Idara ya mahakama yalaumiwa kwa kupotea kwa fedha
Na CHARLES WASONGA
IDARA ya mahakama inalaumiwa kuhusiana na Sh876 milioni zinazodaiwa kuelekezwa kwa majopo 21 lakini Mkaguzi wa Matumizi ya Pesa za Serikali Edward Ouko ameshindwa kubaini jinsi zilivyotumiwa.
Katika ripoti yake ya hivi punde ya mwaka wa kifedha uliokamilika mnamo Juni 2018 Bw Ouko anasema hawezi kuthibitisha kuhamishwa kwa pesa hizo kwa majopo hayo. Ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni Jumatano.
Anasema kuwa wakati wa ukaguzi wa matumizi ya fedha katika idara hiyo maafisa wake walifeli kuwasilisha stakabadhi za kuonyesha jinsi pesa hizo zilitumika
“Katika hali hii, uhakika kwamba Sh876,288 zilitumika katika majopo 21 hauwezi kuthibitishwa kuwa matumizi mazuri ya pesa za umma, ” Bw Ouko anasema katika ripoti hiyo.
Hata hivyo, Bw Ouko hakutoa orodha ya majopo hayo 21 wala sababu za kuundwa kwayo.
Mkaguzi huyo wa matumizi ya pesa za umma pia anaibua maswali kuhusu jinsi Idara ya Mahakama ilijilimbikizia deni la Sh613 milioni ambayo lilielekezwa katika mwaka wa kifedha a 2018/2019.
Stakabadhi
Kile kinachovutia hisia ya Dkt Ouko ni kwamba hakuna stakabadi za kandarasi, risiti za malipo, vyeti vya kikamilishwa kwa miradi na vocha za malipo kuthibitisha uwepo wa madeni hayo.
Kutokuwepo kwa stakabadhi hizo muhimu, Dkt Ouko anasema, usawa na uhalali wa madeni hayo hauwezi kuthibitishwa.
Mkaguzi huyo wa matumizi ya pesa za umma pia ameibua maswali kuhusu ujenzi wa mahakama 39 kote nchini kwa gharama ya Sh3 bilioni, kupitia ufadhili wa serikali kuu.
Kulingana na ripoti ya mkaguzi huyo ambayo iliwasilishwa bungeni Jumatano wiki hii, Dkt Ouko anasema licha ya kandarasi za ujenzi wa mahakama hizo kutolewa mnamo 2013, ujenzi wazo haujakamilishwa mpaka sasa.
Utathmini wa kiwango cha ukamilishwaji wa miradi hiyo kama ilivyoonyeshwa na Idara ya Mahakama kazi ya thamani ya Sh1.5 bilioni imeidhinishwa kwa malipo. Lakini maelezo kuhusu kuhusu vyeti vilivyotolewa na kiasi cha fedha kilicholipwa kwa kila mradi hayakuwasilishwa kwa maafisa wa ukaguzi.
“Kutokuwepo kwa vyeti vya kuonyesha ukamilishwaji wa miradi na stakabadhi za malipo, kupelekea kuwa vigumu kuthibitisha ikiwa miradi iliyolipiwa iliidhinishwa kulingana na kanuni za kandarasi iliyotiwa saini,” inasema ripoti hiyo.
Miradi
Katika mwaka wa kifedha uliopita, Dkt Ouko pia aliibua maswali kuhusu miradi kadha ya ujenzi iliyoendeshwa na Idara ya Mahakama maeneo mbalimbali nchini na ambayo yalikwamba licha ya malipo kutolewa kwa wanakandarasi.
Kwenye ripoti yake ya mwaka wa kifedha uliokamilika mnamo Juni 2017 Bw Ouko alisema kuwa kuna visa ambapo malipo yaliyotolewa kwa wanakandarasi yalizidi thamani ya kazi iliyofanywa. Hii ina maana kuwa kuna visa ambapo wanakandarasi walilipwa pesa nyingi kupita kiasi.
Haswa, Bw Ouko aliiua maswali kuhusu matumizi ya pesa wakati wa ujenzi wa majengo ya mahakama za Narok, Hamisi na Nakuru.
Alieleza kuwa kuna nyakati ambapo malipo yaliyotolea na Idara ya Mahakama kwa wanakandarasi yalizidi thamani ya kazi iliyotekelezwa ilhali katika visa vingine, wanakandarasi walilipwa pesa nyingi kupita kiasi.