Himizo wakulima wakumbatie uongezaji thamani mazao
Na SAMMY WAWERU
KATI ya mwezi Oktoba na Desemba kila mwaka, matundadamu maarufu kama tree tomato huwa msimu wake wa mavuno.
Tayari mavuno ya mwaka huu wa 2020 yamesheheni sokoni. Hata ingawa ni matunda yenye wakulima wachache nchini, wasio na soko tayari hupunjwa na mawakala, mawakala wakitumia fursa hiyo kujinufaisha.
Yanapokomaa na kuanza kuiva, hayana uwezo kusubiri kwa muda mrefu, kwani ni mazao yanayoharibika na kuoza haraka.
Hii ina maana kuwa yanahitaji kuwa na wanunuzi pembezoni ili yasiharibike.
Suala la mazao mbichi ya kilimo kuharibika na kuoza kwa sababu ya kukosa wanunuzi, ni taswira bayana shambani na pia katika masoko.
Wanaokadiria hasara ni wakulima na wafanyabishara-wauzaji, wanaoyapokea kutoka kwa mawakala au moja kwa moja kutoka kwa wakulima.
Changamoto za matunda ya tree tomato yanayofahamika pia kama tamarillo si tofauti na za maparachichi, machungwa, ndizi na maembe (ambayo kwa sasa yamesheheni sokoni) kati ya mengineyo.
Wakulima wa mboga hasa kabichi, viazi na karoti, nyakati zingine hupitia matatizo ya ukosefu wa soko.
David Karira na ambaye amekuwa katika ukuzaji wa matundadamu kwa muda wa miaka kadhaa, anasema hakuna kinachoua na kuzima ari ya mkulima kama kukosa soko la mazao.
“Soko hukosekana kwa namna hii; mawakala hupunja wakulima kwa madai kuwa mazao yamejaa sokoni, hivyo basi wanayanunua wanavyotaka, bei ya hasara. Mkulima asiye na soko tayari au asiye na njia kupata wanunuzi, mazao yake huishia kuharibika endapo hataitikia kuyauza bei wanayotaja,” mkulima huyo anafafanua.
Anasema, awali alipoingilia kilimo cha matunda ya tree tomato, kero la kukosa wanunuzi na mazao yake kuishia kuharibika hayakuwa mageni.
“Mahangaiko yalipungua nilipopata wanunuzi wa moja kwa moja kutoka Nairobi,” David anadokeza, akisema anatafiti namna ya kuyaunda juisi na kuihifadhi wakati akitafuta soko.
Kukwepa matatizo ya kukosa soko, yanayochangia mazao kuharibika, wakulima wanahimizwa kukumbatika uongezaji thamani.
“Changamoto za soko zitatuliwa wakulima wakitathmini nje ya boksi, kuongeza mazao thamani badala ya kuendelea kufuata mkondo wa kuyauza yakiwa mabichi,” anahimiza Dennis Njenga, mwasisi wa E-Farmers Africa, mtandao wa kijamii unaoleta pamoja wakulima na wanunuzi.
Kulingana na Njenga, utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo utawezesha mkulima au mfanyabiashara-mnunuzi kutafuta soko bila hofu yoyote.
“Mazao kama vile matunda, mboga, karoti, na mengineyo ni vigumu kuhifadhika kwa muda mrefu. Yakiongezwa thamani, mfano kwa kuunda juisi ya matunda au kuyakausha, itakuwa rahisi kusaka wanunuzi,” anaelezea.
Aidha, mboga pia zinaweza kukaushwa na kutumika wakati wa ukame.
Ni suala au mfumo unaohitaji hamasisho kupitia serikali na pia wadau husika katika sekta ya kilimo.
Mkulima anayejitambua kama Charity, na ambaye hukuza matundadamu anasema mazao yake mara ya kwanza nusra yaharibikie shambani.
“Niliokolewa na mitandao ya kijamii baada ya kupiga picha ya mazao yakiwa shambani na niliyovuna, nikazipakia katika makundi ya shughuli za kilimo mitandaoni,” anasema mkulima huyo, akiongeza kuwa mazao yaliyosalia yanaelekea kuisha.
Ni kero ambalo limemchochea kutathmini suala la kuongeza mazao yake thamani, katika msimu na misimu ijayo.