Hofu mitandao nyeti ya serikali kuwa katika mikono ya wageni
MASWALI yameibuka kuhusu umiliki wa mifumo ya kidijitali inayotumiwa na serikali kuhifadhi taarifa nyeti za Wakenya.
Ingawa serikali inadai kumiliki mifumo hiyo kama e-Citizen, e-GP, NTSA, na SHA, taarifa zinaonyesha kuwa baadhi yake bado inadhibitiwa na kampuni za kibinafsi ndani na nje ya nchi.
Mifumo hii huhifadhi taarifa za huduma muhimu kama usajili wa magari, malipo ya serikali, huduma za afya na nyinginezo.
Hali hii imeibua hofu ya usalama wa data na ukiukaji wa Sheria ya Kulinda Taarifa, hasa baada ya kuthibitishwa kuwa sava za Tume ya Uchaguzi (IEBC) haziko humu nchini bali nje ya Kenya.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alieleza kuwa kuweka mifumo muhimu ya serikali mikononi mwa makampuni ya kibinafsi ni kosa kubwa kisheria, akisema ni mpango wa ufisadi unaolenga kunufaisha watu wachache serikalini.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kulinda Taarifa, Bi Immaculate Kassait, alisema Sheria hairuhusu kuhamisha data nje ya nchi bila kufuata masharti, ambapo nakala ya data lazima ihifadhiwe Kenya.
Aidha, taasisi zina wajibu wa kuripoti uvujaji wa data ndani ya saa 72.
Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, anapanga kuwasilisha hoja kuamuru ukaguzi maalum wa mfumo wa NTSA.
Hii ni baada ya Waziri wa Fedha, John Mbadi, kufichua kuwa mfumo wa e-GP uliogharimu zaidi ya Sh375 milioni haujamilikiwa rasmi na serikali, kwani bado uko mikononi mwa kampuni ya India (i-Sourcing Technologies) na mshirika wake wa Kenya, SYBYL.
Katika sekta ya afya, serikali iliingia mkataba wa Sh104.8 bilioni kwa miaka 10 kuendeleza Mfumo wa Taarifa za Afya (IHITS) ikishirikiana na kampuni ya Safaricom, Apeiro (kutoka UAE) na Konvergenz.
Hata hivyo, kuna wasiwasi kuhusu umiliki halisi wa mfumo huo kutokana na mabadiliko tata ya umiliki wa hisa.
Huku Waziri wa Afya, Aden Duale, akisisitiza kuwa data zote za afya ziko salama na zimo ndani ya nchi, ukaguzi wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, ulibaini kuwa serikali bado haina udhibiti kamili wa jukwaa la e-Citizen licha ya kukabidhiwa rasmi mwaka 2017.
Ukaguzi huo uligundua malipo yasiyoeleweka, kutoweka kwa stakabadhi muhimu, na unategemea pakubwa kampuni ya Webmasters Kenya Limited licha ya kuwa mkataba wa kukabidhi mfumo huo ulikamilishwa Januari 2023. Hali hiyo imetajwa na wabunge kama “janga” na “ulaghai kamili.”
Mbunge wa Rarieda, Dkt Otiende Amollo, na wenzake wameelezea hofu kwamba serikali inaweza kupoteza data au mabilioni ya fedha endapo makampuni hayo yataamua kusitisha huduma ghafla.
Pia, mikataba mingi haijasainiwa na Mwanasheria Mkuu wala Mawaziri wa Fedha, jambo lililozidisha wasiwasi wa uwazi na usalama wa taifa.
Hali hii imewaacha Wakenya na maswali mazito: Nani anamiliki mifumo ya kidijitali ya serikali? Je, data zao ziko salama? Na iwapo serikali inadhibiti kikamilifu miundombinu ya ICT inayotumika kuhudumia wananchi.