Baba ya Raila, Jaramogi alipokera Amerika
Uhusiano unaozidi kuimarika kati ya Kenya na China umeibua wasiwasi mkubwa nchini Amerika, hali inayokumbusha jinsi Jaramogi Oginga Odinga alivyokera nchi hiyo miaka ya 1960 kwa ujasiri wake wa kushirikiana na mataifa ya Kikomunisti.
Mnamo Mei 1964, Jaramogi, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani, aliongoza ujumbe wa Kenya katika ziara ya mataifa ya Mashariki — China na Urusi. Akiwa pamoja na Joseph Murumbi, aliyekuwa Waziri wa Nchi katika afisi ya Waziri Mkuu, walizuru Beijing (iliyofahamika kama Peking) kwa ziara ya siku nane.
Walipokelewa kwa heshima kuu na viongozi wakuu wa Chama cha Kikomunisti cha China, akiwemo Mao Tse-Tung, Liu Shao-Chi na Waziri Mkuu Chou En-Lai. Mazungumzo ya kidiplomasia yaliendeshwa kwa kina na hatimaye wakafikia makubaliano kuhusu msaada mkubwa wa kiuchumi kwa Kenya.
Katika makubaliano hayo, China ilitoa ruzuku isiyo na masharti ya pauni milioni 1.07 kusaidia Kenya kurekebisha nakisi ya bajeti, hasa katika kulipa wanajeshi wa Jeshi la Kenya, mkopo wa pauni milioni 5.3 usio na riba, kwa kipindi cha miaka mitano, uliolenga kufadhili miradi ya maendeleo ya viwanda na kilimo.China pia iliahidi kutuma wataalamu wa kiuchumi na kiufundi kusaidia katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mikopo hiyo ilikuwa na masharti nafuu na Kenya ingeanza kulipa kuanzia Januari 1975, kwa kutumia bidhaa za kigeni au pesa zinazokubalika na pande zote mbili. Kwa Amerika na Uingereza, huu haukuwa tu msaada wa kawaida, bali njia ya China kujipenyeza barani Afrika na kuongeza ushawishi wake katika mataifa changa yaliyokuwa yakitafuta mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi.
Katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa Beijing, ambapo zaidi ya watu 1,500 walihudhuria, Jaramogi alitoa hotuba kali akishambulia ukoloni na ukoloni mamboleo:
“Sasa kwamba tuko huru, hatupaswi kufumbia macho kwa njama za kiuchumi kutoka kwa mabeberu wanaotaka kututawala kupitia uchumi wetu.”
Akizungumzia mgogoro wa Congo, Jaramogi alilalamikia jinsi rasilimali za Afrika zilivyonufaisha mataifa ya Magharibi badala ya Waafrika wenyewe:
“Amerika ina ukoloni mamboleo mbaya zaidi. Utajiri wa Congo unatumiwa kuwanufaisha mabepari wa Amerika badala ya kuwasaidia Waafrika maskini.”
Matamshi haya yaliwagusa vibaya maafisa wa Amerika na Uingereza, ambao walihofia kwamba Kenya ingeangukia mikononi mwa mataifa ya Kikomunisti.
Baada ya Jaramogi kusaini mikataba hiyo, Jesse MacKnight, afisa mwandamizi wa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, alimwita Mkuu wa Ubalozi wa Uingereza mjini Washington. Alieleza masikitiko ya Amerika kwamba Waingereza, licha ya kuwa na ushawishi mkubwa Kenya, hawakuwa wakizuia ushawishi wa China na Urusi.
Kwa mujibu wa stakabadhi za kidiplomasia zilizofichuliwa baadaye, Amerika ilitaka Waingereza wachukue jukumu la ‘kuokoa Kenya’ dhidi ya ushawishi wa kikomunisti. Mmoja wa wanadiplomasia wa Kiingereza aliandika katika waraka wa siri:
“Tunatumaini kwamba Wamarekani hawatamshambulia Kenyatta au mawaziri wake moja kwa moja, na tunapaswa kuwa tayari kuwazuia iwapo itahitajika.”
Uingereza ilimtuma H.S.H Stanley, Kaimu balozi wa Uingereza Nairobi, kuonana na Mzee Jomo Kenyatta na kufikisha malalamishi ya nchi hizo. Hata hivyo, Kenyatta aliepuka miadi hiyo kwa siku kadhaa, akitambua mgogoro ulionukia kati ya rafiki yake Jaramogi na mataifa ya Magharibi.
Baada ya juhudi za mara kwa mara, Stanley aliweza kukutana na Kenyatta mnamo Mei 14, 1964. Katika kikao hicho, Kenyatta alisema hakuwa amesoma hotuba ya Jaramogi na hakuwa na maoni rasmi. Aliongeza:“Sitaki kutoa maoni nyuma ya mgongo wa Odinga kwa sababu huenda hakuripotiwa ipasavyo.”
Aliahidi kuzungumza naye akiwasili kutoka ziara yake ya Mashariki.
Amerika ambayo ilikuwa imeghadhabishwa sana na matamshi ya Jaramogi na msaada wa China, iliagiza mabalozi wake Dar es Salaam, Kampala na Zanzibar kutathmini athari za ushawishi wa Kikomunisti Afrika Mashariki. Katika taarifa ya siri iliyotumwa London, afisa wa Uingereza aliandika:
“Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika inahitaji tathmini ya kina ya athari za msaada huu kwa maslahi ya Magharibi, mipango ya maendeleo ya Kenya, na ushawishi wake kwa nchi jirani kama Uganda na Tanganyika.”
Hofu kuu ya Amerika ilikuwa kwamba misaada ya aina hiyo ingetumiwa kueneza propaganda na kuwezesha ujio wa wataalamu wa Kikomunisti katika maeneo nyeti ya Afrika.
Katika moja ya mikutano yao, MacKnight alieleza mwenzake wa Uingereza:
“Wakubwa wangu wanaitegemea Uingereza ichukue uongozi wa kudhibiti hali hii. Hatutaki kuona Kenya ikiangukia mikononi mwa China na Urusi.”
Kufuatia shinikizo hizo za kisiasa na kidiplomasia, miradi mingi ya maendeleo ambayo Jaramogi alikuwa ameandaa haikuwahi kutekelezwa. Mikopo ya China na Urusi ilizuiwa katika ngazi mbalimbali, huku wakuu wa serikali wakilazimishwa kubadili misimamo yao kupitia shinikizo za kifedha na kisiasa kutoka kwa mataifa ya Magharibi.
Kwa wataalamu wa historia, tukio hili linaonyesha jinsi siasa za kimataifa, hasa wakati wa Vita Baridi, zilivyoathiri mwelekeo wa mataifa changa kama Kenya. Jaramogi alikuwa na maono ya kuweka Kenya huru kiuchumi, lakini hali ya dunia ilimweka njia panda.