MakalaSiasa

JAMVI: Karata ya Ruto kuhusu BBI yaanikwa

October 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto ameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa Wakenya wanakataa baadhi ya mapendekezo ya ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), imebainika.

Wandani wa Naibu wa Rais waliambia ukumbi huu kuwa mtego wao wa kwanza ni ‘kuteka nyara’ mswada wa sheria itakayotoa mwongozo kuhusu namna ya kuendesha kura ya maamuzi.

Mswada huo tayari umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni. Mbunge wa Ndaragwa, Bw Jeremiah Kioni ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Katiba (CIOC) alisema kuwa mswada huo utawasilishwa kwa mara ya pili ili ujadiliwe na wabunge mwezi huu.

Baada ya kujadiliwa na wabunge, kamati ya CIOC itaalika Wakenya kuwasilisha maoni yao na kisha kuandaa na kupeleka ripoti yake ya mwisho bungeni.Japo ripoti ya mwisho ya BBI haijawekwa wazi, inatarajiwa kupendekeza mabadiliko ya Katiba ambayo yatahitaji kura ya maamuzi.

Ripoti ya mwisho ya jopokazi la BBI inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kabla ya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, Oktoba 20.

Miongoni mwa mabadiliko ambayo yamezua tumbojoto miongoni mwa wapinzani wake ni upanuzi wa serikali ili kujumuisha wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake wawili.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga wiki iliyopita alidokeza kuwa kura ya maamuzi huenda ikafanyika Aprili mwaka ujao.Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa anasema kuwa wabunge wanaounga mkono Dkt Ruto, almaarufu Tangatanga, watashinikiza kujumuishwa kwa kipengele ambacho kitahakikisha kuwa kila suala linalohitaji kubadilishwa kwenye Katiba linapigiwa kura.

“Tutahakikisha kuwa Wakenya hawatapiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘la’ kama ilivyofanyika mwaka wa 2005 na 2010. Badala yake tunataka Wakenya wapate fursa ya kupigia kura kila suala linalohitaji kubadilishwa. Kwa mfano, Wakenya watapiga kura kuamua ikiwa wanahitaji kuwepo kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka au la.

“Baadaye, watachukua karatasi ya pili na kupiga kura kuamua ikiwa wanahitaji fedha zinazotolewa kwa serikali za kaunti ziongezwe au la. Kwa kufanya hivyo, tutahakikisha kwamba Wakenya wanachagua tu masuala wanayotaka na kutupilia mbali wasiyoyahitaji,” anasema Bw Barasa ambaye pia ni mwanakamati wa CIOC.

Mbunge huyo anasema kuwa Wakenya wangali wanahisi makali ya janga la virusi vya corona hivyo hawatakubali kupanuliwa kwa serikali ili kuwezesha wanasiasa wachache kujipa nyadhifa.

Mikokoteni

“Janga la virusi vya corona limesababisha Wakenya kupoteza ajira na biashara zao. Hivyo, wafadhili wa BBI watakuwa na kibarua kigumu kushawishi Wakenya kuunga mkono kupanuliwa kwa serikali ili kuwezesha wachache kujipatia nyadhifa serikalini,” anasema Bw Barasa.

“Ikiwa wanataka BBI kupenya itabidi wajumuishe mambo yanayohusu mwananchi wa kawaida kama vile bodaboda, waendeshaji wa mikokoteni, na kadhalika. Kukiwa na mambo hayo tutaunga mkono BBI,” anaongezea Bw Barasa.

Iwapo watashindwa kupenyeza kipengele hicho kwenye mswada huo, mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany anasema kambi ya Ruto imejiandaa kuendesha kampeni za kupinga BBI.

“Kwa sasa Naibu wa Rais anaungwa mkono na wabunge 150. Kikosi chetu kimekamilika na tuko tayari kuendesha kampeni kote nchini kupinga BBI,” anasema. “Tuna uwezo wa kufanya mikutano miwili katika kaunti zote 47 kwa siku.”

Wandani wa Naibu wa Rais pia wanaamini kuwa wamefanikiwa kubadili mwenendo wa siasa nchini kwa kuwagonganisha walalahoi dhidi ya mabwanyenye ambao wamekuwa wakidhibiti siasa za humu nchini.

“Tumefanikiwa kuondoa suala la ukabila ambalo limekuwa kwenye siasa za nchi hii kwa muda mrefu. Kwa sasa ni walalahoi dhidi ya mabwanyenye. BBI haiendi popote,” akasema Bw Barasa.

Wandani wa Rais Kenyatta pia wanasubiri kwa hamu na ghamu matokeo ya kesi iliyowasilishwa kortini na wanaharakati; mwanauchumi David Ndii, Jerotich Seii, James Ngondi na Wanjiku Gikonyo na Ikal Angelei kupinga mabadiliko ya Katiba.Iwapo mahakama itasitisha mabadiliko ya katiba, basi itakuwa afueni kwa Tangatanga.

Wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wameanza kuhofia kuwa huenda wakawa na wakati mgumu kushawishi Wakenya kuunga mkono BBI iwapo Naibu wa Rais ataruhusiwa kuendelea kuendesha kampeni.Wanaamini kuwa Naibu wa Rais anachochea Wakenya dhidi ya BBI.

Wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wanapanga kuanza msururu wa kampeni ili kuzima wimbi la Naibu wa Rais.Chama cha ODM chake Bw Odinga kimepanga kuanza kampeni ya kuhakikisha kuwa Ruto hapenyi katika ngome zake katika eneo la Pwani, Nyanza na Magharibi.