Ichung’wah afichua walivyochenga Gen Z kisha kupitisha mswada tata wa 2024
Akizungumza wakati wa mazishi ya baba ya Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja Alhamisi, Oktoba 23, 2025, na mbele ya Rais Ruto aliyehudhuria, Ichung’wah alieleza kwamba kugawanya na kupitishwa kwa mswada huo kuliruhusu serikali kuanzisha tena miradi ya maendeleo iliyokuwa imekwama.
Ichung’wah alieleza kwamba baadhi ya vifungu chanya vilivyokuwa kwenye Mswada wa Fedha wa 2024 vilipotea baada ya mswada huo kukataliwa, jambo ambalo lilichelewesha utekelezaji wa baadhi ya mipango ya serikali.
Alisema kwamba muundo mpya wa mswada huo kwa kuugawa katika sehemu nne ulikuwa muhimu ili kuanzisha tena vipengele muhimu vilivyolenga kuongeza ukusanyaji wa mapato.Ichung’wah pia alidai kwamba kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 kulitokana na kushindwa kwa baadhi ya wafanyakazi wa serikali kuhimiza wananchi kuunga mkono sera za serikali, hali iliyowafanya Wakenya kutegemea taarifa zisizo sahihi.
“Maafisa wa serikali, tuwe na mtindo wa kuambia Wakenya ukweli, na mimi huwa ninajipata katika matatizo kwa sababu ya kusema ukweli. Mwaka uliopita, tulipata matatizo kwa sababu ya Mswada wa Fedha, hadi tukatoa mambo ambayo Wakenya walisema kupitia ushirikishaji wa umma kuwa hawayataki. Licha ya hatua hiyo, Wakenya bado wakakataa wakasema, ‘Msirekebishe. Tumekataa.’ Yale mambo mazuri ambayo yalikuwa katika mswada huo wakati rais hakutia saini yalipotea. Hiyo ndiyo maana mmeona tumechelewa katika utendakazi, kwa sababu ule mswada mzuri ambao ungetusaidia kukusanya ushuru, tuliutupa
.”Hata hivyo, mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemkosoa akisema kauli kama hizi zinaonyesha kiburi kile kile kilichojitokeza miongoni mwa baadhi ya wabunge kabla ya maandamano ya Gen Z mwaka wa 2024.