Hofu ripoti ikionyesha wanawake wanazidi kuteswa, kuuawa kikatili kila siku!
IDADI ya wanawake wanaouawa kikatili inaendelea kutisha huku vituo vya uokoaji vikionyesha kuwa visa 4, 000 vya dhuluma dhidi ya wanawake huripotiwa kila mwezi.
Huku polisi wakisema wamerekodi visa 97 ndani ya miezi mitatu, takwimu zinaonyesha kila muda wa saa ishirini na nne, kisa cha mwanamke kuuawa huwa kinaripotiwa nchini Kenya.
Katika vituo vya kuokoa waathiriwa wa ghasia za kijinsia vya hospitali ya Nairobi Women, hali ni ya kutisha huku visa 4,000 vya dhuluma dhidi ya wanawake vikiripotiwa kila mwezi.
“Ni janga, na lazima hatua zichukuliwe,” asema Dkt Sam Thenya, Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Nairobi Women.
“Mzigo kwa uchumi wa ghasia za jinsia ni mkubwa kwa uchumi wetu. Ni lazima tukabiliane na uovu huu unaotendewa wanawake na wasichana. Ni mabinti, wake, dada na mama zetu,” alisema.
Ili kukabiliana na mzozo huu unaozidi kuongezeka, serikali inachukua hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa.
Katibu wa Idara ya Jinsia, Bi Anne Wang’ombe, ametangaza mipango ya kampeni ya kitaifa inayofanana na kampeni iliyofaulu ya kupiga vita Ukimwi miaka ya 1990 na mapema miaka ya 2000.
“Mifumo ya kusaidia waathiriwa ni muhimu,” Bi Wang’ombe aliambia Taifa Leo.
“Tunatambua haja ya dharura ya kuanzisha na kuimarisha mifumo ya usaidizi, ikiwemo makazi, huduma za ushauri nasaha na usaidizi wa kisheria kwa waathiriwa wa ghasia za jinsia. Pia, tunataka kuimarisha ukusanyaji wa data kuhusu mauaji ya wanawake na ghasia za jinsia ili tuweze kuunda sera na kuzifuatilia kwa ufanisi.”
Rais William Ruto pia ameingilia mzozo huo, akihusisha kuongezeka kwa visa vya mauaji ya wanawake na kudorora kwa maadili na uhalifu.
“Ninataka kuwahakikishia kuwa tumejitolea kuwapa polisi wetu vifaa ili kukabiliana na changamoto hii,” Rais Ruto aliahidi, akijitolea kuimarisha uwezo wa kutekeleza sheria.
Mwenyekiti wa chama cha wabunge wanawake Kenya (Kewopa), Bi Leah Sankaire ambaye ni Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kajiado, anaelezea kuchoshwa na kasi ya chini ya kushughulikia visa vya mauaji ya wanawake.
“Serikali, Bunge, na wadau wengine wote hawajafanya vya kutosha kudhibiti tishio hili. Tunahitaji kuona hatua na wahusika wakichukuliwa hatua. Mauaji ya wanawake yamefikia kiwango cha janga la kitaifa, na kama tunavyojua, kuchelewesha haki ni kunyima haki,” alisema.
Bi Susan Otieno wa shirika la Action Aid, anapendekeza kuundwa kwa sajili ya umma ya wahalifu wa mauaji ya wanawake.
Wakati huo huo, mtetezi wa mtoto wa kiume Bi Faith Nashipae, anasisitiza umuhimu wa kuwajumuisha wanaume na wavulana katika juhudi za kukabili uovu huu.
“Tunahitaji kuwachukulia wanaume kama washirika wa kuzuia mauaji ya wanawake,” Bi Nashipae anaelezea.
“Ni muhimu tuchunguze kile tunachoweza kuwafanyia wavulana wetu na kuwawezesha. Pia kuna haja ya kupeleka elimu kuhusu dhuluma za jinsia shuleni na makanisani katika kampeni ya kupiga vita ukatili wa kijinsia,” akasema.