Makala

Hofu Siaya Baada ya Mwili wa Mtoto Aliyezikwa Kufukuliwa na Kuibwa Usiku

June 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KASSIM ADINASI NA LABAAN SHABAAN

MSETO wa mshtuko na hofu ulivaa familia moja katika kijiji cha Kamhinda, kata ndogo ya Komenya-Kowala, Kaunti ya Siaya baada ya kuamkia kaburi wazi la mwana wao aliyezikwa zaidi ya wiki moja iliyopita.     

Bw Joseph Ochieng Origi alimpoteza mwanawe mchanga mnamo Mei 28 saa tatu tu baada ya mkewe kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Siaya.

“Tulizika mwili katika boma langu lakini Ijumaa tuliamka na kupata kaburi wazi na mwili haupo,” alipasua mbarika Bw Origi.

Bw Origi alisema kuwa tukio hilo la kustaajabisha limesababishia familia wasiwasi wasijue la kufanya.

“Tulikuwa tunaanza kupona baada ya kufiwa, kwa sababu hiyo ndiyo tungeweza kufanya pekee. Familia tayari ilikubali, hata hivyo, mtu kuja kubeba maiti usiku ni tukio la kuogofya,” alieleza.

Bw Origi alifichua kuwa hadi wakati huu hawajategua kitendawili cha ufukuzi wa mwili huo nyakati za usiku.

“Kuna matukio ya kawaida ya watu kuiba watoto walio hai, hata hivyo, yule anayeiba maiti kutoka kaburini ni ajabu na haijawahi kusikika,” alisema.

Bw Origi alifichua kuwa mtoto huyo alipata matatizo ya kupumua mara tu baada ya kuzaliwa kabla ya kufariki katika hospitali ya rufaa ya kaunti.

Alisema kilichowatia hofu zaidi ni kubaini kuwa mwili huo ulibebwa ukiwa uchi. Nguo walizomvalisha mtoto mchanga zilipatikana karibu na kaburi.

“Inaonekana kama mazingaombwe kwetu. Kila kitu alichovaa mtoto kiliachwa, hata soksi zake,” alisema.

Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Mwer na wapelelezi wameanzisha uchunguzi wa tukio hilo.

“Sidhani kuna mtu yeyote ambaye nimemdhulumu kiasi kwamba anaweza kuvamia nyumba yangu na kubeba maiti ya mtoto wangu mchanga,” alilalamika.

Mtoto huyo aliaga dunia kabla ya kutajwa hivyo rekodi za hospitali zilimtambulisha kuwa mtoto wa Bw na Bi Origi.

“Tulipanga kumpa mtoto jina siku ya kuondoka hospitalini kama ilivyo ada. Alikaa duniani muda mfupi sana kwa hivyo hata hakupewa jina,” alieleza baba aliyejaa mafadhaiko.

Kulingana na Mzee Christopher Awuondo, katika jamii ya Waluo, kaburi ni muhimu sana kwa sababu watu wanaamini wafu walio hai.

“Kuwepo kwa kaburi hilo katika boma ni muhimu  kwa sababu ni ukumbusho wa kila wakati kwa walio hai kwamba hapo zamani jamaa zao waliishi nao. Ndiyo sababu makaburi yangeundwa na mashina ya migomba kuzikwa kuashiria kaburi,” alisema.

Kwa nini mtu aliiba mwili wa mtoto mchanga na kuuchukua ukiwa uchi? Hilo ndilo fumbo ambalo familia na kijiji kizima cha Kamhinda wanashindwa kufahamu.