Ifahamu densi ghali yenye nidhamu ya juu ambayo ukichafua mavazi unakanyaga nje
NA KALUME KAZUNGU
LAMU imebarikiwa kwa kuwa na aina mbalimbali za ngoma au densi za asili.
Ni densi ambazo zinaenziwa pakubwa kwani hutambulisha, kuhifadhi na hata kuzitangaza tamaduni za wenyeji kindakindaki wa Lamu ambao ni Waswahili wa asili ya Wabajuni.
Miongoni mwa ngoma au densi hizo ni Kirumbizi, Goma na Uta.
Pia utapata Thwari La Ndhiya, Uta na nyingine zikiwa Lele Mama na Vugo.
Katika densi hizi, wahusika huwa na muonekano au mtindo tofauti wa mavazi na pia usakataji wao kulingana na mirindimo ya ngoma husika.
Ni Kaunti ya Lamu ambapo utapata densi ambayo washirika wake hucheza kwa njia ya kujishaua, kuonyesha maringo, madoido, machachari, makeke na pia nidhamu ya hali ya juu.
Densi hiyo ni Goma.
Lamu kuna aina mbalimbali za Goma kulingana na mahali wanachama hutokea.
Utapata Goma La Barani ambalo hujumuisha wakazi, wengi wao wakiwa ni wale wa kutoka vijiji vilivyokumbwa na vita vya Shifta vya miaka ya sitini (1960s).
Vijiji hivyo ni Rubu, Simambae, Kiunga, Mvundeni, Mwambore, Mkokoni na Ishakani.
Pia kuna Goma la Siyu ambalo hujumuisha wakazi wa Siyu pekee na lile la Faza, ambalo wenyeji wa Faza wanalitambua kwa asili yao kama Bati.
Aina zote hizo za densi ya Goma hujumuisha karibu watu 30 wanaoshiriki kwa awamu moja.
Utapata karibu watu 20 ambao jukumu lao ni kushika bakora ilhali wengine karibu 10 wakishughulikia kupiga ngoma tofauti tofauti ilmradi walete mrindimo unaostahili.
Goma pia hujumuisha ngoi ambaye huimba huku akiwaelekeza washiriki wengine kwa makini jinsi wanavyofaa kuzungusha bakora zao ilmradi umaridadi wa Goma uzingatiwe.
Ni densi inayoashiria hadhi ya juu kwani washiriki wote huwa wamevalia kanzu za bei ghali na ambazo zimepigwa pasi iliyokoleza, hivyo kuonekana nadhifu si haba.
Mwenyekiti wa Baraza La Wazee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee, anataja Goma kuwa densi inayozingatia nidhamu na utaratibu mkuu ikilinganishwa na densi nyingine zozote zipatikanazo eneo hilo.
“Goma ni miongoni mwa densi zinazotambulisha mila na tamaduni zetu. Hii ni densi ambayo haichezwi vivi hivi kutokana na hadhi yake ya juu. Pengine utaipata ikichezwa wakati wa kipindi cha Mfungo Sita au wakati kuna wageni mashuhuri kama vile Rais na wengineo. Ni densi ya heshima na ina utaratibu wa aina yake,” akasema Bw Mbwana.
Anasema kinyume na densi zingine zozote za asili ya Lamu, Goma huwa ni ghali, hasa wa wale wanaokodisha kupata tumbuizo.
“Kwa vile inahusisha washiriki wasiopungua 30, wanaokodisha tumbuizo ya Goma ni watu wakubwa, ikiwemo viongozi wa kisiasa, Wabunge au magavana. Utapata kukodisha Goma si chini ya Sh100,000 kwani wanaostahili kutumbuizwa lazima uwalipie nauli,” akaeleza Bw Mbwana.
Ali Athman ambaye ni mchezaji na shabiki mashuhuri wa Goma anasema ni kupitia densi hiyo ambapo aliweza kujipatia mwenza (mke).
Anasema madoido, mbwembwe na unadhifu unaoambatana na densi ya Goma huwavutia wengi.
“Wajua hii densi ya Goma unaposhiriki lazima uwe safi kimwili na mavazi yako ni muhimu yasalie kuwa nadhifu. Hayafai kuchafuka. Hilo tu lilinifanya mimi kujinyakulia mrembo aliyependezwa na usafi wangu wa mwili na mavazi na hadi leo yeye ndiye mama watoto wangu,” akasema Bw Athman huku akicheka.
Unaposhuhudia densi ya Goma, utapata wahusika wakiinma upande mmoja kwa wakati mmoja huku bakora zao wakiziweka begani kwa pamoja.
Aidha utawapata washirika hao hao wakiinua bakora zao juu kwa pamoja, ilmradi waunde shepu ya kupendeza watazamaji.
Mara nyingi wanaoshiriki Goma pia hutanua vifua vyao, hivyo kuwa na muonekano wa watu wenye majisifu, kujitukuza na wenye uwezo katika densi hiyo wanayoshiriki.
Wapiga ngoma nao hawaachwi nyuma kwa umaridadi wao wa kuzicharaza ngoma ili kuleta mirindimo ya taratibu ambayo inaendana na densi hiyo.
Mara nyingi wanachama wa Goma hutengeneza mduara maalum au kupanga foleni wakati wakicheza, hivyo kuwa na mtazamo au muonekano maridhawa kabisa.
Lakini je, aina hii ya densi ina umuhimu gani kwa wanaoienzi?
Bw Omar Yusuf, mkazi wa Siyu, anasema mbali na kukuza na kuhifadhi tamaduni za jamii, Goma pia ni kitega uchumi kwa wachezaji.
Bw Yusuf anasema mara nyingi wamealikwa kutumbuiza kwenye hafla mbalimbali, iwe ni za ndani ya Lamu, kaunti zingine za nje ya Lamu au mataifa jirani.
Anasema mialiko hiyo huwa si bure bali hujumuisha donge nono kwa washiriki wa Goma.
“Wakati wa Tamasha za Utamaduni wa Lamu zinazoadhimishwa kila mwaka kwa mfano, sisi wanachama wa Goma la Siyu hualikwa kutumbuiza watalii na wageni, hivyo kujipatia fedha nyingi. Isitoshe, sisi hupokea mialiko hata ya mataifa ya nje ambapo hujipatia mtaji,” akasema Bw Yusuf.