Jamvi La Siasa

Baada ya muda nitakuanika kwa Wakenya, Gachagua aambia Ruto

Na MWANGI MUIRURI December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua, Jumapili usiku Desemba 1, 2024, alitangaza kuwa atafichua mengi kuhusu Rais William Ruto kwa Wakenya, akisisitiza kuwa walitofautiana kwa sababu alikuwa akiuliza maswali kuhusu sera kandamizi jambo ambalo lilimkasirisha kiongozi wa nchi.

Bw Gachagua alisema sasa anaelewa ni kwa nini rais wa zamani Uhuru Kenyatta alikataa kumuunga mkono Dkt Ruto (ambaye alikuwa naibu wa Kenyatta tangu 2013) katika kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 2022.

Bw Gachagua ambaye alitofautiana na Bw Kenyatta na kuongoza timu ya wanasiasa Mlima Kenya kumuunga mkono Dkt Ruto, aliteuliwa kuwa mgombea mwenza na kusaidia Ruto kuzoa asilimia 87 ya kura za eneo hilo.

Lakini baada ya Gachagua kumtumikia Dkt Ruto kama naibu rais kwa miaka miwili, alitimuliwa Oktoba 17, 2024 na nafasi yake ikachukuliwa na Prof Kithure Kindiki.

Sasa, Bw Gachagua anasema hajuti kumuunga mkono Dkt Ruto kwa kile anadai alipata funzo, japo linaumiza.

“Nina furaha sasa kwamba yeye (Rais Ruto) amekuja kuthibitisha mambo mengi mabaya ambayo Bw Kenyatta alikuwa akituambia faraghani kuhusu Naibu wake, nilikuwa nikitilia shaka masuala yaliyoibuliwa, lakini sivyo tena,” alisema.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa kwenye mahojiano na mtangazaji wa NTV Ibrahim Karanja, Desemba 1, 2024. Picha|Evans Habil

Bw Gachagua alisema kuwa sasa ana furaha kwamba amemfahamu Rais Ruto.

“Yeye si mtu ambaye ninaweza kuthubutu kushughulika naye kama Mkristo, nikipewa nafasi nyingine ya kuzungumza naye, nitashughulika naye kama mwanasiasa, alinipa nafasi ya kutumikia, kumjua zaidi, kupata uzoefu na sasa kuendelea mbele, nitahakikisha watu wa Kenya wanajua yeye ni nani,” Gachagua alisema.

Akizungumza kwenye mahojiano ya NTV, Bw Gachagua, ambaye alipuuza tamko la hivi majuzi la serikali kwamba uchumi umeimarika, alimshutumu vikali rais kwa kuendesha serikali kwa ulaghai.

Alisema utawala wa Rais Ruto una mwaka mmoja pekee kujikomboa.

Alimsifu kiongozi wa Chama cha Wiper Bw Kalonzo Musyoka ambaye alimtaja kama “mwanamume ambaye tunaweza kufanya kazi naye, tuko kwenye mazungumzo, hakika hatuna tatizo kufanya kazi naye.”

“Rais ana takriban mwaka mmoja tu kufanya jambo, uchumi hauendi anavyosema…uliza watu na utapata majibu,” alisema.

Bw Gachagua alisema serikali haihitaji kutangaza kwamba uchumi unaendelea vizuri kwa vile ni watu wanaofaa kuripoti kwa kuthibitisha kwamba wanaweza kuhisi athari za uchumi bora.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA