• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Miili ya mvulana, msichana yakwama chini ya mwamba

Miili ya mvulana, msichana yakwama chini ya mwamba

NA OSCAR KAKAI

WAKATI Bw Alfri Korianyang na mkewe, Bi Cheparkong Alfri walifika nyumbani kutoka sokoni saa moja jioni Jumanne, hawakujua watoto wao wawili walikuwa wanakosekana.

Walianza kusaka wana wao kila kona ya kijiji cha Chemoril, wadi ya Tapach, Kaunti ya Pokot Magharibi kwa matumaini ya kuwapata lakini waliambiwa na baadhi ya watoto kuwa walionekana kwenye barabara wakielekea mtoni.

Familia hiyo iliambiwa kuwa watoto hao, mmoja mvulana wa umri wa miaka 10 na mwingine msichana wa umri wa miaka mitano walisombwa na maji kwenye mto Chemoril uliofurika kutokana na mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo.

Kulingana na mamake watoto hao, wanaye watatu pamoja na mmoja wa jirani walikuwa wameenda kucheza kisha wakaanza kufuata tingatinga ambalo lilikuwa linalima na kufungua barabara katika eneo hilo.

Mama huyo wa watoto wanne anasema kuwa watoto hao wanne walikuwa wanarejea nyumbani wawili walipokutana na mauti walipokuwa wanavuka mto.

“Msichana mdogo ndiye alikuwa wa kwanza kuanguka kwenye maji na ndugu yake akiwa anajaribu kumuoka, wote walianguka kwa maji,” akasema mama huyo.

Mama huyo anasema kuwa mmoja wa wanawe pekee ndiye alirejea nyumbani pamoja na mwingine wa jirani lakini walinyamaza sababu waliogopa kusema kuwa wenzao walikuwa wameanguka kwenye maji.

“Baada ya kusaka kila mahali, watoto hao wawili ambao waliepuka kifo walituambia kuwa wenzao walianguka kwa maji. Watoto wangu walikuwa na ndoto kubwa maishani ya kufaulu katika masomo ili baadaye waje kutusaidia sisi wazazi. Ni uchungu kupoteza watoto wawili. Nimebaki sasa na watoto wawili pekee,” akasema.

Baba ya watoto hao, Bw Korianyang, anasema kuwa amevunjika moyo.

“Watoto wangu walikuwa wa maana sana kwangu. Hawakustahili haya,” akasema Bw Korianyang.

Jumatano, wakazi waliopiga kambi kwenye mto huo wakisaka miili za watoto hao lakini kazi hiyo ilikuwa ngumu kwa kuingia kwenye maji.

Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwenyendu katika Kaunti ya Pokot Magharibi Scholarstica Kapello ambaye alizuru eneo la mkasa jioni na kikosi chake, aliambia Taifa Leo kuwa mto huo uko mashinani na ilikuwa vigumu kujua ni watoto wa nani baada ya wao kufa maji.

“Tukio hilo lilifanyika majira ya saa moja jioni na iliwachukua muda wakazi kujua walikuwa watoto wa nani. Eneo hilo halina mawimbi na ni vigumu kulifika. Ilichukua siku nzima wazazi kupokea habari kamili. Hapo ndipo watoto ambao waliponea kifo walisema ukweli,” akasimulia Bi Kapello.

Bi Kapello alisema kuwa kikosi chake kilizuru eneo la mkasa na kuanza kusaka miili ambapo ilipatikana ndani ya mwamba.

“Mwogeleaji wetu, Bw Patrick Pilisi alifaulu kufika penye kulikuwa na miili lakini ilikuwa vigumu kuiondoa. Mawe hayo makubwa yanafaa kubomolewa. Kutoka Jumanne hadi leo miili haijaondolewa,” akasema.

Naibu wa chifu wa kata ya Kalee Benson Chesolel aliambia Taifa leo kuwa juhudi za kuondoa miili zimelemazwa kutokana na maji mingi na lukumba kwenye mto huo.

“Wakazi wameingia kwenye mto lakini bado wanakumbana na changamoto. Bado tunasaka miili bila wataalamu. Tunatumia miti ambayo haiwezani na huu mto hatari sababu una mawe na maji mengi,” akasema Bw Chesolel.

