HUDUMA NAMBA: Dakika za mwishomwisho
Na SAMMY WAWERU
MAELFU ya watu katika sehemu tofauti za nchi wanaendelea kujitokeza kujisajili kwa Huduma Namba, mpango wa kitaifa kupitia mfumo wa kidigitali wa NIIMS (National Integrated Identity Management System) na ambao serikali imeutetea vikali ikihoji utarahisisha utoaji wa huduma zake kwa raia.
Usajili huu wa maelezo ya kutambua raia wa Kenya na wa kigeni walioko humu nchini ulianza mnamo Aprili 2, mwaka huu, 2019.
Kulingana na serikali ni kwamba siku ya mwisho ya shughuli hii ni mnamo Jumamosi, Mei 18, ikisisitiza kwamba haitaongeza muda zaidi.
Aidha, Wakenya wanaoishi nchi za nje pia wanahusishwa katika usajili huu ambapo shughuli za kunasa kidigitali maelezo yao katika mataifa waliyoko zilianza Mei 6 na zitatamatika Juni 2019.
Huku siku mbili pekee zikisalia usajili humu nchini utie kikomo, foleni ndefu zimeshuhudiwa wiki hii katika vituo mbalimbali vya kujisajili. Watu wamelazimika kusimamisha biashara zao na wengine kukosa kuenda kazini ili kutimiza hitaji hili la serikali, kikatiba.
Hata hivyo, kufuatia uchunguzi wa Taifa Leo imebainika kwamba baadhi ya maeneo fomu za Huduma Namba zinauzwa katika maduka ya kurudufisha stakabadhi.
Katika vituo kadhaa vya kujisajili eneo la Zimmerman, Nairobi, tulivyozuru mapema Alhamisi, baadhi ya wananchi wamefichua kwamba wanalazimika kutafuta fomu katika maduka hayo.
“Watu ni wengi, na wahudumu wanalazimika kufunga idadi ya wanaojisajili kwa kukosa kutoa fomu zaidi ili washughulie waliotangulia. Hivyo basi hatuna budi ila kupiga chapa fomu za waliokabidhiwa kujaza ili tuweze kujisajili,” amesema mwananchi na ambaye ameomba jina lake lisichapishwe.
Ameeleza kwamba leo, Alhamisi ni siku ya pili kujitokeza kuona iwapo atafanikiwa kujisajili.
“Jana (Jumatano) nilikuwa hapa na sikufanikiwa kusajiliwa kwa sababu ya foleni ndefu,” akasema.
Tumezungumza na mmiliki wa duka moja la kupiga chapa Zimmerman, na amekiri uuzaji wa fomu za Huduma Namba unafanyika, moja ikigharimu Sh20.
“Nakala yake imepakiwa mitandaoni, tunaitoa tunapiga chapa na kuwapa wananchi kwa ada,” amedokeza.
Pia, inadaiwa mtaa wa Githurai 45, Kiambu, fomu moja inauzwa Sh50, baadhi ya watu wakizichuuza vituoni.
Iwekwe wazi kwamba serikali ilisema kwamba kujisajili mtu hatozwi ada yoyote.
Siku ya tatu
Wakati huo huo mwanamume mmoja mwenye uraia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), amesema kwamba leo Alhamisi ni siku yake ya tatu kufika kituoni.
Kuna wananchi wanaolalamika kwamba usajili huu unajikokota.
“Laini hazisongi kamwe, tuliwasili hapa saa kumi na mbili alfajiri, sasa inaelekea adhuhuri na hatujahudumiwa. Kwa nini tusiongezewe makarani?” baadhi ya kina mama wamelalamika eneo la Zimmerman.
Kina mama wajawazito na wenye watoto, wanalazimika kuvumilia miale ya jua kali wakisubiri kuhudumiwa.
Wasimamizi wa vituo tulivyozuru wamekataa kuzungumza nasi wakidai hawaruhusiwi kuongea na wanahabari, huku suala la fomu kuuzwa katika maduka ya kupiga chapa likisalia kuwa kitendawili kilichokosa mteguzi.
Hata hivyo, mmoja wao amesema kuna maafisa wanaozuru vituo hivyo kila baada ya muda fulani ili kukwamua mashine zinazoleta utata.
Kufikia mwanzoni mwa wiki hii, Jumatatu, watu 31 milioni ndio walikuwa wamejisajili.
Waziri wa Usalama Ndani Dkt Fred Matiang’i alisisitiza kwamba muda zaidi hautaongezwa baada ya Jumamosi Mei 18, 2019.