MakalaSiasa

JAMVI: Kalonzo njia panda tena

December 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, anakabiliwa na wakati mgumu kudumisha uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga huku wandani wake wa kisiasa wakimshinikiza kuungana na Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Alhamisi, Bw Musyoka alijitenga na matamshi ya aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama aliyedai kuwa mazungumzo yameanza ya kiongozi huyo wa Wiper kuungana na Dkt Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na Bw Musyoka na chama chake, matamshi ya Bw Muthama yalikuwa ya kibinafsi na yalilenga kuvunja uhusiano wake na Rais Kenyatta.

“Kuhusu mjadala na uvumi kwamba ninapanga kuungana na naibu rais, ifahamike kuwa uvumi huu una nia mbaya. Ni juhudi za kuharibu uhusiano wangu na Rais na zimeshindwa,” alisema Bw Musyoka.

Alisisitiza kuwa chama chake hakijaamua mwelekeo mpya wa kisiasa akisema kingali mwanachana wa muungano wa NASA.

Na ingawa alijitenga na matamshi ya Bw Muthama, wadadisi wanasema kila dalili zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wake kuungana na Dkt Ruto.

“Hizi ni siasa. Kauli za washirika wake wa karibu na wa chama chake cha Wiper zinaonyesha kuwa ndoa yake ya kisiasa na vinara wa NASA iliingia doa. Anachotaka kuokoa ni uhusiano wake na Rais Kenyatta ambaye amempatia kazi ya kuwa balozi wa amani nchini Sudan Kusini,” asema mdadisi wa siasa Joseph Mulei.

Kulingana na Bw Muthama, alikuwa na ruhusa kutoka kwa Bw Musyoka kuongoza mazungumzo na kambi ya Dkt Ruto kuhusu ushirikiano wao kisiasa.

Kabla ya kutoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Bw Muthama alikuwa amekutana na wandani wa Dkt Ruto eneo la Ukambani ili kujadili jinsi viongozi hao wawili wangeweza kushirikiana kisiasa.

Ndani ya muda wa wiki mbili, Dkt Ruto alizuru eneo la Ukambani mara mbili kufanya mikutano ya kuchangisha pesa na duru zinasema amepanga ziara zaidi eneo hilo katika juhudi za kuimarisha umaarufu wake.

Wadadisi wanasema Bw Muthama hangefichua kuwepo kwa mipango ya Dkt Ruto na Bw Musyoka kuungana iwapo haingekuwepo.

“Nahisi alichofanya Bw Muthama ni kuifichua mapema au ilikuwa ni mbinu ya kupima hewa. Ikiwa aliifichua mapema, basi Bw Musyoka hakuwa na budi kujinasua ili kudumisha uhusiano wake na Rais Kenyatta ikizingatiwa kuwa uhusiano wa kiongozi wa nchi na naibu wake umeonekana kuwa baridi,” aeleza Bw Mulei.

Mwaka jana, Bw Muthama alisema Bw Musyoka ataungana na wanasiasa wengine kuunda muungano mpya wa kisiasa ambao ungeunganisha Wakenya. Wakati huo alisema muungano huo ungekuwa wa vigogo wa kisiasa waliounga handisheki ambayo Dkt Ruto na wandani wake walikuwa wakipinga.

Kulingana na mwanasiasa huyo, kilichomchochea Bw Musyoka kuanza mazungumzo na Dkt Ruto ni kusalitiwa na washirika wao katika miungano ya kisiasa ya sasa.

Bw Musyoka alikuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga katika NASA na kulingana na mkataba wa muungano huo, kiongozi huyo wa ODM angemuunga mkono kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, Bw Odinga amebadilisha mkondo wake wa kisiasa na hata kukumbatia mahasimu wa Bw Musyoka eneo la Ukambani magavana Dkt Alfred Mutua (Machakos), Kivutha Kibwana (Makueni) na Charity Ngilu (Kitui).

“Kwa kukumbatia magavana hao, ilikuwa wazi kwa wandani wa Bw Musyoka kwamba hana nafasi katika muungano wa kisiasa ambao utatokana na handisheki ingawa yeye mwenyewe anaiunga mkono.

“Hii ndiyo sababu waliamua kuanza mazungumzo na Dkt Ruto ambaye anakabiliwa na upinzani katika Jubilee,” asema mbunge mmoja wa chama cha Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu ya uhusiano wake na Bw Musyoka.

Bw Mulei anakubaliana na Bw Muthama kwamba baada ya Bw Odinga kukumbatia magavana wa Ukambani ambao wamekuwa wakimpiga vita Bw Musyoka, makamu rais huyo wa zamani hakuwa na budi ila kubadilisha mkondo wake wa kisiasa pia.

“Kizingiti kwa sasa, na ilidhihirika katika ujumbe wake wa kujitenga na matamshi ya Bw Muthama, ni uhusiano wake na Rais Kenyatta na washirika wake ambao wamewekea visiki Dkt Ruto hasa kwa kutokumbatia handisheki,” aeleza Bw Mulei.

Kulingana na katibu mkuu wa Wiper Judith Sijeny, matamshi ya Bw Muthama hayafai kuchukuliwa kama msimamo wa chama hicho.

“Chama hakijachukua msimamo kuhusu vyama au viongozi ambao kitashirikiana nao kuelekea 2022. Wiper kingali sehemu ya NASA na kwa hivyo, Bw Muthama sio msemaji wa chama,” alisema Bi Sijeny.

Hata hivyo, duru zinasema kuwa kumekuwa na presha kutoka kwa vigogo wa chama Bw Musyoka ajitenge na Bw Odinga na kuungana na Bw Mudavadi, Wetangula na Dkt Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Hisia za wanaomshinikiza Bw Musyoka kuungana na viongozi hao ni kuwa Bw Odinga sio wa kuaminika kwa sababu aliwasaliti alipokosa kuwahusisha katika mazungumzo yake na Rais Kenyatta na kwa kukiuka mkataba wa NASA.

“Kuna hisia kwamba Dkt Ruto naye amesalitiwa na Rais Kenyatta kwa kukosa kumwidhinisha kuwa mrithi wake. Huu ndio msimamo wa Muthama na wanaotaka muungano huo,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Hata hivyo, anasema Bw Musyoka anahisi kwamba ni mapema mno kuchukua msimamo kabla ya mchakato wa kutelekeza ripoti ya Jopokazi la maridhiano (BBI) kukamilika.

“Kumbuka Bw Musyoka ameunga BBI na inaweza kubadilisha mfumo wa serikali. Anachofanya kwa wakati huu ni kuwa mwangalifu katika kila hatua anayochukua. Kwa kawaida yake, huwa anachukua muda kabla ya kufanya uamuzi,” anaeleza.