Makala

Huu ni mwaka wa 12 akiwalea wanawe baada ya kutokea kifo cha mkewe

August 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PHYLLIS MUSASIA

KWA miaka 12, watoto watu wa Ezekiel Matare wameishi kumjua baba yao kama rafiki wa karibu, abu na pia ‘mama’.

Uhusiano kati yao ni wa kipekee na ambao umejengwa kwa upendo, ujasiri na msingi wa kufuata mafundisho ya Biblia na kuweka tumaini kwa Mungu.

Matare anaishi mtaani Bondeni, Nakuru Mashariki ambapo pia anaendesha duka la kinyozi ili kujikimu maishani.

Mkewe wa takribani miaka 10, marehemu Regina Abuje, aliaga dunia mwaka wa 2008. Aliugua ugonjwa wa figo na kisha kufariki katika hospitali ya Kenyatta alipokuwa anatibiwa.

“Mke wangu alipofariki, watoto wetu walikuwa wa umri mdogo sana. Msichana mkubwa alikuwa na umri wa miaka sita na alikuwa ameanza darasa la kwanza,” akasema Matare.

Kulingana naye, baada ya mazishi ya mkewe yaliyofanyika Bungoma, alijua kwamba alikuwa na kibarua kigumu cha kuwalea watoto bila mama.

“Msichana wa pili alikuwa katika shule ya chekechea na mvulana mdogo alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu,” akasema.

Wakati huo, Matare anasema tayari alikuwa katika maisha ya ukata baada ya kutumia raslimali zake nyingi – karibu zote – kwa matibabu ya mkewe.

Ndoto zote ambazo alikuwa nazo na mkewe anasema zilizima na akawa mnyonge rohoni ila alitamani sana kuwa tofauti na wanaume wengine kwa kuwalea watoto wake kwa ujasiri.

Anasema alianza kwa kuhakikisha kuwa alikuwa rafiki mkubwa na wa karibu kwa watoto hao na mwenye kuaminika kila mara apokuwa nao.

“Si jambo rahisi kuwalea watoto wa kike kama baba kwa sababu wakati mwingine wao huwa na uoga wa kusema mambo mengine lakini nilijaribu sana kuwaondolea uoga na nikawa karibu sana na wao,” akasema.

Baadhi ya mambo ambayo yaliongeza ujasiri wao kwake, anasema, ni kusoma vitabu pamoja, kushiriki mafunzo ya Biblia na kuomba pamoja kama familia.

Ezekiel Matare, 46, akiwa na wanawe Sheldone Nekesa na Shanice Nasimiyu nyumbani kwao mtaani Bondeni, Nakuru Mashariki mnamo Juni 22, 2020. Amewalae wanawe peke yake kwa muda wa miaka 12 sasa baada ya kifo cha mkewe mnamo 2008. Picha/ Phyllis Musasia

Bintiye wa kwanza, Shanice Nasimiyu, anamsifu baba yake, akimtaja kuwa ni zawadi ya kipekee ambayo walipata maishani.

Kulingana na Nasimiyu ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne, urafiki wa dhati miongoni mwao ndio umewasaidia kukaa na baba kwa urahisi bila kuhisi upweke wa kumkosa mama maishani.

“Licha ya kwamba mama aliaga dunia tukiwa wadogo, baba amefanya hima kuhakikisha kwamba tuko salama na wenye furaha kila wakati,” akasema Nasimiyu wakati Taifa Leo iliwatembelea nyumbani kwao.

Baadhi ya changamoto ambazo Matare amepitia katika safari ya kuwalea wanawe jinsi anavyosimulia, ni pamoja na kuwalea watoto katika mazingira ya mtaa duni ambapo mambo mengi hutendeka wakiona.

Hata hivyo, anaongeza kuwa nyanya wa kumzaa mama yao amekuwa wa msaada wa karibu kwao kwa kuwazungumzia kila mara haswa wakati huu ambapo wako tatika umri wa kubalehe.

Aidha, anafichua amekuwa na matatizo na watu ambao humshauri kuoa mke mwingine, yeye akisema kwake imekuwa vigumu kumpata mtu ambaye atampenda pamoja na wanawe kwa usawa.

“Ni kweli kwamba miaka 12 tangu mke wangu alipoaga dunia ni muda mrefu, lakini ninawajali sana wanangu kiasi kwamba naogopa wasije wakateseka katika mikono ya mama wa kambo,” akasema.

Malengo yake anasema ni kuona kwamba wanawe wanapata elimu pamoja na mahahitaji mengine bila kutatizika.