JAMVI: Je, Uhuru anapanga kusalia na ushawishi baada ya 2022?
Na CHARLES WASONGA
PENDEKEZO lilitolewa na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael kwamba Rais Uhuru Kenyatta ataendelea kushikilia wadhifa wa Kiongozi wa chama hata baada ya kustaafu kama Rais 2022, linaashiria nia yake ya kuendelea kuwa na ushawishi serikalini baada ya kuondoka Ikulu.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa na uongozi sasa wanabashiri kuwa Bw Kenyatta akisalia kuwa kiongozi wa chama hicho huenda akaendelea kuongoza “kupitia mlango wa nyuma” endapo Jubilee, na muungano utakaoshiriki, utashinda katika uchaguzi mkuu ujao.
“Hali itakuwa hivyo hata kama Jubilee haitashinda katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu huenda itajipata nambari mbili na kuwa Chama Rasmi cha Upinzani, ikiwa pendekezo la mpango wa maridhiano (BBI) litapitishwa,” anasema Bw Martin Andati.
Ingawa Bw Tuju alifafanua kuwa hakuwa akiongea kwa niaba ya Rais Kenyatta, Bw Andati anasema kuwa wadhifa anaoushikilia katika chama hicho tawala ni wenyewe ushawishi mkubwa kiasi kwamba anachosema sharti kichukuliwe kwa uzito.
“Siongei kwa niaba yake (Rais) lakini sioni ni kwa nini asiendelee kuongoza chama cha Jubilee. Ningependa kusema kuwa kuna muafaka, haswa kutoka miongoni mwetu tunaoshikilia nyadhifa za uongozi chamani, kwamba Jubilee ingali inahitaji weledi wake wa kupalilia umoja katika taifa hili,” Katibu huyo mkuu akasema.
Miongoni mwa wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika katika Jubilee ni Bw David Murathe ambaye amewahi kusema waziwazi kwamba Rais Kenyatta atakuwa na wajibu mkubwa katika serikali ijayo “hata baada ya kuondoka afisini”.
Kauli kama hiyo iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli amewahi kudai “Rais bado ni kiongozi mwenye umri mdogo na hapaswi kustaafu.”
Huku akiunga mkono marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI), Bw Atwoli alisema hivi: “Ikiwa hatutaifanyia marekebisho katiba ili kubuniwe nyadhifa zaidi za uongozi mwafikiria Uhuru ataenda wapi ilhali bado umri wake ni mdogo. Sharti tufanyie mabadiliko katiba na ili tumweke mahali la sivyo ataanza kumsumbua kiongozi atakayechukua hatamu za uongozi,” akasema Bw Atwoli mnamo Mei 1, 2020 wakati wa sherehe za Leba Dei.
Kauli za Murathe na Atwoli zilichochea wapinzani wa muafaka kati Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, uliozaa BBI, kuibua madai kuwa lengo la msukumo wa mabadiliko ya Katiba ni kufanikisha mpango wa wawili hao kugawana mamlaka 2022.
Wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto wamekuwa wakidai kuwa mpango ni kumhakikisha cheo cha Rais kinamwendea Bw Odinga na kile cha Waziri Mkuu kinamwendea Bw Kenyatta.
Hata hivyo, Rais Kenyatta amekariri mara kadha mbele ya vyombo vya habari vya humu nchini na vilevile vya kimataifa kwamba yu tayari kupokezana mamlaka 2022 na kustaafu.
Rais na Bw Odinga wamesisitiza kuwa dhima kuu ya BBI sio kubuni nyadhifa za mamlaka kwa manufaa yao bali kupalilia umoja na utulivu nchini kwa kuzima ghasia ambazo hukumba taifa hili kila baada ya uchaguzi mkuu.
Ishara tosha
Lakini Bw Barasa Nyukuri anasema kuwa pendekezo la Bw Tuju ni ishara wazi kwamba Rais Kenyatta bado atakuwa na ushawishi mkubwa baada ya kustaafu endapo atasalia kuwa Kiongozi wa Jubilee.
