Makala

IEBC: Makamishna tayari kukalia kiti moto

Na SAM KIPLAGAT, BENSON MATHEKA July 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAKAMISHNA saba wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiwemo mwenyekiti wa tume hiyo waliapishwa jana, huku Jaji Mkuu Martha Koome akisema ni jambo la kusikitisha kuwa mchakato wa kuwachagua maafisa hao wapya ulichukua muda mrefu.

Muda wa makamishna waliopita ulimalizika zaidi ya miaka miwili iliyopita, na kulikuwa na pengo la uongozi lililozuia IEBC kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.

Jaji Koome alisema pengo hilo la uongozi lilisababisha kusimama kwa shughuli muhimu kama vile tathimini mpya ya mipaka, jambo linalotishia demokrasia nchini.

“Sasa kwa kuwa Tume imeundwa upya, nawasihi muanze kazi kwa haraka kushughulikia majukumu ya kikatiba na kiutawala yaliyosalia, na pia muanze maandalizi ya mapema ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027,” alisema Jaji Koome.

Tume hiyo mpya itaongozwa na Bw Erastus Edung na waliapishwa baada ya Mahakama Kuu kuidhinisha uteuzi wao. Watatumikia kwa kipindi cha miaka sita.Makamishna hao ni Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol, na Fahima Araphat Abdallah.

Kwa kuapishwa, Bw Edung anaingia katika viatu vya watangulizi wake marehemu Wafula Chebukati na Samuel Kivuitu na Isaac Hassan ambao walitaja kazi hiyo kama kiazi moto. Tayari, upinzani umezua wasiwasi kuhusu uteuzi wao japo unasisitiza kuwa utamshinda Rais William Ruto licha ya kuteua watu wanaoita washirika wake kusimamia IEBC.

Marehemu Chebukati alisimamia chaguzi tatu za urais zilizopingwa kortini naye Kivuitu alisimamia uchaguzi wa 2007 uliofuatiwa na ghasia mbaya zaidi za baada ya uchaguzi nchini. Mnamo Agosti 15, 2022, siku ya kutangazwa kwa mshindi wa urais, taifa lilishuhudia mgawanyiko wa wazi kabisa ndani ya IEBC.

Makamishna wanne—Juliana Cherera (Naibu Mwenyekiti), Justus Nyang’aya, Francis Wanderi, na Irene Masit—walijitenga na matokeo yaliyotangazwa na Chebukati, wakisema “matokeo haya ni ya Chebukati peke yake.”

Bw Hassan, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa polisi, alisimamia uchaguzi wa 2013 chini ya iliyokuwa Tume ya Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC).

Uchaguzi wa urais wa mwaka huo ulipingwa katika Mahakama Kuu ya mgombeaji wa Muungano wa Cord Raila Odinga aliyeshindwa na Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee.

Jaji Koome alieleza kuwa imani ya umma kwa taasisi za serikali iko katika kiwango cha chini sana, na akaongeza kuwa kuna mtazamo unaokua kwamba mashirika ya umma yamejitenga na wananchi wanaowahudumia.

“Pengo hili la imani kati ya serikali na raia ni hatari. Kama mtu wa imani, naamini huu ni wakati wa kujenga upya—kuziba nyufa. Kwangu, ufa wa dharura zaidi ni kuporomoka kwa imani kati ya raia na taasisi za serikali,” alisema Jaji Mkuu.

Rais William Ruto alichapisha majina ya watu hao saba katika gazeti rasmi la serikali saa chache baada ya Mahakama Kuu kumkosoa kwa kuthibitisha uteuzi wao ilhali kulikuwa na amri ya mahakama iliyositisha mchakato huo.

Mahakama ilisema uteuzi huo haukukosa kuzingatia kanuni za kikatiba za ushirikishaji wa umma, mashauriano na vyama vya siasa, na upatikanaji wa taarifa.

Aidha, mahakama iliamua kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (NADCO) hayahusiani na suala la uteuzi, na kuapishwa kwa Mwenyekiti na Makamishna wa IEBC.

Kesi hiyo iliwasilishwa na Roy Omondi na Boniface Mwangi waliopinga mchakato ulioendeshwa na jopo la uteuzi wa makamishna wa IEBC pamoja na uteuzi uliofanywa na Rais Ruto kabla ya kuwasilisha majina kwa Bunge.

Walalamishi hao wawili pia walipinga sifa, uadilifu, ustahiki na uwezo wa walioteuliwa, pamoja na muundo wa orodha ya makamishna saba kwa msingi wa ukosefu wa usawa wa kikanda na kutokuwepo kwa mwakilishi wa watu wenye ulemavu.

Mwanasheria Mkuu na Bunge walitetea mchakato huo kwa kusema kuwa walalamishi hawakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yao, walitafsiri vibaya sheria husika, na kesi ilikiuka misingi muhimu ya kisheria kama kutenganisha madaraka na kutumia njia zote za kisheria kabla ya kuwasilisha kesi mahakamani.

Mahakama ilipokuwa ikitupilia mbali kesi hiyo, Majaji Roselyn Aburili, John Chigiti na Bahati Mwamuye walisema hakuna ushahidi wowote wa ukiukaji wa taratibu au ukiukaji wa katiba au upendeleo.