanaoponda raha kwenye ufuo wa Shela kimsingi pia huwa na urembo wa uhalisia fulani ambao huvutia macho ya wengi.

“Ni dhahiri kivuko cha Shela kwenye Bahari Hindi Lamu ni hatari kwani kina chake cha maji ni kirefu. Hilo hufanya maji kufuma, kurindima na kuwa makali kabisa kwa waogeleaji na wasafiri,” akasema Bw Kupi.

Aliongeza, “Ila eneo hilo limesalia kupendwa kwani linapendeza kwa macho. Ufukwe pale ni safi na uliosheheni mchanga mweupe, hivyo kuwanasa wengi, ikiwemo watalii wazimawazima wasiitambue hatari iliyoko pale.”

Afisa huyo wa Idara ya Majanga na Uokozi aidha aliwashauri wananchi, wageni na watalii kuwa waangalifu wanapoogelea pale.

“Najua fika kabisa kwamba maamuzi ya kuepuka kuogelea eneo hilo la kivuko cha Shela ni  magumu kwani wengi wamepazoea pale. Ila ninawashauri wanapoogelea wawe waangalifu. Jihadharini kuusongelea mkondo zaidi ndani ya bahari. Mnaweza kuogelea kandokando tu ya mkondo na bado mtazipata raha mzitafutazo za kuogelea,” akasema Bw Kupi.

Abdalla Omar, 40, mkazi na muogeleaji mashuhuri kwenye fukwe za Lamu, alisema Shela ndio kusema katika masuala ya raha za baharini.

Bw Omar alianza kuogelea akiwa umri wa miaka mitano.

Licha ya kuogelea karibu katika kila ufuo Lamu, bado anashikilia kuwa Shela ina raha yake.

“Nimeogelea kwenye fukwe za Mji wa Kale wa Lamu, Wiyoni, Matondoni, Kipungani, Kizingitini, Ndau, Faza, Pate, Mkokoni, Kiwayu na kwingineko lakini sijapata burudani la kuogelea kama lile nihisilo nikiwa ufuo wa Shela. Hapa mandhari ni safi, tulivu na hewa safi inapepea vyema,” akasema Bw Omar.

Bi Alice Ouma, mtalii wa ndani kwa ndani, anasema yeye hupenda sana kufika kwenye ufuo wa Shela kila anapofanya ziara yake Lamu kutokana na kwamba idadi ya wanaoponda raha pale huwa ni kubwa.

Bi Ouma anasema fuo nyingi ambazo amewahi kuzitembelea Lamu huwa zina idadi finyu ya waogeleaji au wanaofika pale kupitisha muda.

“Hapa ufuo wa Shela hakuna kuboeka. Kila alasiri inapoingia, iwe ni siku za juma au wikendi, utapata watu wamefurika hapa. Kuna wanaoogelea ilhali wengine wakijianika kwenye mchanga mweupe. Pia milima ya mchanga mweupe ya Shela imelipa eneo zima mandhari ya kuvutia na kupendeza,” akasema Bi Ouma.

Harry Franklin,35, mtalii wa kimataifa kutoka Uingereza, anasema maji ya rangi ya bluu (samawati) yanayokolezwa na waupe wa milima ya mchanga mweupe ya Shela ndilo jambo kuu linalomvutia kufika eneo hilo kujivinjari.

“Nikitaka kutazama mandhari ya jua likichomoza au kutua mimi huja hapa ufuo wa Shela. Usafi wa ufukwe hapa pia huniridhisha. Waweza kutembelea baadhi ya fukwe na kutoka huko umekasirika kutokana na uchafu wa plastiki na harufu mbaya. Ila Shela hilo haliko. Ni raha tupu hapa,” akasema Bw Franklin.

Wapenzi wa ufukwe na kivuko cha Shela hata hivyo waliisifu serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kwa kuweka mikakati kabambe ya usalama, hasa kwenye fuo mbalimbali za Lamu.

Kila mara wananchi, wageni na watalii wanapofurika kwenye fukwe za Bahari Hindi Lamu, ikiwemo Shela, iwe ni katika harakati zao za kuogelea, kubarizi kwa kujianika mchangani au hata kukimbia hapa na pale, utapata walinda usalama na maafisa wa kushughulikia majanga ya baharini wakipitapita kutekeleza doria zao ilmuradi usalama wa wanaoendeleza shughuli zao kwenye maeneo husika udhibitiwe kikamilifu.