Makala

Hoteli ya mkosi wa shambulio la Al-Shabaab yalia kupoteza wateja licha ya kujikakamua

May 31st, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

HOTELI inayosifika sana Mpeketoni na iliyokuwa imejenga jina ya Breeze View ni yenye kupambwa au kurembeshwa hadi kupendeza kabisa kwa macho.

Hoteli hiyo iko pembezoni mwa mji huo wa Mpeketoni ulioko Kaunti ya Lamu.

Ni miongoni mwa hoteli za hadhi ya juu zinazotambulika, siyo Mpeketoni tu bali kote Lamu.

Mnamo usiku wa Juni 15, 2014, hoteli ya Breeze View iligonga vichwa vya vyombo vya habari ambapo ilikuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza kabisa kushambuliwa na kuteketezwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Magaidi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari, zikiwemo bunduki, guruneti na visu, waliuvamia mji huo wa Mpeketoni na kuua zaidi ya watu 90, wengi wao wakiwa wanaume kwa usiku huo mmoja.

Zaidi ya nyumba 30, zikiwemo hoteli na makazi ya watu na magari zaidi ya 40, viliteketezwa na magaidi hao.

Miaka 10 baadaye, wenye hoteli na majumba mengine mjini Mpeketoni wamejikaza na kujenga upya, hivyo kuushinda kabisa ugaidi.

Lakini katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Alhamisi, mmiliki wa hoteli ya Breeze View, Bw John Kiuna Wanyoike, alilalamika kuwa licha ya kujitahidi na kutumia fedha nyingi katika kuisimamisha hoteli yake, changamoto bado zinaikumba hoteli hiyo kwani wateja wanaokodisha vyumba hotelini humo ni haba.

Bw Kiuna alitaja shambulio hilo la kigaidi la 2014 kuwa doa jeusi na mkosi kwa biashara yake ya hoteli ambayo bado haijasimama.


Hoteli ya Breeze View, Mpeketoni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hoteli ya Breeze View, kwa mfano, ina jumla ya vyumba 25 pamoja na ukumbi wa kuandalia mikutano.

Bw Kiuna anasema kinyume na miaka ya awali kabla ya shambulio kutekelezwa, ambapo hoteli yake ilikuwa ikijaa kila siku kwa zaidi ya asilimia 50, miaka ya sasa baada ya tukio la kigaidi la 2014 imeshuhudia idadi finyu ya wateja ambapo ni wawili au watatu pekee wanaokodisha vyumba kwenye hoteli yake kwa siku.

Kulingana na Bw Kiuna, zipo siku nyingine ambapo hata mteja mmoja hukosekana hotelini humo.

Bw Kiuna aliishukuru serikali ya kitaifa kwa jitihada zake katika kuimarisha usalama Mpeketoni na Lamu kwa ujumla.

Aidha aliiomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na biashara nchini kuzindua kampeni maalum ya kuutangaza utalii wa Lamu Kenya na mataifa ya nje ili kuwezesha wageni na watalii kuzuru hoteli zao kwa wingi, hivyo kuwawezesha wamiliki kujipatia mtaji.

“Nilikadiria hasara kubwa wakati magaidi walipoiteketeza hoteli yangu. Sikufa moyo. Nilijikaza. Nikachukua mikopo ili kuijenga upya hoteli kama uonavyo. Nilitarajia kwamba biashara ingerudi kama zamani ili niweze kulipa madeni. Hali imegeuka au kwenda visivyo kabisa miaka ya sasa. Watalii na wageni niliotegemea kufika hotelini kwangu kukodisha vyumba hawaji tena. Kuna wengine hata wafikapo Mpeketoni huikwepa hoteli yangu,” akasema Bw Kiuna.

Aliongeza, “Watu wafahamu kuwa usalama upo Mpeketoni na Lamu kwa jumla. Wasiione hoteli ya Breeze View kuwa eneo la mkosi wa shambulio la Al-Shabaab bali watambue kujikakamua kwetu katika kurejesha mambo shwari kama uonavyo. Waje wakodishe vyumba hapa kwani viko tele. Wasiwe na shaka. Usalama umedhibitiwa vyema na serikali yetu tukufu.”

Mjasiriamali huyo aidha anatoa wito kwa jamii ya Lamu kudumisha umoja, uwiano na utangamano wa dini na makabila yote yapatikanayo eneo hilo.

Anasema ni kupitia umoja ambapo amani na utulivu utazidi kudumishwa Lamu.

Pia anawashauri wanajamii wa Lamu kutochoka kuendelea kuukemea na kuukashifu ugaidi, akishikilia kuwa ni kupitia kashfa hizo ambapo adui hatapata nafasi ya kupenya miongoni mwao na kuisambaratisha jamii.

“Endapo hatutaendeleza kashfa dhidi ya ugaidi tutaonekana kana kwamba tunaukaribisha. Magaidi watasalia kuwa maadui wetu wakuu sote Lamu, Kenya na ulimwengu mzima. Ugaidi umeacha wengi na machungu, iwe ni ya kupoteza wapendwa wao, kuachwa na majeraha au makovu ya maisha, kupoteza mali na kuacha wengi wakihangaika kwa ufukara. Lazima tuushinde ugaidi tukitumia njia zote,” akasema Bw Kiuna.

Baadhi ya wateja kindakindaki wa Breeze View walisifu jitihada za Bw Kiuna katika kurejesha hadhi ya hoteli hiyo.

Bw Simon Mwangi alisema mara kadhaa yeye binafsi amelala kwenye hoteli hiyo na kwamba iko chonjo.

“Kwa wale wanaoogopa kulala Breeze View wajue hali ni shwari pale. Huduma ziko sawa. Malazi ni ya kifahari na ya kuridhisha. Sioni sababu ya wewe kukosa kuuonja utamu wa Breeze View,” akasema Bw Mwangi.

Naye Bi Susan Njuguna alisifu ukumbi wa mikutano ulioko Breeze View, akiwarai wenye nia ya kuandaa mikutano Mpeketoni kuteua hoteli hiyo kufanyia makongamano yao.

“Nimefanya mikutano kadhaa na wanachama wangu pale Breeze View. Ukumbi wao ni wa kifahari. Hewa inapepea vyema na kuiburudisha kabisa nafsi na moyo,” akasema Bi Njuguna.

Wakazi aidha wanasisitiza haja ya serikali kuboresha miundomsingi, hasa barabara Mpeketoni, Hindi, Baharini na sehemu nyingine ili kuwavutia wawekezaji zaidi kuwekeza miradi yao ya maendeleo kote Lamu.

Wateja wakiwa ndani ya hoteli ya Breeze View, Mpeketoni. PICHA | KALUME KAZUNGU