Ipo haja ya kuzingatia lugha za kiasili
NA STEVE MOKAYA
Hapo Februari 21, dunia iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha za Mama. Jamii mbalimbali ulimwenguni husherehekea lugha zao za awali, na kujadili mbinu za kuziimarisha.
Taifa letu la Kenya lina makabila 43 na lugha za mama sawia. Ila, kwa bahati mbaya, siasa potovu za humu nchini zimetufunza kutumia lugha zetu za awali kuendeleza chuki na utengamano miongoni mwetu.
Lakini ukweli ni kwamba, lugha za mama zinao umuhimu mkubwa, jinsi tutakavyoona hivi punde.
Kwanza kabisa, lugha za mama ni fahari ya taifa letu la Kenya. Kuwa na lugha mbalimbali katika taifa moja ni sababu tosha kwa taifa hilo kujivunia.
Jamii mbalimbali hutunga na kuimba nyimbo mbalimbali kwa lugha zao, na nyimbo hizi hutumika kuliuza taifa letu kwa watalii.
Wageni kutoka mataifa mbalimbali huja Kenya kutumbuizwa na kwaya hizi za jamii mbalimbali. Bila shaka, taifa hujipatia hela za kigeni.
Pesa hizi hutumika katika kufanikisha maendeleo nchini. Pili, lugha za mama huwa ni nguzo muhimu katika kuwaunganisha watu wa jamii moja.
Watu wanaongea lugha moja ya huja pamoja kwa urahisi, na kufanya mambo kwa ushirikianao. Kwa mfano, vyombo vya habari vinavyotumia lugha za mama katika mawasiliano yao huwaunganisha watu kwa urahisi.
Vyombo hivi huwapa wanajamii mafunzo mbalimbali ya kujiendeleza. Hii ni njia rahisi sana ya kutoa mafunzo, kwani waliosoma na wale ambao hawajasoma huweza kuelewa, hasa wanapozungumziwa, kama vile kwenye redio.
Hata zaidi, jamii mbalimbali zinapokuwa na utangamano, umoja huo husambaa katika kiwango cha kitaifa, na nchi huwa na umoja.
Isitoshe, lugha za mama hutumika kama kitambulisho miongoni mwa watu wa jamii moja. Ushawahi kuwa kwenye kituo cha magari, watu wakiwa wametulia, pasipo na yeyote wa kuongea na mwingine?
Ghafla, simu ya abiria mmoja inapigwa, na mpokezi anazungumza kwa lugha ya mama?Ni nini hufuata? Mara nyingi, baada ya kukata simu, unaona mtu ama watu kadhaa waakimkaribia na kuanza mazungumzo kwa lugha iyo hiyo iliyotumika.
Kisha unapata watu waliokuwa wametulia wakichapa gumzo. Mbona wakaanza kuongea?
Lugha iliwatambulisha na kuwavutia karibu. Fauka ya hayo, lugha za mama hutumika kuwaelekeza watoto wanapokua.
Wanapewa mafunzo kwa ishara pamoja na maneno kadhaa ya lugha ya mama. Kadhalika, wao huiga yale yanayosemewa na wale walio karibu nao.
Ni kwa sababu hii shule za msingi katika miaka michache iliyopita zilikuwa zinawatahini wanafunzi katika somo la lugha ya mama.
Wanafunzi kuanzia chekechea hadi darasa la tatu wangefunzwa kikamilifu kuhusu misamiati na mila na desturi za jamii zao, na lugha zao, na kwa lugha zao za mama.
Lugha za mama zimekuwa na umuhimi mkubwa tangu awali. Ila sasa, katika miaka ya hivi karibuni, matumizi ya lugha hizi yameanza kupungua sana, na ni jambo la kusikitisha.
Ni jambo la kuatua moyo sana kuwa katika taifa letu, lugha za mama zinaangaliwa kama za watu wa tabaka la chini.
Jambo hili limepelekea wazazi wengi kuasi kabisa mafunzo ya lugha zao kwa watoto wao. Badala yake, wanawafunza kuongea Kiingereza sana na Kiswahili kidogo.
Hata hivyo, si kweli kuwa lugha za mama ni lugha za maskini, kwani hata Rais Uhuru Kenyatta, huongea lugha ya Kikuyu mara moja moja kwenye hadhara za jamii ya Agikuyu.
Je, rais wetu ni maskini? Je, rais wetu ni mtu ambaye hajakengeuka? Na jambo la kusikitisha hata zaidi, wanafunzi wa vyuo vikuu wamechangia pakubwa katika kuziangamiza lugha hizi.
Wanafunzi wengi katika vyuo vikuu huabika sana kuongea lugha zao za mama.
Wengi huona kuwa wakisikika wakiongea lugha hizo hawatachukuliwa kama watu waliosoma. Lakini bado,fikira hizo ni potovu na si za kweli, kwani tumewaona wasomi, hata maprofesa, wakizungumza lugha zao, tena kwa fahari.
Kwa mfano, Profesa Ngugi wa Thiong’o, ameandika vitabu katika lugha ya Kikuyu.
Ipo haja ya kubadili mitazamo yetu kwa lugha zetu za mama. Ipo haja ya kupunguza matumizi ya sheng ili kuziendeleza lugha zetu za mama na zile za kitaifa.
Kadhalika, wazazi wanafaa waanze kuwafunza watoto wao, wafahamu lugha zao za mama. Ni aibu kubwa kujua lugha za kigeni, ilihali hujui ama unajifanya kutojua lugha yako ya mama.