Makala

IMF yataka utajiri wa Rais na maafisa wakuu serikalini kuwekwa wazi

Na PATRICK ALUSHULA, CHARLES WASONGA January 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HAZINA ya Kitaifa itaanza kuanika utajiri wa maafisa wakuu wa serikali wakiwemo Rais na naibu wake kama mojawapo ya hatua za kuimarisha uwajibikaji na maadili serikalini, Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) linavyopendekeza.

Kulingana na Taarifa kuhusu Sera ya Bajeti (BPS) ya 2025 iliyochapishwa juzi, serikali sasa imejitolea kuweka hadharani mali ya maafisa hao kupitia mfumo wa dijitali.

Hata hivyo, haijataja siku kamili ambayo hatua hiyo itaanza kutekelezwa.

Hayo yanajiri baada ya IMF kuhoji sheria zinayolenga kusawazisha kanuni ya kutangazwa kwa mali ya maafisa wa serikali na sheria kuhusu mgongano wa kimasilahi ili ifikie viwango vya kimataifa.

IMF ilikuwa imeiambia Kenya kwamba sheria hizo zina mapengo yakiwemo ukosefu wa njia za kubaini uhalali wa mali zilizotangazwa.

Hazina ya Kitaifa inasema ufisadi, ikiwemo ubadhirifu wa rasilimali za umma, inasalia kuwa “tishio” kubwa katika kufikiwa kwa malengo ya Ajenda ya kiuchumi ya utawala wa Rais William Ruto, ya kuendeleza uchumi kuanzia mashinani (BETA).

Aidha, inaamini kuwa kuwekwa hadharani kwa utajiri wa maafisa wakuu kutaimarisha uongozi.

“Sasa serikali itakuwa ikichapisha maelezo kuhusu utajiri wa maafisa wake wakuu,” Hazina ya Kitaifa inasema.

Hiyo ina maana kuwa mtu yeyote anayesaka maelezo kuhusu mapato, mali na madeni ya watu wanaoshikilia nyadhifa serikalini atapata kuwa fomu zenye maelezo hayo kwenye tovuti ya Hazina ya Kitaifa.

Itakuwa tofauti na hali ilivyo sasa ambapo maafisa wa umma hutangaza mali yao lakini maelezo kwenye fomu za kutangaza mali husalia siri.

Waziri wa Fedha John Mbadi na Katibu wa Wizara hiyo Chris Kiptoo hakujibu simu zetu na jumbe fupi tulipotafuta ufafanuzi kuhusu ni lini hatua itaanza kutekelezwa au ikiwa wizara imeanzisha mfumo utakaotumika katika mtindo huo wa kuanika mali ya maafisa wakuu.

Ikiwa Hazina ya Kitaifa itatekeleza mpango huo, Wakenya wataweza kujua utajiri halisi wa Rais, Naibu wake, mawaziri, wabunge, maseneta, magavana, Jaji Mkuu, wakuu wa mashirika ya serikali na maafisa wengine wa ngazi za juu.

Afisi za baadhi ya maafisa hawa zimeitajwa katika ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kufeli kuwajibikia mabilioni ya pesa za umma.

Japo mawaziri, makatibu wa wizara na mabalozi wateule hutaja thamani ya mali yao wanapopigwa msasa na wabunge kubaini ufaafu wao kwa nyadhifa hizo, baadhi yao huchelea kutoa thamani halisi ya mali yao.

Aidha, ongezeko la utajiri wao wakiwa afisini huwa halitangazwi.

Aidha, haijulikani ikiwa Hazina ya Kitaifa itapendekeza mageuzi yafanyiwe Kanuni ya Kupata Taarifa  zinazohifadhiwa na Serikali ya 2023 au Mswada wa Kuhusu Mgongano wa Kimasilahi wa 2023 ili kufanikisha mpango wa kuanikwa kwa mali ya maafisa wakuu serikali.

Kanuni ya kuhusu kupatikana kwa taarifa zinazohifadhiwa na serikali inatoa taratibu za kufuatwa na asasi za umma katika kufichua taarifa kama hizo. Kwa upande mwingine Mswada kuhusu Mgongano wa Kimasilahi unawazuia maafisa wa umma kushirikia vitendo vinavyokinzana na masilahi ya umma.

Rais Ruto anayepokea mshahara wa Sh1, 650,000 kila mwezi, ni miongoni mwa maraisa wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi ikilinganishwa na utajiri wa nchi zao.

Aidha, Dkt Ruto ni miongoni mwa viongozi matajiri zaidi nchini Kenya na barani Afrika.