Jamila Mohamed amuenzi ‘Beloved’ Kipenzi Rita Tinina
NA JAMILA MOHAMED
KWA wengi waliomfahamu Rita, T9, RT, Yiapan, Maasai kama alivyotambulika na wenzake, maneno yanayoelezea kumhusu ni haya; alikuwa mtu wa kutegemewa.
Rita alikuwa mwanahabari ambaye kazi yoyote aliyopewa aliitekeleza kwa uwezo wake wote na hakufanya vitu hivihivi.
Kazi yake ilionyesha dhahiri umahiri wake.
Iwapo mhariri aliangalia hapa na pale kutafuta ni nani atakayetumwa kuandaa taarifa fulani, jina la Rita lilikuwa la kwanza kuitwa. Ni kwa sababu alikuwa tegemeo katika chumba cha habari.
Nilipata fursa ya kufanya kazi naye kwa miaka 10 katika runinga ya NTV, na katika muda huo wote, sikuona hata mara moja Rita akishindwa na kazi. Alikuwa na nidhamu kazini, mkarimu na mwenye mavazi ya kuvutia! Nakumbuka tukimtania kuhusu mavazi yake mazuri, tukisubiri ni lini atarudia nguo au viatu! Alikuwa akituangalia tu, akitabasamu na kusema, “mtangoja tu!”
Nakumbuka T9 alikuwa wa kwanza kuelekea jijini The Hague kuangazia kesi zilizokuwa zinaendelea huko. Alifika tu na saa chache baadaye tulikuwa na taarifa za Kiswahili na Kiingereza.
Mara nyingi aliporudi baada ya kukusanya taarifa, Rita alikuwa mwepesi wa kuanza kuandika taarifa hizo bila kupoteza wakati.
Kidogo ungemsikia akiniita: “Farah! Stori ndio hiyo, andika Kiswahili!”
Rita alifanya kazi yake kwa umahiri na kwa utaratibu uliofaa.
Tulipata fursa ya kuzunguka kaunti 47 naye tukifanya makala ya ‘Jarida la Jimbo’ au ‘The County Edition’.
Kwa wengi wetu tuliopata fursa ya kushiriki, ulikuwa wakati muhimu katika kazi yetu hii ya uanahabari. Tulikuwa tukiwasili katika kaunti na mara moja kila mmoja wetu anaenda njia yake kutafuta taarifa. Tunaporudi, Rita alikuwa akitusaidia sana kukamilisha kuandaa taarifa.
Tulikuwa tunamwita ‘editor’, kumaanisha mhariri wa picha. Alikuwa mmoja wa waandishi habari wa kwanza waliojifunza kuhariri kanda za video. Mara nyingi alikuwa akijitolea kusaidia ili wenzake tuweze kuendelea na shughuli nyingine. Safari hizo za kila Alhamisi au Ijumaa zitasalia kama kumbukumbu za siku zilizopita zenye furaha tele.
Mhariri wake Joe Ageyo alisema licha ya umaarufu aliokuwa nao, Rita alisalia kuwa mtu thabiti ambaye hakuruhusu mengine kuingilia kazi zake. Kwake, ilikuwa kazi kwanza. Lakini pia alikuwa mkarimu na alipenda kuwasaidia wenzake. Utawasikia wanahabari kadhaa wakisema aliwashika mkono katika chumba cha habari na kuwasaidia kupata mwelekeo.
Aliyekuwa mwanahabari wa biashara Stephen Kimani anasema “nakumbuka siku yangu ya kwanza nilipojiunga na NTV, Rita alikuwa wa kwanza kunialika niandamane naye kutafuta taarifa… alikuwa mtulivu na mwenye subira.”
Mwanahabari mwenzake Melita ole Tenges alisema T9 aliongoza na kuwafungulia wenzake njia katika taaluma hii.
Huyo ni Rita, kila aliyefanya kazi naye ana simulizi ya kuvutia.
Kwa familia yake, Rita alipendwa na wote waliotangamana naye. Aligusa mioyo ya wengi. Aliwashika mikono waliohitaji usaidizi, alikuwa mtulivu wa kusikiliza na kuongoza. Alikuwa wa kutegemewa na kutoa mwelekeo.
Pengo aliloacha halitakuwa rahisi kulijaza.
Buriani Rita… Mola akulaze palipo na wema!