Alisema kuwa mto huo haujawahi kuua mtu katika muda ambao yeye ameujua kufikia sasa.

Kulingana na wakazi, miamba na maji mengi yamelemeza juhudi za kuondoa miili ya watoto hao.

Wanakijiji na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakitafuta miili ya watoto wawili. Miili hiyo ilikwama chini ya mwamba kwenye mto Chemoril. PICHA | OSCAR KAKAI

Mwakilishi wa Wadi ya Tapach Timtim Korinyang amewaonya wakazi dhidi ya kuvuka mito ambayo imefurika sababu ni hatari kwa maisha yao.

“Mvua imesababisha maafa. Wakulima wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa baada ya mazao yao kuharibika,” akasema Bw Korinyang.

Aliwashauri wakazi kujitahadhari wakati huu wa masika.

“Hawafai kuacha watoto na mifugo karibu na mito,” akasema.

Ameitaka serikali kuu, ya kaunti na wafadhili wengine kuja na kusaidia kujenga madaraja.

“Kuna haja ya serikali kujenga madaraja sababu wakazi wanaumia sana,” anasema Bw Korinyang.

Kulingana na idara ya utabiri wa hali ya anga kwenye kaunti hiyo, wakazi wa maeneo ya nyanda za juu watarajie mvua kubwa wiki hii na matokeo mema ana mabaya.

Kulingana na ripoti za mashinani, kuna visa vya mipasuko na mianya kwenye milima na maporomoko ya tope.

Afisa wa utabiri wa hali ya anga kwenye kaunti hiyo Wilson Lonyang’ole amewataka wazazi kuchukua tahadhari dhidi ya wanao hasa wale wanaenda shule wakivuka mito.

Afisa huyo anasema kuwa wakazi wanaoishi kwenye maeneo hatari kuhamia maeneo salama ili wasiathirike na maporomoko ya tope na mafuriko.

Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin alisema kuwa wako tayari kukabiliana na athari za mvua kubwa kutokana na maelezo ya idara ya utabiri wa hali ya anga kutokana na mvua kubwa ambayo inanyesha eneo hilo.

Bw Kachapin alisema kuwa wameweka kamati ambayo inashirikisha washika dau kutoka kwa wizara za barabara, maji,afya na kilimo.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Ortum, Kongelai, Kacheliba, Parua, Nyarkulian na Muino ambayo yanashuhudia mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Alisema kuwa wanahamasisha wakazi kupitia kwa vyombo vya habari kuhusu athari za mvua kubwa.

Aliwataka wakazi kujijali na serikali pia itawasaidia wakati wa mikasa wawe salama kila wakati.

“Juzi tulinunua ambulensi kusaidia wakati wa dharura. Tunataka serikali kuu kutengwa fedha nyingi za majanga,” akasema.

Jumatatu, watu wanne walijeruhiwa vibaya katika kijiji cha Kaptaram, tarafa ya Kapro, kaunti ndogo ya Pokot ya kati, kaunti ya Pokot Magharibi baada ya maporomoko ya tope kutokea eneo hilo.

Mwaka wa 2019, zaidi ya watu 20 waliuawa, uharibifu mkubwa na maelfu ya wakazi kupoteza makazi katika vijiji vya Muino, Nyarkulian na Parua baada ya maporomoko ya tope kutokea.

Tukio jingine baya lilikuwa la mwaka wa 2020 ambapo watu 50 walipoteza maisha, mali kuharibika, zaidi ya wakazi 1,500 kupoteza makazi katika eneo la Chesegon baada ya mafuriko na maporomoko ya tope kutokea.

Mwaka 2023, mwanamke mmoja aliaga dunia eneo la Muino, kaunti ndogo ya Pokot ya Kati, majengo ya shule ya upili ya Chemutlokotyo kuharibiwa pamoja na soko la Ortum kusombwa na mafuriko.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mafuriko: Waliotafuta hifadhi shuleni waingiwa na wasiwasi

Mackenzie aomba sabuni ya kuoga na ruhusa ya kumuona mkewe...

T L