Jaji Grace Nzioka: Ninatoa hukumu bila uoga wowote
NA WANDERI KAMAU
JAJI Grace Nzioka wa Mahakama Kuu amesema kwamba huwa hahofii maisha yake, licha ya maamuzi ambayo amekuwa akifanya kuhusu kesi tofauti.
Jaji Nzioka alisema hayo siku chache baada ya kutoa uamuzi kuhusu kesi ya mauaji iliyomkabili Joseph ‘Jowie’ Irungu, ambapo alimhukumu kifo.
Jowie alipewa hukumu hiyo baada ya kupatikana na makosa ya kumuua mfanyabiashara Monicah Kimani mnamo Septemba 19, 2018.
Jaji Nzioka alijipatia umaarufu miongoni mwa Wakenya kwa ufahamu mkubwa wa lugha ya mahakama na lugha nyepesi aliyotumia katika kumhukumu Jowie.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, jaji huyo alisema kuwa huwa anatembea kama Mkenya wa kawaida, bila kuogopa lolote.
“Sijawahi kuhofia hata siku moja. Huwa natembea kama raia wa kawaida. Ningetaka kuliweka hili wazi; ikiwa unafanya kazi yako kwa uadilifu na huna nia ya kumdhulumu yeyoye, huna haja ya kuogopa,” akasema Bi Nzioka.
Jaji huyo aliongeza kwamba huwa anamwogopa Mungu kwani ndiye mlinzi mkuu.
“Hakuna siku ambayo nimejifungia kwa nyumba kutokana na uamuzi niliyofanya. Naamini kwamba huwa ninafuata sheria na hilo pekee linatosha,” akasema.
Alisema kwamba ameridhika na kazi yake, na huwa anaifanya kutoka kwa moyo wake.
Hata hivyo, alisema kuwa kama kazi nyingine, huwa anajifunza kutoka kwa makosa anayofanya.
“Ikiwa unapenda kazi yako na huwa inakuridhisha, itakulazimu uamke ili kwenda kuwahudumia raia,” akaongeza.
Jaji Nzioka amehudumu katika Idara ya Mahakama kwa muda mrefu; ambapo amepanda ngazi hadi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Amehudumu katika vitengo kadhaa, baadhi vikiwa; kitengo cha uhalifu wa kibiashara na makosa ya jinai.
Lakini Jowie alitoa notisi Ijumaa kwa Mahakama ya Rufaa akionyesha nia ya kukata rufaa.