• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Hofu biashara zenye hatari ya milipuko zikitapakaa mitaani

Hofu biashara zenye hatari ya milipuko zikitapakaa mitaani

NA MWANGI MUIRURI

MUUNGANO wa Wahandisi wa Upangaji Miji ya Kaunti (TCPAK) umetoa tahadhari kwamba wananchi katika maeneo yao ya makazi wanaishi na hatari tele za milipuko.

Mwenyekiti wa muungano huo Bw Mairura Omwenga amesema kwamba mlipuko wa gesi ambao hadi sasa umeua watu 12 na kujeruhi zaidi ya 300 katika mtaa wa Mradi, Embakasi, Kaunti ya Nairobi mapema Februari 2024 ni ishara tu ya jinsi mambo yalivyo.

“Ni hatari kubwa sana inayotukodolea macho kwa kuwa miji yetu haina ramani za upangaji. Utapata viwanda vilivyo na hatari ya milipuko au kutoa gesi za sumu vikiwa katika makazi ya watu,” Bw Omwenga akasema.

Aliongeza kwamba viwanda hivyo ni pamoja na vile vya kutengeneza rangi, mivinyo, upakiaji wa gesi na hata bidhaa za kimatibabu na kemikali za kila aina.

“Ni baada tu ya janga kuzuka ambapo kila anayenyooshewa kidole hukwepa uwajibikaji na kulaumu kila aina ya kimbilio,” akasema.

Hata hivyo, Bw Omwenga alisema kwamba kazi ya kudumisha uadilifu katika upangaji miji ni serikali za Kaunti.

“Serikali za Kaunti ndizo wamiliki wa ramani za miji na hata mitaa. Ukipata kiwanda ndani ya makazi ya watu, wa kulaumiwa ni kaunti. Utapata hata mochari karibu na mito inayotumika na wakazi kuchota maji ya kunywa kando na majitaka kumwagwa ndani ya maji ya kupikia,” akasema.

Bw Omwenga alisema serikali za kaunti ndizo hutoa idhini za ujenzi na katika kufanya hivyo, zinawajibishwa na sheria kukinga binadamu na maendeleo ya madhara.

“Lakini bora tu ulipe ushuru, kwingine ikiwa ni hongo, utakubaliwa ujenge au uwekeze katika viwanda vya mauti mitaani. Serikali hizo ndizo pia zinafaa kukagua mikakati ya afya ya umma na usalama wa kuhepa hatari katika majengo lakini hilo halifanyiki katika Kenya ya sasa,” akasema.

Bw Omwenga aliteta kwamba baada ya majanga kuzuka, yakiwemo yale ya kuporomoka kwa nyumba, serikali hucheza siasa za kutishia, kubembeleza na hatimaye za kuchukua mlungula hadi kesi hizo zififie.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

IMF, World Bank waapa kusaidia Kenya kuondoka orodha ya...

Polisi wafichua sababu nyeti za kuua washukiwa

T L