Makala

Historia yajirudia Raila akijikuta pale pale babake Jaramogi alikuwa 1992

Na JUSTUS WANGA, CECIL ODONGO March 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HISTORIA ya familia ya Jaramogi Oginga Odinga kuwaniwa inajirudia kisiasa, wakati mwingine ikisalitiwa uchaguzini licha ya kuahidiwa uungwaji mkono na wapinzani.

Kinara wa ODM Raila Odinga anaonekana kuandamwa na yaliyomfika Babake Jaramogi kutokana na jinsi ambavyo anawaniwa kisiasa kiasi kuwa sasa anaahidiwa uungwaji mkono kutoka wanasiasa mbalimbali mnamo 2027.

Baada ya kushindwa kufanikisha azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mwezi uliopita, Bw Odinga amerejelea siasa za Kenya kwa kishindo.

Waziri huyo mkuu wa zamani anaendelea na mikutano ya kusaka maoni ya Wakenya kuhusiana na mwelekeo wa kisiasa ambao atauchukua suala hilo ligawanya hata wandani wake.

Bw Odinga amekuwa akiwaniwa na mrengo wa Rais William Ruto ambaye alimuunga mkono kwenye azma yake ya AUC iliyokosa kutimia.

Aidha Raila kwa sasa anaonekana kuwa na ushirikiano na utawala wa Kenya Kwanza baada ya kuiokoa isizime kutokana na maandamano ya Gen Z yaliyofanyika mnamo Juni mwaka jana kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

Hata hivyo, kilichoashiria kujirudia kwa historia ni jinsi ambavyo Raila sasa anawaniwa na wanasiasa wa Mlima Kenya wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Raila na Uhuru mnamo Jumanne walikutana kwenye makazi ya Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe japo Bw Murathe alisema mkutano huo ulikuwa sadfa kwa sababu viongozi wote wawili walikuwa Kilifi.

Hata hivyo, duru zimearifu Taifa Leo kuwa Uhuru alirai Raila asibanduke kwenye upinzani kwa ahadi kuwa atamuunga mkono mnamo 2027. Bw Kenyatta aliunga mkono Bw Odinga mnamo 2022 ila hakufaulu huku Mlima Kenya ukimuunga mkono Rais Ruto.

Bw Gachagua kwenye mahojiano na runinga moja nchini wiki moja iliyopita naye alisema yupo tayari kumfanya Raila awe rais 2027 iwapo ataungana nao kwenye upinzani.

“Raila anapendeza zaidi kwa sababu tayari ana kura milioni 6.8. Tulimshinda kwa kura 200,000 pekee. Tukikubali kuungana naye na nimeona jinsi ngome zake zinavyopiga kura, naye anapiga kura kati ya saa nne na saa tano asubuhi, atakuwa Rais kabla apige kura,” akasema Bw Gachagua.

Kama tu Raila, Jaramogi alipewa ahadi ya kufanywa kuwa rais baada tu ya mfumo wa vyama vingi kuridhiwa na utawala wa Kanu.

Mapema 1990, Jaramogi alikuwa ameamua kuchukua mwelekeo wake wa kisiasa na kuwania uongozi wa nchi. Kwa kuwa upinzani ulitaka kumngóa Rais Daniel Moi mamlakani, wakili Paul Muite aliwaita wanasiasa Kenneth Matiba na Charles Rubia nyumbani kwake na kuwarai waungane na Jaramogi kuondoa Moi madarakani.

Kwa mujibu wa Bw Muite, mkutano huo pia ulihudhuriwa na Askofu Okullu na mwanasiasa Job Omino na wote wakaamua kumfikia Jaramogi ili awe mgombeaji wa urais wa upinzani.

Mabwa Rubia na Matiba walikutana na Jaramogi afisini mwake jumba la Agip ambapo walisema watamuunga mkono lakini kigogo huyo akazua shauku. Hii ni kwa sababu ndoa yake na Mzee Jomo Kenyatta iliishia pabaya, akibanduliwa serikalini mnamo 1966 licha ya kukabidhi rais wa kwanza uongozi wa nchi kuelekea uhuru.

Mabwa Matiba na Rubia walikamatwa na kuzuiliwa kwa mwaka moja. Baada ya kuachiliwa, Bw Matiba alienda kupokea matibabu ngámbo.

Akiwa huko mwanasiasa moja kutoka Mlima Kenya alienda kumtembelea na kumwaambia awanie urais badala ya kumuunga mkono Jaramogi eti kwa sababu alikuwa na umaarufu wa kutosha.

Kwa mujibu wa Bw Muite ambaye alikuwa akiunga mkono urais wa Jaramogi, Rubia alimwaambia mikataba ya kisiasa haikuwa sheria ya kuheshimiwa.

Bw Matiba naye alimwaambia “Hujui Paul, hata hao Wajuluo watapigia Ken Matiba na si Jaramogi,”

Usaliti huo haukuwa jipya kwa Jaramogi na akaamua kuzindua azma yake ya urais huku baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya kama Bw Muite, Gitobu Imanyara na Kiraitu Murungi wakisimama naye na kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 1992.