Makala

HYRAX HILL: Makavazi ya kipekee Nakuru

May 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa Nakuru Ijumaa waliungana na ulimwengu kusherehekea Siku ya Makavazi Duniani, iliyoratibiwa na Baraza la Kimataifa kuhusu Makavazi (ICM).

Hafla hiyo imekuwa ikiandaliwa kila mwaka, na mara hii ilifanyika katika makavazi ya Hyrax Hill, hatua chache kutoka mjini Nakuru.

Iliwaleta pamoja washikadau kutoka sekta mbalimbali waliohimiza wakazi kuzingatia mshikamano baina ya matabaka yanayokaa mjini.

Wanafunzi wa vyuo vikuu, shule za upili na zile za msingi kutoka mbali na karibu ya Nakuru walipata fursa ya kuwasilisha kazi zao za sanaa kupitia nyimbo, michoro na maigizo.

Watumbuizaji wa ngoma za kiasili kutoka jamii ya Ogiek wakiwaongoa wageni kwenye hafla ya kusherehekea siku ya makavazi duniani katika makavazi ya Hyrax  . Picha/ Richard Maosi

Baadhi ya shule zilizohudhuria hafla hiyo ni Jomo Kenyatta High, Shule ya msingi ya Engashura, Upper Hill na Hyrax.

Wageni kutoka dhehebu la Hindu, Bodi ya Utalii nchini ,kampuni ya mawasiliano ya Telkom, Taasisi ya Ulimbwende Vera na Chuo cha East Africa Institute of Certified Studies pia walipata mwaliko.

Mbali na burudani wageni walizuru makavazi na kujifunza mengi kuhusu asili ya binadamu wa kwanza, amali za jamii na utamaduni wa Mwafrika.

Mtunzaji wa vifaa kwenye makavazi ya Hyrax, Bi Lilian Amwanda alisema hii ni tafrija ya kumbukumbu kote ulimwenguni.

Wanafunzi waliojumuika kwenye makavazi ya Hyrax mjini Nakuru kuadhimisha Siku ya Makavazi ulimwenguni. Picha/ Richard Maosi

“Ni matumaini yetu kufikia mwisho wa siku, kila mtu atajifunza jambo,kuhusu asili ya binadamu tangu miaka mingi iliyopita,” Bi Amwanda akasema.

Aidha mboreshaji wa makavazi kutoka eneo la Kati Abdi Galgalo aliongezea kuwa makavazi ya kitaifa yameweka mikakati itakayowasaidia wanafunzi kujifunza mengi kuhusu histotia yao.

Aliongezea kuwa wizara ya utalii itakuwa ikifanya kazi kwa ukaribu sana na shule, ili kubadilisha mtazamo hasi wa raia kuhusu makavazi ya kitaifa.

“Tumefikia makubaliano na Kaunti ya Nakuru kuwa mlima wa Hyrax utaboreshwa ili kuvutia wageni zaidi,na kufikia hadhi ya kimataifa,” alisema.

Wageni watazama mnyama huyu aliyehifadhiwa hapa. Picha/ Richard Maosi

Naye mkurugenzi wa utalii kutoka kaunti ya Nakuru, Dominic Saitoti alisema makavazi ya Hyrax yanatambulika kutokana na mchango wake kuwavutia watalii Nakuru.

Kwa upande mwingine mkurugenzi wa jinsia na utamaduni.kutoka kaunti ya Nakuru, Bi Alice Gekonde aliwahimiza wakenya kujihusisha na utunzaji wa mazingira yanayohifadhi wanyama na mimea ya kiasili.

“Tubadilishe kasumba kuwa maeneo ya kutalii yametengenezewa wazungu na matajiri wenye mifuko iliyojaa hela. Rasilimali za humu nchini zinafaa kutufaidi sisi kabla ya kumfurahisha mgeni,” aliongezea.

Hyrax ilipatiwa hadhi ya kuwa makavazi ya kibinafsi 1945 lakini 1965 ilichukuliwa na serikali ya Kenya na kuorodheshwa rasmi kama makavazi ya kitaifa.

Watu wengi walihudhuria hafla hiyo ambayo iliwapa fursa kujionea maisha ya zamani. Picha/ Richard Maosi

Mlima wa Hyrax unapatikana katika kaunti ya Nakuru na umebeba kumbukumbu nyingi kuhusu maisha ya binadamu miaka 3000 iliyopita.

Wanasayansi wamekuwa wakitumia Hyrax kuchunguza baadhi ya mafuvu na mifupa ya binadamu na wanyama iliyopatikana mlimani.

Makavazi ya Hyrax yalitambuliwa na mwanasayansi Lous Leakey, Mnamo 1926 akiwa katika shughuli za kufanya uchunguzi kuhusu asili ya binadamu.

Katika awamu ya kwanza alitambua mabaki ya binadamu karibu na ardhi,kisha baadaye alipofukua ardhi alikumbana na chuma,mawe na vyombo alivyotumia binadamu wa kwanza kufanya ukulima.

Njia ya kutalii eneo ambapo baadhi ya binadamu wa kwanza duniani waliaminika kuishi. Picha/ Richard Maosi

Jami hii ya watu uliwaleta pamoja wafugaji,wahunzi,waliokuwa wakiishi ndani ya mapango.

Kulingana na Leakey, miaka 8500 iliyopita ziwa Elementaita lilikuwa na vyanzo vyake kwa mito kutoka kwenye mlima wa Hyrax.

Lakini kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya anga, Hyrax ilibaki kama kisiwa kidogo kilichowavutia wanyama na watu waliofanya kuwa eneo la makazi.

Mlima wa Hyrax aidha ulitumiwa kama makazi ya mkoloni, ikiaminika ni sehemu iliyoinuka na kutoa taSwira nzuri ya ziwa Nakuru na Elementaita.

Makavazi haya ya kihistoria huwakaribisha watalii kwa sababu ya vivutio kama vile mabaki ya wanyama yaliyokaushwa, mafuvu, hafla za kitamaduni na sanaa ya kupiga picha.