Idadi ya vijana yapungua kanisani kwa kushurutishwa wavalie suti
NA FRIDAH OKACHI
BAADHI ya viongozi wa makanisa mbalimbali nchini wanaendelea kutumia notisi na michoro ya picha za mavazi yasiyofaa ili kupitisha ujumbe na kuhimiza vijana kuvalia mavazi ya staha kurejesha maadili wakati wa kuhudhuria ibada.
Notisi hiyo iliwakataza kuvalia mavazi yaliyo kwenye kategoria za mavazi ya michezo, kaptula, marinda yanayofika kwenye magoti wasiingie maabadini.
Kijana Sir Erambo,29, aliambia Taifa Jumapili kwamba anaona ugumu kuhudhuria ibada ya kanisani tangu Oktoba 2023, pindi tu walipoweka notisi.
Bw Erambo alisema hatua hiyo “ni sawa na kunyimwa uhuru wa kuabudu.”
“Siku mojawapo ya Septemba 2023 nilienda kanisani nikapatana na notisi iliyotoa mwelekeo wa mavazi kwa kumulika mavazi ambayo hayafai maabadini. Mimi ni mmoja wa walengwa na nilianza kujiuliza iwapo ni mavazi yanayosikiliza ibada ama ni nafsi yangu,” akasema Bw Erambo.
Bw Erambo alishangazwa jinsi usimamizi wa kanisa ulivyofikia uamuzi huo bila kuzingatia kwamba wako vijana wa michezo ambao hawajawahi kumiliki suti.
“Mimi ni mchezaji wa soka na mavazi yangu mengi ni jezi na tracksuit. Sina mavazi mengine kutokana na shughuli zangu za michezo,” alieleza.
Hata hivyo kijana huyo alitaka kamati ya Kanisa kuandaa kikao na vijana kusuluhisha swala hilo.
“Niko tayari kukutana na usimamizi wa kanisa kuwauliza viongozi mambo mengi kuhusu mavazi,” aliongeza Bw Erambo.
Naye Bi Jencita Nyakio kutoka Riruta, Nairobi, alifichua amekosa kutangamana na waumini wengine trakriban miaka miwili sasa, baada ya mhubiri kutoa mfano akimrejelea yeye.
“Acha nifanye maombi nikiwa kwa nyumba. Jumapili moja pasta alinisimamisha na kuambia waumini wengine kwamba nguo kama niliyokuwa nimevaa, haifai,” akakumbuka Bi Nyakio.
“Ulikuwa ni mwaka 2022 ambapo pia Jumapili ya pili nilisimamishwa kama mfano mbaya na hapo nikajua kumbe wakiwa pale mbele, kazi yao ni kuangalia waumini jinsi wanavyokuwa wamevalia. Niliapa siwezi kuenda kwa kanisa jingine ikiwa hivyo ndivyo walivyo,” alisema Bi Nyakio.
Kiongozi wa ‘Youth for Christ na Young Adult’ katika kanisa Katoliki eneo la Dagoretti Fred Khaemba, aliambia Taifa Jumapili kwamba masharti hayo ni kutokana na vijana wengi kukosa busara ya kuteua mavazi ya heshima.
Alikiri kuwa baada ya kuchapisha picha hiyo, baadhi ya vijana waliondoka kanisani kwa muda mchache na kisha wakajipanga upya na idadi yao inaanza kuongezeka.
“Kuvalia long’i za mtindo wa kuraruka, na marinda yanayobana, miongoni mwa mavazi mengine, kunaleta picha mbaya. Kuna siku nilimfukuza kijana mmoja ambaye alikuwa amevaa nguo inayoishia juu ya magoti wakati tulifaa kuenda kwa parokia nyingine. Nilimtuma aende nyumbani avalie vizuri kabla ya kurejea,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi amewataka vijana kurudisha mtindo wa hapo awali kuvalia suti na mavazi mengine ya staha.