Gachagua aanzisha misafara Mlima Kenya, amwambia Ruto ajiandae kuonana naye 2027
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ameweka wazi kuwa atawania urais mwaka wa 2027 kwa lengo la kumwangusha Rais William Ruto, ambaye sasa anamlaumu kwa “kumsaliti na kumfedhehesha” machoni pa taifa.
Akiwahutubia wakazi wa Karatina katika Kaunti ya Nyeri mwishoni mwa wiki, Gachagua alitangaza rasmi kuwa amerudi nyumbani kuanzisha vuguvugu la kisiasa litakalounganisha Mlima Kenya na kuondoa utawala wa sasa ambao aliutaja kuwa wa ukandamizaji na uliojaa vitisho.
“Nimerudi kutoka Amerika nikiwa na nia moja – kuomba msamaha kwa kosa la 2022 la kuwalazimishia Ruto na pia kupata baraka zenu za kuwania urais 2027. Nitamrithi Ruto,” alisema Gachagua huku akishangiliwa na umati.
Bw Gachagua alikosoa vikali utawala wa Rais Ruto akisema unatumia mbinu za kiimla, vitisho na ufisadi kugawanya Mlima Kenya, ili kudhibiti kura za eneo hilo kupitia siasa za “gawanya utawale”.
“Ruto anadhamini wanasiasa wawili kutoka Murang’a kuanzisha chama cha kisiasa ili kunipokonya ushawishi wa Mlima. Hizi ni njama za kutugawanya ili tupoteze kura zetu kama ilivyotokea 2002,” aliongeza.
Gachagua pia alidai kuwa Rais Ruto na washirika wake walihusika katika kuvuruga mapokezi yake ya kurudi nchini kutoka Amerika mnamo Agosti 21, 2025.
Alisema alilazimika kufuta maandalizi ya kupokewa JKIA na mkutano mkubwa Kamukunji kutokana na vitisho vya kukamatwa na kutokea kwa vurugu.
“Nilitarajia kukaribishwa kwa heshima na wafuasi wangu lakini njama za kisiasa zilikatiza mpango huo. Hii ni ishara wazi kuwa kuna wale wanaogopa sauti ya wananchi,” alisema.
Katika ziara yake ya kaunti za Murang’a, Kiambu na Nyeri, Gachagua alieleza malengo yake manne makuu: kuunganisha Mlima Kenya, kulea viongozi wa kizazi kijacho, kushirikiana na maeneo mengine ya nchi na kumng’oa Rais Ruto madarakani kwa njia ya kidemokrasia.
Akiwa Kenol, Murang’a, Gachagua alitaja mbinu tano anazodai kuwa Rais Ruto anatumia kudhoofisha upinzani katika eneo hilo:Kutoa hongo kwa viongozi wa Mlima Kenya; kudhamini wagombea wengi wa urais kutoka eneo hilo ili kugawanya kura, kuwanyima vijana vitambulisho, kuwahangaisha viongozi wa eneo hilo kupitia kwa kesi na kukamatwa, kuendeleza utekaji, mauaji ya kiholela na visa vya kutoroshwa kwa mabavu.
Gachagua alisema kuwa Mlima Kenya haupaswi kugawanywa tena, na kwamba ni wakati wa eneo hilo kujiamulia hatima yake.
Wakati huo huo, serikali kupitia msemaji wake Isaac Mwaura imemtaka Gachagua na wafuasi wake kuacha siasa za migawanyiko na badala yake kumuunga Rais Ruto katika juhudi za kuleta maendeleo.
Hata hivyo, Gachagua alipuuzilia mbali kauli hiyo akidai kuwa “maendeleo ya kweli hayawezi kuletwa kwa mbinu za hongo, urafiki wa kisiasa na njama za kisaliti.”
Ameahidi kuendelea na ziara zake katika maeneo mengine ya Mlima Kenya na baadaye kupeleka kampeni zake pembe nyingine za taifa.
“Tutawaondoa wote wanaoshirikiana na serikali hii ya mateso, kuanzia Rais hadi wasaidizi wake. 2027 ni mwaka wa ukombozi wa wananchi,” alisema akiwa Mukuyu mnamo Jumamosi.