Makala

Hofu ya Knec mitihani ikivujwa kupitia mitandao ya kijamii

Na MERCY SIMIYU, BENSON MATHEKA October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BARAZA la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) limeeleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa visa vya udanganyifu wa mitihani kupitia mitandao ya kijamii, hasa Telegram na WhatsApp wakati huu ambao mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) unaendelea kote nchini.

Kulingana na ripoti ya ufuatiliaji ya Agosti 2025, jumla ya vituo 18 vya Telegram vimetambuliwa na KNEC kwa kusambaza karatasi zinazodaiwa kuwa za mtihani wa KCSE na wa Baraza la Mitihani la Wahasibu na Makatibu Kenya (Kasneb), kati ya jumla ya vituo 51 vilivyotambuliwa.

Licha ya kuwepo kwa sheria zinazolinda wanafunzi na kuhakikisha uwajibikaji, changamoto kuu sasa ni mienendo ya wasimamizi wa mitihani.

Mtihani wa kitaifa wa KCSE ulianza wiki iliyopita, huku shule zikijiandaa kwa mitihani ya Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA) na Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) itakayoanza Jumatatu, Oktoba 27 hadi Oktoba 30.

Hata hivyo, ucheleweshaji wa mgao wa fedha kwa shule umesababisha changamoto katika maandalizi ya mitihani katika baadhi ya vituo.

KNEC imesema kuwa jumla ya wanafunzi 3,424,836 watafanya mitihani ya kitaifa mwaka huu. Kati yao, 996,078 ni watahiniwa wa KCSE, 1,130,669 wanafanya mtihani wa KJSEA ambao ndio wa kwanza, na 1,298,089 wanafanya KPSEA.

Mwaka huu unafungua ukurasa muhimu katika mageuzi ya elimu nchini, mwaka mmoja tu baada ya kundi la mwisho la wanafunzi milioni 1.4 kufanya mtihani wa KCPE mwaka 2023.

Hii pia ni kundi la pili kutoka mwisho kufanya KCSE kabla ya mfumo wa Mtaala ya Umilisi (CBC) kutekelezwa kikamilifu.

Imebainika kuwa baadhi ya wasimamizi wa mitihani wamekuwa kiungo muhimu katika uvujaji na usambazaji wa mitihani hiyo.

Maafisa wa elimu na usalama wamefichua kuwa wanafunzi waliobobea katika teknolojia kutoka vyuo vikuu vitano wanatumia ujuzi wao wa kidijitali na uzoefu wa zamani kama watahiniwa wa KCSE kujinufaisha kifedha kwa kuvuja mitihani.

Takwimu za KNEC zinaonyesha kuwa kufikia Agosti 2025, vituo 51 vya Telegram na WhatsApp viliripotiwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano (CAK) kwa kusambaza maudhui ya mitihani, huku 19 kati ya hivyo vikiendelea kufanya kazi.

Kwa sasa, kesi 36 zinachunguzwa, huku walimu sita mwaka huu na walimu 117 mwaka 2024 – jumla ya walimu 123 – pamoja na wanafunzi 10, wakikamatwa kuhusiana na udanganyifu wa kabla ya mtihani.

“Kwa sasa tatizo si wanafunzi pekee — bali kwa wale waliopewa jukumu la kusimamia mitihani. Tumejitahidi kuhakikisha uadilifu, lakini changamoto kuu ni uaminifu wa wataalamu wetu, hasa wakuu wa shule, wasimamizi na maafisa wa elimu,” alisema afisa mmoja mkuu wa KNEC.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo wanafunzi ndio walikuwa wakihusishwa zaidi na udanganyifu, sasa walimu na wakuu wa shule ndio wanaonekana kuhusika zaidi katika uvunjaji wa sheria na biashara haramu za mitihani.

“Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba wale wanaopaswa kulinda mfumo ndio wanaousaliti,” akaongeza afisa huyo.

Mkurugenzi Mkuu wa KNEC, Dkt David Njengere, alisema kuwa Baraza limekamilisha maandalizi yote ya kimikakati, yakiwemo majaribio ya awali ya mitihani ya shule za sekondari msingi mapema mwaka huu.

“KNEC itahusisha wasimamizi 10,765, wasimamizi wakuu 12,126, wasimamizi wa mitihani 54,782, maafisa wa usalama 22,247 na madereva 2,692. Vituo vinavyohudumia KJSEA na KPSEA vitahitaji idadi kubwa zaidi,” alisema Dkt Njengere.

Kwa kuimarisha ulinzi wa mitihani, KNEC imeanzisha mfumo wa kufuli za kidijitali, na kuongeza idadi ya jumla ya kontena za kuhifadhi mitihani kutoka 617 hadi 642.