Cherargei motoni tena kwa kusherehekea madhila ya Njagi na Oyoo
KWA mara nyingine Seneta wa Nandi Samson Cherargei amekemewa kwa kusherehekea kutekwa nyara na kuteswa kwa wanaharakati wa Bob Njagi na Nicholas Oyoo nchini Uganda kwa muda wa siku 38.
Kile kilichowakera wengi ni kwamba mwanasiasa huyo ambaye ni mtetezi sugu wa serikali ya Rais William Ruto alitoa kauli hiyo ndani ya kanisa moja mjini Kapsabet, kaunti ya Nandi; taasisi ambayo inapaswa kupinga visa vya ukiukaji haki za kibinadamu.
Cherargei aliitia shime Uganda na nchi zingine jirani akizitaka kupambana vikali wanaharakati kutoka Kenya kabla ya kuwarejesha Kenya wadhulumiwe zaidi.
“Wafinye kabisa hawa watu… kisha warudishe nyumbani tuwamalizie,” Cherargei akasema Jumapili iliyopita, akaonekana akiziambia serikali za Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mwenzake wa Uganda Samia Suluhu Hassan.
Licha ya kushambuliwa vikali na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, kiongozi wa chama cha Democracy for Citizen Party (DCP) Rigathi Gachagua na uongozi wa kanisa alikotoa kauli hiyo, Jumanne wiki hii Seneta huyo alishikilia kuwa hajuti kutoa kauli hiyo.
“Bado nasisitiza kuwa Museveni alifanya vizuri kwa kufinya Bob Njagi na Nick Oyoo walienda nchini mwake kusababisha fujo. Hakuna sheria inayoruhusu yeyote kuingi nchi nyingine kuchochea maandano,” Cherargei akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.
Awali, mnamo Jumatatu, Bw Gachagua alimsuta vikali Cherargei akimtaja kama kiongozi asiye na utu.
“Huyu Cheragei anafaa kufahamu kwamba akina Bob Njagi ni raia wa jumuiya ya Afrika Mashariki na wako na kibali kuzuru taifa lolote wanachama. Cherargei awe na utu, kesho ni mtu kutoka jamii yake atatekwa nyara Uganda na kuteswa. Je, atasherehekea hatua kama hiyo?” akauliza.
Kwa upande wake Bi Martha Karua alidai kuwa matamshi ya Cheragei ni ithibati kwamba serikali ya rais William Ruto inashirikiana na zile za Museveni na Samia kuendeleza ukatili dhidi ya watetezi wa haki na kibinadamu na utawala bora.