Makala

IG Kanja ataka polisi waache kuchukua hongo, waridhike na mishahara yao

Na WACHIRA MWANGI March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, amewaonya maafisa wa polisi dhidi ya kushiriki katika vitendo vya rushwa, akiwataka waridhike na mishahara yao na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo cha Polisi cha Mbaraki, kilichojengwa kupitia Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF), Kanja alisisitiza kuwa maafisa wa polisi wanapaswa kuhudumu kwa uaminifu na kufuata sheria.

“Tunapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kuheshimu sheria. Polisi ni waajiriwa wa wananchi, na mishahara yetu inatoka kwao. Kwa hivyo, tuache tabia ya kudai hongo na tutosheke na mishahara tunayopata,” alisema IG Kanja.

IG Kanja pia alilaani vikali uanzishaji wa vituo vya polisi visivyoidhinishwa, akisema kuwa kuna utaratibu maalum wa kufuata.

“Ni makosa kufungua kituo cha polisi bila kufuata taratibu zinazofaa. Wananchi wanaweza kushiriki katika mjadala wa umma pamoja na viongozi wao, kisha maombi yao kuwasilishwa kwa wakuu wa polisi wa kaunti ndogo kabla ya kufika ofisini kwangu.

Ikiwa wanasisitiza kuwa na kituo cha polisi, basi lazima wafuate mchakato rasmi,” alifafanua Bw Kanja.

Haya yanajiri siku chache baada ya mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 26 na mwanaharakati wa kisiasa, Collins Leitich maarufu kama Chepkulei, aliyeunda kituo cha doria cha polisi bila idhini katika eneo la Cherus, Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu.

Bw Leitich, mkazi wa Asis katika eneo la Ndugulu, anaripotiwa kuanzisha Kituo cha Doria cha Cheboror kwa kupaka rangi jengo la kukodisha kwa rangi rasmi za Huduma ya Kitaifa ya Polisi, kisha kulipangilia kwa vyumba vya mahabusu na ofisi.

Kituo hicho kilifanya kazi kwa muda wa takriban miezi sita bila idhini au ufahamu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi.

IG Kanja alieleza kuwa kufunguliwa kwa Kituo cha Polisi cha Mbaraki kutaimarisha usalama kwa wakazi wa eneo hilo, ambao hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za polisi.

“Nawashukuru viongozi wa eneo hili kwa kuhakikisha kuwa sasa wakazi wana kituo cha polisi karibu. Mazingira mazuri ya kazi yanahakikisha kuwa maafisa wetu wanatoa huduma bora na kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aidha, alihimiza ushirikiano kati ya polisi na wananchi kwa kusema, “Usalama ni jukumu la kila mtu. Wananchi na polisi wanapaswa kushirikiana kuhakikisha jamii yetu ni salama.”

Bw Kanja pia alizungumzia matukio ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Nairobi baada ya ziara ya Rais William Ruto, akiahidi kuwa wahalifu waliorekodiwa kwenye kamera wakipora wananchi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat, naye aliwataka wakazi wa Mombasa kushirikiana na polisi katika vita dhidi ya mihadarati, pombe haramu, na uhalifu.

“Hatutaruhusu watoto wetu kuangamizwa na dawa za kulevya. Lazima tupambane na uuzaji wa pombe haramu na bangi hadi tutakapozikomesha kabisa,” alisema Bw Lagat.

Mbunge wa Mvita Mohamed Soud alisema kuwa wakazi wa Mvita sasa wanaweza kuhisi usalama baada ya kuanzishwa kwa kituo hicho kipya.

Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake kuhusu utendakazi wa baadhi ya maafisa wa polisi, akisema kuwa kuna changamoto ya mawasiliano kati ya wananchi na maafisa wa usalama.

“Mwananchi anaposhikwa anatafuta mwakilishi wake, lakini anapopiga simu kwa polisi hapokelewi,” alisema.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa hatotetea wahalifu au watu wanaojihusisha na dawa za kulevya. “Sitaenda kutetea muuzaji wa bhangi au mtumiaji wa dawa za kulevya. Hao si marafiki zangu,” aliongeza.

Aidha, alilalamikia baadhi ya maafisa wanaotumia mamlaka vibaya kwa kushurutisha wananchi waliokamatwa kwa makosa madogo kulipa hongo ili waachiliwe. “Wengine wanakamata watu kwa makosa madogo kisha wanataka hongo ya Sh30,000 au Sh50,000. Wanachukua simu za watu na kujitumia pesa kupitia M-Pesa,” alidai.

Aliwataka polisi kuwa waadilifu na kuzingatia misingi ya huduma kwa wote kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za kikosi hicho.

Bw Soud pia alihimiza polisi kuwa na utu na kuhakikisha kuwa wanyonge hawaonewi huku wahalifu sugu wakiachwa huru. “Polisi wanajua maeneo ambayo wahalifu wanapatikana, lakini badala ya kuwakamata, wanawasumbua wanyonge,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Mombasa, Peter Kimani, aliahidi kuongeza doria, hasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ili kuwalinda waumini na wafanyabiashara.

“Kituo cha Mbaraki sasa kimeimarishwa rasmi. Tumejipanga kuhakikisha kuwa wakazi wa Mombasa wanapata huduma bora na kwa wakati unaofaa,” alisema Bw Kimani.

Uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Mbaraki ni hatua muhimu katika kuboresha usalama wa Mombasa, huku viongozi wakihimiza ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama ili kuhakikisha amani na utulivu.