Jamvi La Siasa

DCP kujivumisha zaidi Pwani baada ya kulambishwa sakafu Magarini

Na ANTHONY KITIMO December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

BAADA ya chama kinachohusishwa na aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua cha DCP kupoteza katika uchaguzi mdogo wa Magarini, chama hicho kitaanzisha kampeni kabambe eneo la Pwani kikilenga uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Gachagua amedai kuwa chama cha ODM hakina sababu ya kujigamba kushinda katika uchaguzi huo mdogo kwani chama chake hakijamaliza hata mwaka tangu kibuniwe.

“Ningependa kupongeza Bw Stanley Kenga kwa kuibuka wa pili katika uchaguzi wa November 27. Tulionyesha umahiri kwani chama cha ODM kimekuwa katika siasa kwa muda. Kura tulizopata ni dhahiri kuwa Bw Kenga alijitahidi mno,” alisema Bw Gachagua kwa taarifa mtandaoni.

Hata hivyo, Bw Gachagua amesema chama hicho kitaanzisha mchakato wa kusajili wanachama wapya Pwani ilikujiandaa kwa chaguzi zijazo.

“Nitashinda Pwani wakati wa likizo kusajili wanachama wapya na kufungua ofisi za chama katika maeneobunge mbalimbali ili kusaidia kuuza sera za chama hicho,” alisema Bw Gachagua.

Katika eneo la Pwani, mbunge wa Nyali Mohammed Ali ndiye mbunge wa pekee anayetarajiwa kutumika kujaribu kuvunja ngome za ODM Pwani kwani naye ana kibarua kujaribu kupenya Kaunti ya Mombasa kwani ametangaza azma yake ya kuwania ugavana.

Bw Ali ni mbunge wa pekee katika Kaunti hiyo Kati ya wabunge sita ambaye hakuchaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM.

Japo hajatangaza chama atakachowania kiti hicho cha ugavana, mkutano wake wa hivi karibuni na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ni dhihirisho anamezea mate tiketi ya Wiper.

Katika uchaguzi mdogo uliofanyika wiki iliyopita, ODM kupitia mgombeaji wao Bw Harry Kombe iliibuka mshindi kwa kura 17,909 huku mpinzani wake wa karibu Bw Stanley Kenga akipata kura 8,907.

Katika uchaguzi uliopita, Bw Kombe alishinda kwa kura 11,946 dhidi ya mpinzani wake Bw Kenga ambaye alipata kura 11,925.

Bw Kenga alijiunga na DCP baada ya kudinda kushurutishwa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kupitia chama cha UDA.

Bw Kenga alisema hatajutia kamwe uamuzi wake kuingia DCP na kumpa nafasi ya kugombea ubunge wa Magarini.

Hata hivyo, wakazi wasema ushindi mkubwa ulioshuhudiwa wa Bw Kombe ulitokana na kuungwa mkono kwa ODM na chama tawala cha UDA pamoja na kile cha PAA kinachoongozwa na Spika wa Seneti Amason Kingi.

Hatua hii ilimpa nguvu Bw Kombe na hivyo kushinda kwa kura nyingi katika uchaguzi huo mdogo.

Mbali na hilo, kukosekana kwa Bw Gachagua katika kampeni za Magarini kumetajwa kuwa chanzo cha Bw Kenga kupata kura chache.

“Licha ya Bw Kenga kugombea kwa ctiketi ya hama cha DCP, Bw Gachagua hakujitokeza kumpigia debe kwani alionekana akitilia mkazo uchaguzi wa Mbeere Kaskazini,” asema Bw Hajji Karissa, mkazi wa Magarini.

Hata hivyo, chama cha ODM kimesema hakuna chama kingine kinachoweza kubadili wakazi kwani hicho chama ndicho kinajali maslahi yao.

Gavana wa Mombasa ambaye pia ni naibu kinara wa ODM Abdulswamad Nassir alisema katika uongozi wake, “Uchaguzi wa Magarini sisi hatukuongea sana. Tulionyesha kwa vitendo na hivyo ndivyo hali itakuwa siku za usoni. Pwani ni ngome ya Chungwa na hakuna chama kitaweza kubadili hilo,” alisema Bw Nassir.

Licha ya hayo, ndoa ya ODM na UDA katika Serikali Jumuishi inaonekana kuendelea kugawanya chama hicho kote nchini kwani UDA imetumia ushirikiano wao kudhoofisha ngome za ODM.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, UDA ilijizolea zaidi ya asilimia 40 za kura zote eneo la Pwani jambo ambalo lilionekana si la kawaida kwani kwa miaka 15 kabla uchaguzi huo, ODM imekuwa ikiongoza kwa kura zaidi ya asilimia 85.

Uchaguzi mdogo uliopita ulivutia wagombeaji 10. Baadhi ya walioshiriki walipata kura chini ya 300 kila mmoja.

Bw Furaha Ngumbao Chengo wa chama cha DNA alipata kura 227 naye mgombeaji mchanga zaidi kwa umri katika kinyang’anyiro hicho Bw Amos Katana aliyekuwa mgombeaji huru alipata kura 182.

Sarah Wahito Gakahu, mwanamke wa pekee alipata kura 12 huku mgombea wa chama cha Federal Party of Kenya Jacob Themo akipata kura 70.

Mgombeaji wa Roots Party Bw Hamadi Karisa alipata kura 138.

Bw Emmanuel Kalama wa chama cha The We Alliance Party (TWAP) naye alipata kura 60 huku Kasisi John Sulubu Masha wa Kenya Social Congress akijizolea kura 10 pekee.