‘Baba’ anaweza? Ushindi wa Mutharika, 85, waibua gumzo kuhusu Raila 2027
BAADA ya ushindi wa babu Peter Mutharika, 85, katika uchaguzi mkuu wa Malawi, gumzo limezuka iwapo Kinara wa ODM Raila Odinga, 80, anastahili kuwania urais wa Kenya.
Bw Mutharika, ambaye amewahi kuhudumu kama rais wa Malawi sasa atarejea ikulu baada ya rais wa sasa Lazarus Chakwera kukubali kushindwa Jumatano.
Mnamo 2019, Mutharika alimshinda Chakwera lakini uchaguzi huo ukafutiliwa mbali na mahakama kutokana na udanganyifu mkubwa ulioshuhudiwa.
Chakwera ambaye wakati huo alikuwa akishabikiwa sana na kuonekana kama wa kuleta uongozi bora, alishinda marudio ya kura na akawa rais.
Jumatano, Chakwera alikiri kushindwa na kumpigia simu Mutharika kumpongeza. Wadadisi wanasema alianguka kutokana na kutotimiza ahadi na sera zake hasi za kiuchumi.
Kufikia wakati ambapo atatamatisha muhula wake, Mutharika atakuwa ametinga umri wa miaka 90.
Ukongwe wake umewashaajisha baadhi ya wafuasi wa Raila mitandaoni kuwa bado nyapara huyo wa upinzani, anaweza kujaribu bahati yake na kuwania urais kwa mara ya sita.
Kiongozi huyo wa ODM atakuwa na umri wa miaka 82 na miezi minane wakati ambapo uchaguzi wa 2027 utakuwa ukifanyika.
Kushaajishwa huku kunatokana na hali kwamba baadhi ya mataifa kama Cote d’ivoire wana marais ambao wamehitimu zaidi ya umri wa miaka 80. Rais Alassane Ouattara wa Cote d’ivoire ana umri wa miaka 83.
Mnamo Jumanne, Bw Odinga aliwaonya wabunge wa ODM dhidi ya kumfanyia kampeni Rais William Ruto, wengi wakikisia kuwa huenda amepiga abautani na analenga kujaribu bahati yake tena 2027.
“Bado hatujapitisha chochote kuhusu jinsi ambavyo uchaguzi wa 2027 utakavyokuwa. Kwa hivyo msiwekee chama masuala mengine ambayo hayajajadiliwa,” akasema Bw Odinga kwenye mkutano na kundi la wabunge wa ODM.
“Wacha mambo hayo yajadiliwe kwanza. Sisi ni ODM, nani aliwaambia ODM haitakuwa na mwaniaji mwaka wa 2027?” akauliza.
ODM tangu Juni mwaka jana imekuwa kwenye ukuruba wa kisiasa na UDA baada ya vyama vyote viwili kuingia kwenye mkataba wa maelewano.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuwa kama ODM, msimamo wa chama kuhusu uchaguzi huo ni jambo ambalo litajadiliwa baadaye.
Raila amewania uchaguzi wa urais mara tano (1997, 2007, 2013, 2017 na 2022) lakini hajawahi kufua dafu mara nyingi akitilia shaka matokeo yanayotangaza na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC).
Kwa upande mwingine, Wakenya wengine nao wanaona kushindwa kwa Chakwera kama onyo kwa Rais Ruto kuwa asipotimiza ahadi, atahudumu muhula moja pekee.