MakalaSiasa

JAMVI: ‘Jenerali’ kutua nchini bila gwaride wala fataki…

March 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

MWANASIASA wa Upinzani Miguna Miguna atarejea humu nchini Jumatatu huku kukiwa na dalili kwamba hatalakiwa kwa mbwembwe na wafuasi wa National Super Alliance (Nasa).

Umaarufu wa Dkt Miguna ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee ulididimia mara tu baada ya kinara wa NASA Raila Odinga kutangaza kuwa atafanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta wiki mbili zilizopita.

Dkt Miguna ambaye amejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la NASA, National Resistance Movement (NRM), alifurushwa na serikali kwa nguvu kutoka Kenya hadi Canada mwezi jana kutokana na madai kuwa hakuwa Mkenya.

Kabla ya kufurushwa, mwanaharakati huyo wa NASA alikamatwa na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi katika kaunti za Kiambu na Nairobi na kisha kufikishwa katika mahakama ya Kajiado baada ya siku tatu ambapo alifunguliwa mashtaka ya uhaini.

Bw Miguna ndiye aliapisha Bw Odinga kuwa ‘Rais wa Wananchi’ uwanjani Uhuru Park mnamo Januari 30, mwaka huu. Hata hivyo, serikali ilisisitiza kuwa kiapo hicho kilikuwa haramu na kisha kuwapokonya bunduki, paspoti na walinzi baadhi ya wanasiasa wa NASA huku vuguvugu la NRM likiharamishwa.

Tangu kusafirishwa nchini Canada kwa lazima, Dkt Miguna amekuwa akizunguka katika mataifa ya Amerika, Uingereza na Ujerumani ambapo amekuwa akihutubia makundi mbalimbali kuhusiana na hali ya kisiasa ya Kenya na yaliyojiri wakati wa uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26, mwaka jana.

“Machi 24, 2018, vuguvugu la NRM litakuwa jijini London, Uingereza kabla ya kutua jijini Nairobi Machi 26,” akasema Dkt Miguna.
Mwanaharakati huyo alitangaza kurejea wiki mbili baada ya Mahakama ya Rufaa kumwondolea vikwazo huku ikisema kuwa yuko huru kurejea.

Wafuasi wa NASA walimkumbatia DktMiguna na kumtaja shujaa alipojitokeza kukabiliana na serikali ya Jubilee huku akidai kuwa uchaguzi wa mwaka jana uligubikwa na dosari chungu nzima.

Lakini tangu Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, wafuasi wa NASA wameonekana kumtelekeza Miguna huku wengi wakiunga mkono hatua ya kiongozi wa Upinzani kukubali kushirikiana na serikali.

Wengi wa wafuasi wa NASA wamemchukulia Bw Odinga kama mpenda amani huku baadhi wakimwona kama msaliti kwa kuamua kushirikiana na serikali.
Bw Odinga pia ameonekana kujitenga naye tangu Miguna alipopasua mbarika kuwa baadhi ya maafisa wa NASA walipokea fedha za hongo kutoka kwa Jubilee kabla ya kuapishwa kwa Bw Odinga Januari 30.

Tangu Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta, Dkt Miguna amekuwa mkosoaji mkubwa wa kiongozi wa Upinzani huku akimtaja kuwa msaliti kwa wafuasi wake.

Amesisitiza kuwa vuguvugu la NRM litandelea kupigania haki katika masuala ya uchaguzi licha ya Bw Odinga ‘kujiunga’ na serikali.

“Kwa kukubali kufanya kazi na Rais Kenyatta ‘aliyemwibia’ ushindi wake, Bw Odinga amesaliti mamia ya Wakenya waliouawa na kuhataraisha maisha yao baada ya uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26,” akasema Dkt Miguna.

Mwanaharakati huyo pia alitangaza kuongoza maandamano katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia kesho ili kushinikiza kufanyika kwa mageuzi katika mfumo wa uchaguzi huku akisema kuwa: “ushindi haupatikani kwa kusalimiana (kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga) katika chumba cha mikutano katika afisi ya rais kwenye Jumba la Harambee.”

Dkt Miguna ambaye alibwagwa na Mike Sonko katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi wa Agosti 8, huenda akajizolea maadui zaidi; kutoka upande wa Jubilee na chama cha ODM atakaporejea kesho humu nchini.

Kulingana na aliyekuwa waziri na mwaniaji wa urais 2013, James Ole Kiyiapi, Dkt Miguna atakabiliwa na upinzani kutoka kwa Jubilee na ODM kutokana na mtindo wake wa kutaka kusema ukweli.

“Miguna Miguna anasema mambo ambayo wanasiasa hawataki kusikia uwe upande wa Jubilee au NASA. Miguna ni mwaminifu na ndiye kiongozi anayefaa kuongoza Kenya,” alisema Prof Kiyiapi.