• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Amejiokoa au kujimaliza? Sababu zitakazomfanya Mwangaza kuwa UDA kwa jina tu

Amejiokoa au kujimaliza? Sababu zitakazomfanya Mwangaza kuwa UDA kwa jina tu

TANGAZO la Gavana wa Meru Kawira Mwangaza kwamba amejiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) limefasiriwa kama mkakati wake mpya wa kupunguza joto la kisiasa linaloendelea kumwandama katika kaunti hiyo.

Gavana huyo ameendelea kukumbwa na hali ngumu kisiasa kuponea mara mbili kutimuliwa afisini baada ya Seneti kutupilia mbali hoja zilizopitishwa katika madiwani wa Meru.

Hii ni baada ya juhudi zake za kupalilia uhusiano mzuri na Naibu wake Isaac Muruma, madiwani 69, wabunge tisa na Seneta wa Kaunti hiyo Kathuri Murungi kugonga mwamba.

Kwa mfano, wakati wa ziara ya Rais William Ruto katika kaunti ya Meru Januari mwaka huu, Gavana Mwangaza alizomewa vikali katika eneo la Igembe.

Eneo hilo lenye idadi kubwa ya watu ndiko anakotoka Bw Mutuma, ambaye alitofuatiana na bosi wake mwaka jana kufuatia madai kuwa alikuwa miongoni mwa “waliodhamini” hoja ya kumtimua Mwangaza afisini.

Ilimlazimu Rais Ruto kuingilia kati kutuliza kundi la vijana walimpigia kelele Gavana Mwangaza katika kituo cha kibiashara cha Muringene, eneo bunge la Igembe ya Kati.

Baadaye gavana huyo alielekeza kidole cha lawama kwa mbunge wa eneo hilo Dan Kiili na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi aliodai ndio waliwakodisha vijana hao kumzomea mbele ya rais.

Kanusha madai

Bw Kiili, ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza alikana madai hayo akiyataja kama yasiyo na msingi wowote.

Baada ya tukio hilo Gavana Mwangaza alikatiza ziara zozote katika eneo hilo, ambalo pia linashirikisha maeneo bunge ya Igembe Kaskazini na Igembe Kusini, akidai mahasidi wake wa kisiasa walitishia maisha yake. Amerejea huko juzi tu.

Aidha, kiongozi huyo aliwahi kunukuliwa akidai kuwa wanasiasa hao ndio walijaribu kumhusisha na mauaji ya kinyama ya mwanablogu Daniel Muthiani, almaarufu ‘Sniper’ “ili wakazi wanichukie zaidi.”

Hata hivyo, kakake Mwangaza, Murangiri Kenneth Guantai ni miongoni mwa wale waliotuhumiwa kwa muaji hayo ya Desemba 2023, lakini hamna ambaye amepatikana na hatia kufikia sasa. Wiki jana, Gavana Mwangaza alipata pigo jingine kisiasa baada ya mradi wake wa kugawa ng’ombe wa maziwa kwa familia masikini kuzimwa na madiwani wa kaunti ya Meru.

Sakata

Kamati ya bunge la kaunti hiyo kuhusu Kilimo na Ufugaji lilizima ufadhili kwa mradi huo wa thamani ya Sh67 milioni wakiutaka kama “sakata kubwa ya ufisadi”.

Akiwasilisha ripoti yake katika Bunge la Kaunti ya Meru, mwenyekiti wa kamati hiyi Ken Naibae aliongeza kuwa waligundua kuwa mradi huo umekuwa ukitekeleza kinyume cha sheria na bila uwazi.

“Tuligundua kuwa mchakato wa kutambua familia za kufaidi, ununuzi wa ng’ombe hao na usambazaji wao uliendeshwa bila sera wala mfumo wowote wa kisheria ilhali mradi wenye unafadhiliwa kwa pesa za umma,” Bw Naibae akanukuliwa akisema kabla ya madiwani kupiga kura ya kupitisha ripoti hiyo.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Nelson Mutungi anasema haya ni miongoni mwa sababu zilimfanya Gavana Mwangaza kutangaza kujiujnga na UDA.

“Gavana sasa ameng’amua kuwa uwezekano wa yeye kuridhiana na wanasiasa ni finyu mno. Mradi wake ambao ungemwongezea uungwaji mkono miongoni mwa rais masikini pia unapigwa vita na madiwani,” anasema.

“Hii ndio maana sasa amekimbilia UDA kujitakasa kisiasa ikizingatiwa kuwa wakati wengi wanakishabikia chama hicho,” anaongeza.

Sheria haimruhusu kujiandikisha rasmi

Hata hivyo, mchanganuzi huyo anasisitiza kuwa japo Bi Mwangaza ametangaza kujiunga na UDA, kisiasa, masaibu yake hayataisha hivi karibu kwani hajaridhiana na viongozi wa Meru.

“Akidiriki kujihusisha moja kwa moja na masuala ya chama hicho, kama vile uchaguzi wa mashinani, huenda akapata upinzani kutoka kwa viongozi halisi UDA kama vile Seneta, wabunge na madiwani,” Dkt Mutungi anaeleza.

Kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Vyama Vya Kisiasa ya 2022, Gavana Mwangaza hajajiunga na UDA kwa hofu kwamba akifanya hivyo atapoteza kiti chake.

Kipengele cha 85 cha Katiba ya sasa kinatoa nafasi kwa mtu yeyote kuwania kiti chochote cha kisiasa kama mgombeaji huru mradi asiwe mwanachama wa chama chochote cha kisiasa miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Mtu kama huyo atapoteza nafasi hiyo endapo atajiunga na chama cha kisiasa hata baada ya kushinda wadhifa huo.

Na kulingana na sehemu ya 14 ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2024 mwanasiasa atapoteza nafasi yake endapo atavumisha sera na misimamo ya chama cha kisiasa ambacho hakikumdhamini uchaguzini.

Hitaji la sehemu ya sheria hii pia linawaathiri walioshinda viti kama wagombeaji huru kisha wakajiunga na vyama vya kisiasa kabla ya kukamilika kwa mihula yao.

Hii ndio maana Gavana Mwangaza hawezi kudhubutu kujiandikisha rasmi kama mwanachama wa UDA na kupewa nambari ya uanachama.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaambia Uhuru: Tumia ile afisi ya Kibaki lau sivyo...

Sheria mpya kulainisha utoaji leseni kaunti zote

T L