Makala

Huenda ‘kuruka’ mimba kukawa kosa la ufisadi wa kuadhibiwa kisheria Kenya

January 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

Wakora wa kimapenzi huenda wajipate katika mtego wa kushtakiwa kupitia kwa sheria za ufisadi ikiwa mjadala uliozinduliwa na Mkuu wa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) Bw Twalib Mbarak utanogeshwa.

Akiongea katika Kaunti ya Murang’a majuzi katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ufisadi Duniani, Bw Mbarak alisema kwamba “wanaume ambao hutunga wanawake mimba na kisha kuingia mitini wanachangia ufisadi kukita mizizi nchini”.

Alifafanua kwamba mtoto anafaa kupata malezi bora yaliyo na maadili lakini kuwaacha wanawake kuwalea watoto wakiwa peke yao bila mchango wa mwenye mbegu kunatwika jamii na taifa watoto waliojaa watundu.

“Ni vigumu sana kulea mtoto ukiwa peke yako…hasa upande wa mama. Kuna yale maadili ya kimsingi yatakosa katika hayo malezi na ni hali ambayo huathiri mtazamo wa mtoto huyo katika maisha yake ya baadaye,” akasema.

Bw Mbarak alisema maadili ya kutotaka ufisadi yanafaa kuwekwa katika mawazo na mtazamo wa mtoto akiwa mchanga “lakini sisi kama wazazi tunaweka ufisadi mbele ya kila kitu huku watoto wakishuhudia na kuishia kurithi ukora wetu”.

Alisema ufisadi ukiwa na mazingara ya kuustawisha hata ndani ya malezi, tumeishia kuwa na taasisi fisadi ajabu, hata maeneo ya ibada yakiathirika ambapo nyadhifa za uongozi na manufaa mengine yanaafikiwa kupitia utapeli.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Patrick Mukuria alisema ulevi ni hatari nyingine ambayo inavumisha ufisadi kwa kiwango kikuu katika afisi za umma.

“Unapata mfanyakazi ambaye amekesha kwa baa na akiingia afisini hata ubongo umekwama, kichwa kimegungana na hakuna hata kufikiria kunaweza ibuka ndani ya ubongo huo uliojaa tembo…hawezi hata akajielewa wala kuelewa kazi yake. Unapata amekuwa kizingiti kikuu katika kuafikia malengo ya kiutawala na huo pia ni ufisadi,” akasema.

Bw Mukuria aliongeza kwamba walevi wakifika afisini ni ama wawe wanasinzia au wanakwepa kuhudumia umma huku wengine hata wakichomoka kwenda mitaani kusaka pombe ya kujikwamua akili almaarufu ‘kutoa lock’.

Bw Mukuria alisema wengine huingia kazini na kuweka makoti kwa dawati zao za huduma ndio waonekane kana kwamba wako kazini lakini wako nje wakitumikia ulevi wao.

Kamishna huyo alisema kwamba “ni lazima tupambane na aina hiyo ya ufisadi ambayo hata imewageuza baadhi ya wafanyakazi wa umma kupanga njama za kuita wanaosaka huduma ndani ya mabaa ili watoe hongo au wawanunulie pombe”.

Bw Mbarak alisema kwamba iwapo taifa hili litaweza kupambana na ufisadi kwa umoja, wananchi wataweza kuafikia ubora wa kimaisha kwa wepesi.

“Hili ni taifa lililobarikiwa ajabu na Maulana. Tuko na rasilimali na watu walio na ubunifu na bidii. Lakini ufisadi umetupokonya mianya ya kustawi…Kuna mataifa ambayo hayana baraka ya rasilimali asili lakini yametupiku kimaendeleo…Sisi hapa kazi ni kufisadi tu,” akasema.

Bw Mbarak alilalama kuwa ufisadi huo umejipenyeza katika vitengo muhimu vya huduma kwa wananchi kiasi kwamba umekuwa janga.

[email protected]