• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Jamii ya Wakore hatarini kumezwa kabisa na makabila mengine

Jamii ya Wakore hatarini kumezwa kabisa na makabila mengine

NA KALUME KAZUNGU

JAMII ya wachache ya Wakore ndio inayotambulika kuanzisha kijiji cha Koreni kilichoko eneobunge la Lamu Magharibi.

Kijiji hicho leo hii kinatambuliwa kuwa ngome ya jamii za wafugaji, hasa Wasomali na Orma.

Waswahili wa asili ya Wabajuni, Wasanye, na Wagiriama na kabila la Wakikuyu na wengineo waliojenga makao Pwani, pia huishi kwenye kijiji hicho cha Koreni miaka ya sasa.

Mzee wa Nyumba Kumi na Mwenyekiti wa Jamii ya Wasomali wanaoishi Koreni, Bw Muhumed Kalmei, anasema kijiji hicho kilibuniwa miaka ya zamani kabla ya ukoloni.

Ikumbukwe kuwa Wakore, ambao ni jamii ya wachache nchini, miaka ya themanini (1980s) idadi yao ilikuwa finyu, ambapo ni kati ya 200 na 250 pekee ndio waliopatikana Kenya.

Kulingana na historia ya miaka kabla ya 1870, Wakore wanadaiwa kuwa miongoni mwa makabila tanzu ya Maa kwenye eneo la Kati nchini Kenya.

Baada ya kukabiliwa na kushindwa na kabila la Purko Maasai miaka hiyo ya 1870s, Wakore wanasemekana kutorokea Kaskazini Mashariki mwa Kenya, ambako nako huko walichukuliwa mateka na jamii ya Wasomali.

Baada ya kuhudumu kwa miaka mingi kama watumwa katika nyumba na familia za Wasomali, Wakore waliachiliwa huru kupitia usaidizi wa mabeberu wanajeshi wa Uingereza mwishoni mwa Karne ya 19.

Historia pia inaeleza kilichowasukuma Wakore kuja Lamu katikati mwa kipindi cha karne ya 20 kwamba kichocheo kikuu kilikuwa baada ya wao kupoteza mifugo wao wote.

Isitoshe, kwa wakati huo, Wakore walikuwa tayari wamepoteza kabisa lugha yao iliyoshabihiana na ile ya Maa.

Katika ulimwengu wa leo, jamii hiyo ya Wakore wa Maa imepoteza lugha yake ya asili, hivyo kuzungumza lugha ya Kisomali na hata kupokezwa na kuzikubali mila na desturi za Wasomali.

“Kijiji hiki cha Koreni kilichipuka miaka kabla ya ukoloni. Jamii ya wachache ya Wakore waliotorokea hapa ndio walioibuka na jina la kijiji hiki cha Koreni,” akatanguliza Bw Kalmei.

Mzee Mwanahistoria wa Koreni ambaye ni Afisa wa Nyumba Kumi na pia Mwenyekiti wa Jamii ya Wasomali katika Kaunti ya Lamu, Muhumed Kalmei. Asema licha ya Wakore kuanzisha kijiji cha Koreni, wanajamii hao wako katika hatari ya kuangamia kwa sababu wanamezwa na makabila mengine. PICHA | KALUME KAZUNGU

Baadaye Wasomali walitagusana vyema na Wakore kiasi kwamba walianza kuoana.

Kwa sababu Wakore idadi yao ilikuwa ndogo si haba waliishia kumezwa na Wasomali na hata Waswahili Wabajuni wanaoishi Koreni.

“Leo unapotembelea Koreni, kumbukumbu ya Wakore iliyosalia ni jina la kijiji tu ila wao wenyewe kama kabila huwezi kuwapata popote. Yaani wanaoishi Koreni ya sasa ni Wasomali, Orma, Waswahili wa asili ya Wabajuni, Sanye, Wagiriama, na pia Wakikuyu na makabila mengineyo,” akaongeza.

Kulingana na Mzee Kalmei, Wakore wote kijijini hapo wamemezwa kabisa na jamii nyinginezo.

“Kumbukumbu yao ya pekee ni jina Koreni lililopewa kijiji chetu” akasema.

Kijiji cha Koreni leo ni makazi kwa zaidi ya watu 400.

Licha ya idadi kubwa ya wakazi kuwa Wasomali, ambao ni wafugaji wa kuhamahama, Kijiji cha Koreni bado kimepiga hatua kubwa kimaendeleo, ambapo wakazi wanajivunia kuwa na shule ya Msingi ya Koreni na bwawa la kutibu mifugo.

Isitoshe, barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia imepita karibu na kijiji cha Koreni, hatua ambayo imeongeza hadhi ya kijiji hicho, hasa kimaendeleo.

Bw Ali Hassan, mkazi wa Koreni, anasema matumaini ya jamii ya Wakore kuendelezwa hata hivyo bado yapo kwani Mkore mmojammoja bado unaweza ukampata kwenye baadhi ya miji eneo hilo.

“Twafahamu kwamba Wakore bado wapo Lamu. Ukifika mahali kama Mokowe, utapata kuna Wakore, japo wachache wakiishi pale. Cha msingi ni kuwa Wakore wengi wanahisi kumezwa na Wasomali kupitia kukubali lugha, mila na desturi zao,” akasema Bw Hassan.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wa kiume watekwa na mashugamami

IEBC: Mswada wa kuajiri marefarii wa uchaguzi watua bungeni

T L