IG MTEULE: Hillary Nzioki Mutyambai
Na SAMMY WAWERU
HILLARY Nzioki Mutyambai, Inspekta Mkuu mteule wa Polisi (IG) na ambaye aliteuliwa na Rais kuongoza zaidi ya maafisa 100, 000 angekuwa Papa Mtakatifu wa Kanisa la Katoliki iwapo ndoto zake za utotoni zingezaa matunda.
Bw Nzioki ambaye Alhamisi alipigwa msasa na kamati ya pamoja bungeni (bunge la kitaifa na seneti) ya usalama, ikiwa ataidihinishwa macho yote yataelekezwa kwake kukabiliana na suala tete la mashambulizi ya kigaidi, uhalifu, kuongoza kukamata washukiwa wakuu katika vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi na kufanikisha uchaguzi mkuu wa 2022.
Masuala hayo manne yametajwa kama kibarua kikuu kinachomuandama katika utendakazi wake wa miaka minne ijayo, ambapo akikamilisha awamu yake sawa na mtangulizi wake Joseph Boinnet hatateuliwa tena kwa wadhifa huo.
Afisa huyu alizaliwa 1964 katika Hospitali ya Pumwani, Nairobi na kulelewa kaunti ndogo ya Mwala, Machakos, katika familia yenye msingi wa Kikristu. Alisomea shule zilizofadhiliwa na Katoliki, na anasema nusra ajiunge na mafunzo ya ukasisi.
Mwaka wa 1990 Bw Mutyambai alifunza masomo ya Bayolojia, Hesabu na Fizikia katika shule ya upili ya Pope Paul VI Junior Seminary, aliyosomea.
Hata hivyo, washauri wake 1991 walimsihi kujiunga na kikosi cha polisi.
Ana Shahada ya Masuala ya Sayansi na Kilimo, kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) ambapo baadaye alisomea Shahada ya Uzamili Masuala ya Usalama wa Kitaifa kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia. Pia IG huyu mteule ana cheti cha uongozi wa kukabiliana na uhalifu kutoka Chuo Kikuu cha New Orleans, Louisiana, Marekani.
“Maisha yangu katika shule za Kikatoliki yalichochea utu nilionao na kunifanya niwe mnyenyekevu. Kuna wanaolalamikia hulka zangu za unyenyekevu, zimekolea nafsini na ni vigumu kubadilisha,” anasema Mutyambai.
Ni mchache wa maneno hasa yanayochochea ubishi, Bw Mutyambai anasema habari za uteuzi wake kumrithi Joseph Boinnet alizipokea kwa kishindo.
“Bayana, sikutarajia kuteuliwa. Uteuzi umejiri, na nikiidhinishwa na bunge nitachukua hatamu na kuonesha jitihada zangu,” anaeleza.
Mkuu wa kitengo cha ujasusi (NIS), Wachira Kameru, kwenye pendekezo lake kwa Rais anamfafanua Mutyambai kama mtu “mtulivu, wa kutegemewa, mwaminifu, mpole, rahisi kuongea naye, mkakamavu na kiongozi.”
Wengine waliompendekeza kwa wadhifa huo ni Michael L’Estrange, aliyeongoza Chuo cha Kitaifa cha Masuala ya Usalama, Australia.
Uteuzi wake umejiri wakati ambapo maafisa wa polisi wanalalamikia suala la marupurupu hasa ya nyumba, upewaji madaraka, kuunganishwa kwa kikosi cha askari tawala (AP) na wale wa kawaida pamoja na sare mpya. “Nikiidhinishwa nitaimarisha utendakazi wa NPS, kwa kuangazia changamoto zinazofika maafisa,” akaambia kamati ya pamoja ya usalama bungeni, iliyomhoji.
Pia, afisa huyu ameahidi kushirikiana na asasi husika katika vita dhidi ya ufisadi, kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi, uhalifu na unyanyasaji wa kijinsia, huku akipongeza juhudi za mtangulizi wake kusaidia kuleta mabadiliko katika NPS.
Ni muhimu kutaja kuwa uteuzi wake umejiri wakati kuna malalamishi ya utovu wa nidhamu miongoni mwa maafisa wa polisi haswa ufisadi, mauaji ya kikatili na kuhangaisha raia.
“Ninajua safari ya wadhifa huu haitakuwa rahisi. Jukumu nililotwikwa lina mengi, wajibu wangu utakuwa kuleta uaminifu na kuangazia changamoto zinazotuandama. Mimi si mgeni katika idara ya usalama, nimekuwamo ndani karibu muda wangu wote wa utendakazi,” anasema.
Anasema atashirikisha wataalamu wa masuala ya usalama na uongozi, ili kulainisha kikosi cha polisi katika nyanja zote. “Hii italeta pamoja maafisa wote, waweze kufanya kazi kwa kushirikiana. Itaondoa dhana ambapo maafisa wakuu wanajiona kuwa wao ni mababe na kunyanyasa wadogo wao, wote nitawasawazisha,” anasema.
Kuimarisha
Anafichua kuwa mbali na majukumu yake katika NIS, amekuwa kiungo muhimu katika kusaidia kuimarisha usalama wa kitaifa.
Hadi kuteuliwa kwake, Mutyambai alikuwa akihudumu kama naibu mkuu wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi nchini, na anasema hatua hii imemuwesha kuimarisha sekta ya usalama.
“Pia nimekuwa nikishirikiana na timu za pamoja za kiusalama ikiwamo ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), kuchunguza na kushtaki washukiwa wa kigaidi,” anaeleza.
Mmoja wa marafiki wake wa karibu anamtaja kama mpelelezi wa hadhi ya juu, akitambulika ulimwenguni kukabiliana vilivyo na wahalifu na magaidi. “Analeta ukwasi wake wa tajiriba ya miaka 28 kikosini kama mpelelezi na mtekelezaji sheria. Ana uzoefu wa kuimarisha wafanyakazi, kuwapa mafunzo na uongozi,” mwandani wake akaambia Taifa Leo.
Anasema maafisa wa polisi watajivunia jitihada zake, kunoa wale chipukizi, kuongoza kwa mfano mwema na kuunga mkono wachapakazi, bila kusahau kuleta umoja kikosini.