Makala

Itumbi aahidi urejeo wa kumulikwa macho na kampuni ya Worldcoin

April 2nd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI
BW Dennis Itumbi ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto sasa anataka kampuni ya Worldcoin iliyokuwa ikimulika watu macho irejeshwe kuhudumu hapa nchini.

Hii ni baada ya kampuni hiyo inayojulikana kama OpenAI, kutimuliwa nchini mnamo Agosti 2, 2023.

Inamilikiwa na Sam Altman.

Kabla ya kufurushwa, Wakenya hasa vijana walikuwa wameikumbatia ambapo kujisajili kuwa mwanachama ilikuwa ni kupitia kupigwa skani ya jicho.
Akizungumza wikendi katika chuo kikuu cha Mt Kenya (MKU), Bw Itumbi alisema atashinikiza kampuni hiyo irejeshwe.

“Nitaandaa harakati mahususi sawa na vita vya utetezi hadi irejelee huduma hapa nchini,” Itumbi akasema.

Alisema harakati hizo ni za kusaidia kampuni hiyo kuwafaa vijana kiuwekezaji kupitia ununuzi wa sarafu za Worldcoin.

Guru huyo wa masuala ya kidijitali, alisema kwamba wakati kampuni hiyo ilifurushwa nchini sarafu hiyo ilikuwa na thamani ya Sh7 na ambapo kwa sasa imepanda hadi Sh48.

“Wale walikuwa wamenunua sarafu hiyo ikiletwa hapa Kenya kwa sasa wangekuwa na uwezo wa kujipa faida ya Sh41 kwa kila sarafu. Kabla ya mwaka mmoja kuisha, natazamia kwamba bei itakuwa imefika hadi Sh2, 000,” alielezea.

Matamshi ya Bw Itumbi ambaye hawezi akakosa ufahamu wa utendakazi wa serikali, yanaipa uzito taswira kwamba huenda utawala wa Rais Ruto umeingia katika mkataba wa kurejesha kampuni hiyo hapa nchini.

Taharuki ilitanda wakati kampuni hiyo ilizindua harakati zake nchini kupitia kupiga picha ndani ya macho ya wasajiliwa na kisha kumtunuku kila mwanachama mpya zawadi ya Sh8, 256.

Bw Itumbi alihimiza wanafunzi na wadau waliokuwa katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mt Kenya waweke macho yao tayari kwa msururu mwingine wa kumulikwa kwa miale ya kamera za kidijitali.

Idadi kubwa ya vijana walijitokeza kumulikwa macho na kujipatia hela, kabla ya kampuni hiyo kufukuzwa Kenya.

Uhalisia wake ulitiliwa shaka, wakosoaji wakilalamikia uwezekano wa data za walioshiriki kudukuliwa.

Dennis Itumbi (aliye na shati la rangi ya kahawia) alipowasili katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya (MKU) Mjini Thika kwa hotuba maalum. PICHAMWANGI MUIRURI