Himizo vijana sasa wapangiwe ndoa wakisema zina upendo, heshima, ukomavu na huruma
WAZEE waliopangiwa ndoa na wazazi wao wamezisifia wakiwashauri vijana wa sasa kuanza kuzikumbatia kwa manufaa yao.
Bw Mohamed Mbwana Shee, 67, amekuwa akiishi kwenye ndoa aliyopangiwa na wazazi kwa miaka 38 sasa.
Anasema wazazi wake ndio walimchagulia mke aliye naye, Bi Mwanaheri Mohamed, 68, wakaoana mwaka wa 1987.
“Kwanza, watu watofautishe kuwa ndoa ya kupangwa na wazazi si ya mtu kulazimishwa kuoa fulani bali ni kama kupendekezewa tu kwamba fulani twahisi akufaa ukimuoa,” akasema Bw Mbwana.
Aliongeza, “Mimi binafsi nimeishi kwa ndoa sampuli hiyo kwa miaka 38. Ndoa za aina hii zimejaa upendo wa kweli, heshima, tabia nzuri na huruma. Ndiyo maana ninawashauri vijana wa leo kuzikumbatia ili kuepuka misongo ya mawazo, utengano na talaka.”
Bw Mbwana ni mzawa wa Mvundeni, Lamu Mashariki ilhali mkewe, Bi Mwanaheri akiwa ni kutoka Ngomeni, Kaunti ya Kilifi.
“Wazazi wangu ilibidi wafunge safari kwenda kuniposea mke wangu Bi Mwanaheri kule Ngomeni hata bila ya mimi mwenyewe kujua.
Baadaye walinifahamisha na kunipendekezea kwamba wakati wangu wa kuoa ulikuwa umewadia na kwamba nilifaa nioe Mwanaheri.
Bi Mwanaheri kwa upande wake asema msingi wa kudumisha ndoa ni wahusika kudumisha heshima, mawasiliano mwafaka na kusameheana kikweli kila wanapokumbwa na migogoro.
“Wazazi wetu walikuwa werevu. Walichagua wachumba wetu kulingana na historia kuihusu familia husika. Mambo waliyozingatia sana ni tabia nzuri, dini na misingi ambayo watoto katika familia wamekuzwa kwayo,” akasema.
Bw Khaldun Mahmoud Vae, 60, mzee na mshauri wa masuala ya ndoa katika jamii kutoka kijiji cha Kizingitini, Lamu Mashariki, ana wake watatu ambao wote alipangiwa na wazazi. Amejaliwa watoto 19 kutoka kwa wake hao watatu.
“Ndoa ya kupangwa na wazazi imejaa ukomavu. Mnafunzwa jinsi ya kupendana, kuvumiliana na kustahimiliana. Ndoa nyingi za vijana wa leo zinayumbayumba kutokana na wao kukurupuka tu wanataka kuoa.
“Mtu unaoa mke au unaolewa na kijana ambaye humjui wala misingi na tabia za familia yake huifahamu. Watu warejelee hizi ndoa za kupendekezewa au kupangwa na wazazi,” akasema Bw Vae.
Baadhi ya vijana hata hivyo wanapinga vikali kauli hizo wakisema zimepitwa na wakati.
Bw Simon Mbuthia kutoka Mpeketoni, anasema si sahihi mzazi kumuamlia mwanawe mume au mke wa kuishi naye.
“Ndoa ni maisha ya watu wawili wapendanao wanaokwenda kujenga familia yao. Hivyo basi, wawili hawa wanapaswa kufanya maamuzi kuhusu maisha yao ya baadaye na wala si lazima yafanane na wazee wao. Wazazi wanafaa kuwa washauri tu,” akasema Bw Mbuthia.
Kwa upande wake, Mzee na Mshauri wa Maisha ya Jamii, Bw Daniel Karisa Kaingu, anasema cha msingi katika ndoa yoyote ni heshima, kuvumiliana, upendo, kuelewana na moyo wa kusameheana.
Aidha, anawaonya wanandoa dhidi ya kuegemeza ndoa yao katika masuala mali, urembo na hadhi ya wahusika.