“Endapo Jubilee inakumbwa na changamoto nyingi wakati huu, sidhani kama chama hicho kitasambaratika kabisa baada ya uchaguzi mkuu wa 2022. Kuna uwezekano mkubwa kwamba kitabuni muungano mwengine na ODM na vyama vingine vyenye maono sawa kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Na huenda mgombea wa urais atakayependekezwa na muungano huo ndiye ataibuka mshindi wa urais,” akasema mtaalamu huyu wa masuala ya uongozi.
Na endapo, muungano ambao utabuniwa na Jubilee utaunda serikali, Bw Nyukuri anaongeza, bila shaka Bw Kenyatta kama kiongozi wa mojawapo wa vyama tanzu katika muungano huo atakuwa na ushawishi mkubwa serikalini.
“Kwa kuwa BBI inapendekeza kuwa chama chenye wabunge wengi bungeni ndicho kitatoa waziri mkuu BBI ikipitishwa, kuna uwezekano mkubwa Bw Kenyatta atashawishi uteuzi wa afisa kama huyo ambaye atasimamia shughuli za kila siku za serikali,” mtaalamu huyo anaeleza.
Kauli ya Bw Nyukuri inapata mashiko katika kipengele cha tisa cha Katiba ya Jubilee kuhusu mamlaka ya kiongozi wake wa kitaifa. Kulingana na kipengele hicho, kiongozi wa chama ana mamlaka makuu ya kumpa mwelekeo kiongozi na kuhimiza uthabiti wa kisiasa chamani.
Kiongozi wa chama cha Jubilee, kwa mujibu wa kipengele hicho, pia ni mwenye mamlaka juu ya wanachama na maafisa wake na ndiye atakayeongoza mikutano yote ya Baraza Kuu la Kitaifa (NEC), Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) na Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa Jubilee (NDC).
“Kiongozi wa chama pia ndiye anaongoza mikutano ya Kundi la Wabunge (PG) na lile la Maseneta wa Jubilee kando na kuongoza mashauriano, mazungumzo na ushirikiano na vyama vingine au miungano ya vyama,” inasema Katiba hiyo.
Kwa hivyo, endapo Rais Kenyatta asalia kuwa Kiongozi wa Jubilee baada ya kustaafu 2022, ataendelea kujihusisha na shughuli za kila siku za chama hicho. Bila shaka atakuwa mamlaka makubwa katika chama hicho hata kuliko Rais, endapo mgombeaji wa Jubilee ndiye ataibuka mshindi.
Hali kama hii inashuhudiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) rais mstaafu Joseph Kabila anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Rais Felix Tshisekedi kwa kuwa kiongozi wa chama kikuu nchini humo. Hii ni kwa sababu chama cha Kabila kwa jina “Common Front for Congo” kilipata wabunge wengi kuliko kile cha Rais Tshisekedi, “Union for Democracy and Social Progress”.
Chama hicho cha Kabila kina jumla ya wabunge 342 kwenye bunge la DRC lenye viti 485. Na kulingana na Katiba hiyo nchini hiyo chama chenye wabunge wengi ndicho hutoa Waziri Mkuu, hali inayoakisi pendekezo la BBI.
Kwa hivyo, mshikilizi wa cheo cha Waziri Mkuu nchini DRC, Bw Sylvester Ilunga Ilukamba, anatoka chama cha “Common Front for Congo”, ambacho Bw Kabila anaendelea kukiongoza. Kando na kutoa mshikilizi wa wadhifa wa Waziri Mkuu, wafuasi kadhaa wa Kabila wameteuliwa katika baraza la mawaziri la serikali ya Tshisekedi.
Hali kama hii huenda ikashuhudiwa nchini Kenya endapo Rais Kenyatta ataendelea kushilikilia nafasi ya kiongozi wa Jubilee anavyopendekeza Bw Tuju.
Hata hivyo, wandani wa Dkt Ruto wamepuuzilia mbali pendekezo hilo wakisema kuwa Jubilee kitasambaratika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
“Rais hataongoza chochote kwa sababu sawa na PNU ya Kibaki, Jubilee ataporomoka na kuzikwa kwenye kaburi la sahau. Sisi kama wafuasi wa Naibu Rais tunapanga kubuni muungano mpya,” akasema Mbunge mmoja kutoka Rift Valley ambaye aliomba tulibane jina lake.